25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Ilala kuja na kampeni ya kutokomeza ‘ziro’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Kata ya Ilala inatarajia kuanza kampeni ya kutokomeza sifuri ili kuongeza ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne.

Hatua hiyo inafuatia baada ya uongozi wa kata hiyo kubaini kuwapo kwa ongezeko kubwa la wanafunzi wanaopata sifuri katika mtihani wa kidato cha nne licha ya baadhi yao kufanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba.

Akizungumza wakati wa kukabidhi samani za viti na luninga kwa walimu wa Shule za Msingi za mkoani na Boma, Diwani wa Kata ya Ilala, Saad Khimj, amesema shule hizo kila mwaka zimekuwa zikitoa watoto wanaopata wastani wa alama A lakini matokeo ya kidato cha nne hayaridhishi.

“Matokeo ya kidato cha nne hayafanani na mwamko wanaotoka nao darasa la saba kuingia kidato cha kwanza, kuna sehemu tunakosea msingi tunafanya vizuri lakini sekondari hali si nzuri. Tuige mfano wa Wilaya ya Kisarawe ambayo imepata mafanikio makubwa baada ya kuja na kampeni ya kutokomeza ziro,” amesema Khimj.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Almasi Kasongo, akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Boma luninga kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Kushoto ni madiwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Naye Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ambaye alikuwa mgeni rasmi, Almasi Kasongo, alikubali kuwa mwenyekiti wa kamati ya kutokomeza ziro na kwamba atahakikisha kata hiyo inapiga hatua katika sekta zote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Karume, Haji Bechina, amewataka wazazi na walezi kushirikiana na walimu kuhakikisha wanafuta sifuri katika mtihani wa kidato cha nne.

Akizungumzia msaada huo alioutoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, amesema mtaa wa Karume unalea shule hizo na walimu waliomba kusaidiwa samani na luninga ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo msaada huo unaohusisha viti 100, luninga mbili (nchi 40 kila moja) na ving’amuzi viwili una thamani ya zaidi ya Sh milioni 7.

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Boma, Theopista Almasi, amesema kwa miaka mitano shule hizo zimekuwa zikifanya vizuri kitaaluma na kuwa katika kumi bora za wiaya kwa mitihani ya darasa la nne na saba.

Aidha ameshukuru kwa msaada huo kwani mwenyekiti huyo pia amekuwa akisimamia mpango wa lishe ambapo wanafunzi wote wanapata uji na chakula cha mchana, wakati wa mitihani ya taifa pamoja na kuwapatia ndoo za maji tiririka na vitakasa mikono.

Hata hivyo amesema shule hizo zinakabiliwa na changamoto za kukosa uzio na kusababisha kuingiliwa kwa mipaka ya shule na wanajamii hivyo wanafunzi kukosa maeneo ya kuchezea pamoja na vijana wanaotumia mihadarati kuvamia eneo la shule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles