29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mwinyi amzungumzia Mengi

CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

MAMIA ya waombolezaji wakiongozwa na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, jana waliendelea kufika nyumbani kwa marehemu Dk. Reginald Mengi, Ada-Estate, Kinondoni kuendelea kuifariji familia yake.

Mwinyi akitoa pole, alisema Mengi alikuwa mkarimu wa nafsi na mali zake pia.

Alisema kuondoka kwake ni pigo kwa familia na taifa kwa ujumla kwakuwa kila chake kilikuwa ni cha jamii nzima.

“Hadi anaondoka duniani alikuwa anagawana na Watanzania wenzake bila kubagua…leo ametutoka pole mno kwa familia na jamii,” alisema  Mwinyi.

Alisema hata maandiko matakatifu yanasema anayekosa na kurejea kuomba msamaha anatakiwa asamehewe.

“Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe msamaha, pale alipokosea katika maisha yake ya kutafuta asamehewe,” alisema Mwinyi.

Naye, Mwenyekiti Msaidizi wa Bodi ya Parole Taifa, Clemence Munisi, alisema yupo tayari kutoa eneo lake la kiwanja lililopo nyuma ya Bamaga Sinza kwa lengo la kujenga mnara wa kumbukumbu ya Dk. Mengi.

Alisema matendo aliyoyafanya yanagusa jamii, hivyo ameshauri Serikali ijenge mnara huo na endapo litakosekana eneo, yupo tayari kutoa lake.

Kwa upande wake, Waziri wa zamani wa Mazingira, Thelesa Huvisa, alisema alifanya kazi na Mengi ambaye alipanda miti mingi nchini.

Alisema Mengi alitetea nchi hii hadi nchi nyingine za Afrika ambapo hewa inayovutwa hapa nchini imechagizwa na yeye.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani, Michael Danford, alisema wameguswa na kifo cha Mwenyekiti huyo Mtendaji wa Kampuni za IPP.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasiiona Tanzania, Louis Benedict, alisema marehemu alikuwa na mahusiano makubwa na chama hicho.

Alisema watakosa mambo mengi ambayo Mengi aliwaahidi ikiwamo kuendeleza taasisi yake ya Dk. Mengi Foundation.

“Sauti yake ya ‘yes we can’ bado inapenya katika masikio yetu, nasi tutaendelea kuyaishi maisha yake kwa vitendo, walioachiwa urithi wa mali zake waendelee kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu,” alisema Benedict.

Pia, Mwanasheria Methusela Gwajima alisema alikutana na marehemu Wilaya ya Nzega mkoani Tabora alikofika kwa lengo la kusaidia vikundi vya kijamii.

Alisema Mengi alikuwa mtu wa kujishusha na alikuwa mtu wa kawaida.

“Ametuacha na fundisho maisha ni mafupi kadiri mtu anavyopanda kimaisha na kubarikiwa, tujitahidi kutoa kwa wengine,” alisema Gwajima.

Alisema Dk. Mengi ni nembo ya upendo na ushirikiano hivyo ni vyema tukayaishi maisha yake.

Mwenyekiti wa Shule ya Msingi Regnald Mengi, iliyopo Sinza, Twaha Chigeka alisema marehemu aliwajengea uzio katika shule hiyo na kuwapa Sh milioni 100 hivyo amefanya makubwa kwao.

Alisema kutangulia kwake iwe ni mfano kwa wengine kusaidia jamii.

Baadhi ya watu mashuhuri waliohudhuria ni pamoja na Waziri mstaafu wa Fedha, Cleopa Msuya, Mbunge wa Chadema Easter Matiko na aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles