23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

CCM Tabora wapanda miti 2,000 kuokoa mazingira

Na Allan Vicent, Tabora

KATIKA kusherekea miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Viongozi na wanachama wa chama hicho mkoani Tabora wameshiriki zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali ili kuepusha uharibifu wa mazingira.   

Akizungumza kwenye sherehe ya uzinduzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika Kimkoa leo Jumapili Januari 30, 2022 katika viwanja vya shule ya msingi Ilege, kata ya Ilege wilayani Kaliua, Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Solomon Kasaba alisema wamepanda miti hiyo ili kuunga mkono juhudi za serikali za kulinda mazingira.

Amesema shamrashamra za maadhimisho hayo zilianza Januari 23, mwaka huu kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji miti ambapo zaidi ya miche 2,000 imepandwa katika wilaya zote za mkoa huo.

Amesisitiza kuwa zoezi la upandaji miti ni endelevu na litakuwa likifanyika mara kwa mara katika wilaya zote za Mkoa huo chini ya usimamizi wa Wataalamu wa Mazingira ili kulinda uoto wa asili katika maeneo yote ya Mkoa huo.

Kasaba alibainisha shughuli nyingine zilizofanywa na wana-CCM wa Mkoa huo kuwa ni kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, vituo vya kutolea huduma za afya, kutembelea na kusaidia watu wenye mahitaji maalumu na kushiriki ujenzi wa nyumba za watumishi wa chama.

Alitaja mambo mengine kuwa ni kushiriki zoezi la uchangiaji damu kwa hiari na kupima afya ikiwemo kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na kuelimishwa juu ya umuhimu wa kujikinga na ugonjwa huo.    

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Nzega Amos Kanuda alipongeza mshikamano mzuri wa Viongozi na Wana-CCM wa Mkoa huo ambao umekifanya chama hicho kuendelea kuaminiwa na wananchi wote.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora Mjini Mohamed Katete aliwataka wanaCCM na jamii kwa ujumla kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini ili kuepusha machafuko na uhasama unaoweza kugharimu maisha yao.

Diwani wa Kata ya Ilege (CCM) ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua, Jafael Lufungija aliwashukuru Viongozi wa Chama ngazi ya Mkoa kwa kuwaamini na kuwapa fursa ya kuandaa sherehe za uzinduzi wa maadhimisho hayo Kimkoa ambayo yatahitimishwa Februari 3, 2022 mjini Tabora. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles