24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NAIBU WAZIRI AONYA UVUVI HARAMU

Na TUNU NASSOR-PWANI


 

NAIBU Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Abdallah Ulega, amewataka wavuvi nchini, waache uvuvi haramu kwa kuwa unasababisha madhara yakiwamo uuaji wa mazalia ya samaki.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kisiju, Wilaya  ya Mkuranga, mkoani Pwani, Ulega alisema atakayekiuka agizo hilo, atashughulikiwa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Hatutakuwa na huruma kwa mvuvi yeyote atakayejihusisha na uvuvi haramu, tutakayemkamata, tutamshughulikia kikamilifu na adhabu kali itachukuliwa dhidi yake.

“Natambua asilimia kubwa ya wakazi wa kata hii wanategemea uvuvi na kilimo cha korosho, hivyo kuendekeza uvuvi haramu iko siku watakosa mazao ya samaki kutokana na kuua mazalia.

“Katika hili, ieleweke kwamba, hakuna aliyekatazwa kuvua, lakini kama Serikali tumesema ugomvi wetu ni yule anayevua kwa njia haramu, yaani, huyo ndiye tutakayeshughulika naye,” alisema Ulega.

Aliwataka washirikiane kwa pamoja katika kuhakikisha Wilaya ya Mkuranga inapiga hatua za kimaendeleo kama ilivyo wilaya nyingine nchini.

“Nimekuwa nikipokea simu zikidai kuwa nimekataza kuvua samaki, hivi nimekataza wapi, nilichokataza ni uvuvi haramu na tutashughulika na wavuvi haramu wote,”alisisitiza Ulega.

Wakati huo huo, Ulega alifika katika Visiwa vya Koma na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa zahanati na kuona ujenzi wa zahanati hiyo ulipofikia kwa kuwa alishiriki uazishwaji wake.

Baada ya kushuhudia ujenzi huo, alichangia saruji na mabati ya kuezekea.

Akiwa ameongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo pamoja na viongozi mbalimbali, Ulega aliwahimiza viongozi waendelee kuwahamasisha wananchi ili waendelee kujitolea ili kufikia maendeleo ya haraka.

Wakati huo huo, Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu  Vullu (CCM), alichangia mifuko 50 na marumaru kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo na maeneo ya kujihifadhi watoto wa kike shuleni.

Katika Zahanati ya Kijiji cha Kisiju pia alichangia mifuko 20 ya saruji na kuahidi kuendelea kuchangia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles