Na Koku David, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amekitaka Chuo cha Kodi (ITA) kufanya utafiti pamoja na kuwapa mbinu bora wahitimu wake ili kukuza mapato.
Aliyasema hayo juzi katika hotuba yake iliyosomwa na na Kamishna wa Sera za Ununuzi wa Umma kutoka wizara hiyo Dk Fredrick Mwakibinga wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kutunuku vyeti wahitimu 389.
Alisema ufinyu wa wataalamu wa masuala ya kodi, umekuwa ukiikosesha serikali mapato hivyo ITA inatakiwa kufanya utafiti zaidi ili kupata mbinu bora za ukusanyaji kodi hususani kodi ya majengo.
“Kuna mabadiliko makubwa katika sekta hii hivyo mfumo wa kodi ili uwe sahihi unahitaji watalaamu hawa, ITA inatakiwa kuangalia namna ya nzuri ya kuboresha mifumo ya kodi ya majengo pamoja na kupitia utafiti,” alisema Dk. Mwakibinga.
Alisema uzoefu unaonyesha kuwa serikali imekuwa ikipoteza mapato kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ukwepaji kodi hivyo wataalamu hao kupitia utafiti, watasaidia kutoa ushauri wa namna nzuri ya kukusanya kodi.
Naye, Profesa Isaya Jairo alisema chuo hicho kinatarajia kuanzisha mafunzo ya masafa ya mbali kwa kutumia mtandao ili kutoa fursa kwa wanaohitaji elimu ya kodi, ushuru na mapato.
Alisema katika matokeo ya utafiti walioufanya mafunzo kwa wahitimu wanaotoka katika chuo hicho iwapo watayatumia vizuri, yatafanikisha ukusanyaji wa kodi na kuwezesha mapato ya serikali yanayokusanywa wa TRA kuongezeka.
“Kutokana na umahili wa chuo chetu tumekuwa tukitoa mafunzo kwa wanafunzi kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika na ukanda wa Afrika Mashariki, na kwamba kiliteuliwa kuwa kituo cha umahiri kuhusu masuala ya ushuru na kodi kwa ukanda huo,” alisema Profesa Jairo.
Alisema chuo hicho kimesaini makubaliano na nchi ya Sudan Kusini, kutengeneza mpango kazi wa ushuru, kodi na mapato katika mamlaka ya nchi hiyo.
Katika mahafali hayo ya 13 ya chuo cha ITA, jumla ya wahitimu 389 walitunukiwa vyeti katika ngazi ya shahada, stashahada na astashahada.