24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

IMF yatoa ahadi nzito kwa Rais Magufuli

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Idara ya Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Abebe Selassie, amesema shirika hilo litatuma timu ya wataalamu wake kuja nchini ili kupitia maeneo yote yaliyoainishwa katika matazamio ya ukuaji wa uchumi.

Kauli ya mkurugenzi huyo wa IMF, imekuja baada ya hivi karibuni taarifa ya shirika hilo kuvuja huku ikitaja ukuaji wa uchumi wa Tanzania kuwa ni asilimia 4 kwa mwaka huu kutoka asilimia 6.6 mwaka 2018.
Kutokana na hilo, Sellasie jana alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Mimi na Rais Magufuli tumekubaliana kuwa IMF na Tanzania watabaki kuwa wadau wanaoaminiana, tunaona fursa nyingi na muhimu katika nchi hii ikiwemo mipango mizuri ambayo Rais Magufuli ameianzisha.

“Katika wiki zijazo tutaendelea na mazungumzo na kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania na tutaleta timu ya wataalamu watakaokuja kujadiliana na Serikali ya Tanzania ili kutazama maeneo yote yaliyofanyiwa mageuzi makubwa na kuyawianisha na ukuaji wa uchumi,”alisema Selassie.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwahakikishia Watanzania kuwa wizara yake imejipanga kutoa ufafanuzi wa maeneo yote ambayo yanapaswa kuwemo katika taarifa ya IMF ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi.

“Ili uchumi wa nchi ukue ni lazima uwe unawekeza na bahati nzuri Rais Magufuli amemweleza mgeni wake jinsi tunavyowekeza kwenye miundombinu hususani ujenzi wa reli ya kati, jinsi tunavyowekeza katika ujenzi wa bwawa kubwa litakalotupatia megawati 2,100 za umeme na miradi ya barabara na viwanda vingi vilivyojengwa, haya ndiyo yanayokuza uchumi na sisi tunaamini kabisa wenzetu hawakuyazingatia kabisa katika taarifa ya awali (iliyovuja),”alisema Dk. Mpango.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi aliwatoa hofu wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuendelea kuwa na imani na mazingira ya uwekezaji ya Tanzania.
“Nashukuru kwamba hata wawekezaji wenyewe hawana hofu kwani hata baada ya taarifa hiyo kuwa imevujishwa bado wengi wameendelea kuja na kuonesha nia ya kufanya kazi na sisi na nashukuru IMF kwa kuja kuzungumza na sisi.

“Hii ni dalili kuwa shirika hili bado lipo nasi na bado tunaendelea na mazungumzo, wale ambao walidhani pana ugomvi mkubwa kati ya IMF na Tanzania walikuwa wamekosea kabisa na msimamo wa Tanzania utafahamika baada ya mazungumzo kuanza na kuweza kuwapitisha katika miradi mikubwa ya maendeleo inayofanyika,”alisema Profesa Kabudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles