27.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

TPA YANUNUA VIFAA VYA KISASA BANDARI YA MTWARA

Na Mwandishi Wetu-MTWARA


MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imenunua vitendea kazi vipya na vya kisasa kwa ajili ya bandari ya Mtwara ili kuongeza ufanisi.

Vifaa hivyo ambavyo tayari baadhi vimeshawasili bandarini hapo ni pamoja na mzani wa kisasa ‘Movable Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 ambao tayari unatumika.

Vifaa vingine vilivyonunuliwa na vinavyotarajiwa kuwasili kuanzia mwezi huu ni pamoja na ‘Reach Stalker’ mbili mpya zenye uwezo wa kubeba tani 40 kwa wakati mmoja.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa majumuisho ya ziara za Kamati za Bodi za Wakurugenzi wa TPA zinazoshughulikia Tehama na Utelekezaji na ile ya Uwekezaji na Maendeleo ya Biashara.

Wakurugenzi wa Bodi za Kamati hizo ambazo ziliongozwa na Mwenyekiti, Dk. Jabiri Bakari ni pamoja na Jayne Nyimbo, Renatus Mkinga, Aziz Kilonge na Jaffer Machano.

Kamati hizo zilitembelea miradi mbalimbali iliyopo bandari za Mtwara na Lindi na kutoa maelekezo kadhaa ambayo ni muhimu katika kuendeleza bandari hizo ili kuongeza huduma zake.

Akizungumzia vifaa vipya vilivyowasili na vinavyotarajiwa kuwasili hivi karibuni, Mhandisi Kakoko alisema ununuzi wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa mipango ya kuifanya bandari hiyo kuwa ya kisasa zaidi.

“Ununuzi wa vifaa tunaofanywa sasa hivi utasaidia kuboresha na kuimarisha zaidi utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara na kuongeza ufanisi zaidi,” alisema Mhandisi Kakoko.

Licha ya hali hiyo, alisema vifaa vingine ambavyo mchakato wa manunuzi umeshafanyika ni pamoja na mzani mwingine wa pili wa kisasa ‘Movable Weigh Bridge’ wenye uwezo wa kupima hadi tani 100 pia.

Amevitaja vifaa vingine kuwa ni pamoja na boti maalumu za kuhudumia mafuta ‘Mooring Boat’ moja na boti moja ya ulinzi ‘Pilot Boat’.

Mbali ya vifaa hivyo, Bandari ya Mtwara pia itapokea ‘Terminal Tractors’ 9; matrekta maalumu yanayovuta ‘matrela’ yaliyopakiwa kontena au makontena yakiwa bandarini.

Bandari ya Mtwara pia inatarajia kupokea mashine maalumu ya kubebea makontena ‘Empty Container Handler’, folklift mbili moja ya tani 16 na nyingine tani 20 pamoja na ‘Automatic Glab moja ya tani 15.

Kama sehemu ya ziara hiyo, Mhandisi Kakoko pia alifanya kikao na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mtwara na kuwaagiza kukutana na Mawakala wa Forodha wa Mtwara ili kuwaelimisha umuhimu wa kutoa mizigo ya wateja kwa wakati.

Awali akitoa maelezo kwa Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi wa TPA inayoshughulikia Tehama na Utelekezaji, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA (Miundombinu), Mhandisi Karim Mattaka, alisema vifaa hivyo vitawasili Bandari ya Mtwara kuanzia mwezi ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles