26.1 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

IGP SIRRO AMTANGAZIA KIAMA MANGE KIMAMBI

NA RAYMOND MINJA IRINGA


MKUU wa Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amesema jeshi lake linaendelea na upelelezi juu ya taarifa za mwanaharakati wa mitandao ya kijamii anayeishi Marekani, Mange Kimambi, kuwakejeli na kuwatukana viongozi wa nchi kwenye mitandao.

Akizungumza na wanahabari katika  ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Sirro alisema. “Kwenye kazi hii ya upelelezi huwezi kuweka kila kitu wazi, tunajua (Mange) anavunja sheria za nchi, tunafanya nini, siwezi kusema,” alisema.

Sirro ametoa msimamo huo baada ya hivi karibuni, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema hawatavumilia vitendo vinavyofanywa na Kimambi pamoja na kundi lake.

Katika taarifa hiyo, Boaz alisema jeshi hilo litawasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola watu wanaoshirikiana na mwanaharakati huyo kutoa taarifa za uongo, uzushi, matusi na kejeli kwa viongozi wa nchi.

Sirro alikuwa mjini Iringa jana katika mwendelezo wa ziara zake za kufanya ukaguzi wa jeshi hilo na kuzungumza na maafisa wa polisi, askari na kamati ya ulinzi na usalama wa mikoa mbalimbali.

Katika hatua nyingine, IGP Sirro alisema jeshi hilo litaendelea na jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao ikiwa ni pamoja na kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahalifu wote wakiwemo wale wasiojulikana.

“Kumekuwepo na changamoto ya matumizi ya neno hili. kimsingi Watanzania wanatakiwa kujua mtu anafanya tukio akiwa hajulikani na anapopanga kufanya uhalifu huo haji polisi kutoa taarifa kwamba nataka kufanya uhalifu,” alisema.

IGP Sirro aliwataka askari polisi wafanye kazi kwa kuzingatia maadili na haki ili wananchi walio katika maeneo yao waendelee kuishi kwa amani na utulivu na waendelee kuliamini jeshi hilo.

Aliwataka wananchi wanaohitaji msaada wa askari na kuukosa kwa sababu ya makosa yanayofanywa na askari hao, watoe taarifa hizo kwa viongozi wa juu wa jeshi hilo au wengine wa serikalini ili wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua.

“Hakuna askari polisi aliyepo juu ya sheria, akitenda kosa tunataratibu zetu za kumshughulikia, anafukuzwa kazi na kupelekwa mahakamani,” alisema.

Pia  IGP Sirro alisema kumekuwa na tatizo la ubakaji watoto wa umri wa mdogo katika maeneo mbalimbali nchini kwasababu ya imani za kishirikina.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna kazi kubwa ya kutoa elimu kwa watu  wanaofanya vitendo hivyo viovu. “Huwezi kupata utajiri kwa kubaka watoto,” alisema.

Aliwaomba viongozi wa dini wasaidie kutoa elimu hiyo katika nyumba za ibada ili jamiii iweze kubadilika na kuona vitendo hivyo havikubaliki mbele ya wanadamu na mbele ya Mungu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles