IGP Sirro afunguka mazito

0
542

Na Asha Bani -Dar es salaam

MKUU wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, amesema tatizo ndani ya jeshi hilo ni unafiki na kusisitiza mwenye wadhifa alionao yupo mmoja tu.

Hayo aliyasema jana wakati akifungua kikao kazi kwa makamishna, makamanda wa mikoa, vikosi na maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Alisema ana muda mchache wa kukaa katika kiti hicho, hivyo  wale wanaoona hafai nafasi hiyo wasubiri kidogo kwani wakati wao ukifika na wao wataweza kuchukua madaraka mbalimbali ndani ya jeshi hilo.

“Tatizo linalotusumbua sisi Jeshi la Polisi pia ni unafiki. ‘There is no way’ tukawa na IGP zaidi ya mmoja, mimi sikujichagua.

“Kamanda wa Kinondoni unanisikia (Mussa Taibu)? Kubali yaishe, sikujiteua mwenyewe, siwezi kujiona kama sitoshi katika nafasi hii.

“Natamani kumaliza nafasi yangu Jeshi la Polisi likiwa na heshima yake. Jeshi hili likiharibika tumeharibikiwa wote, na mimi siwezi kumuwekea mtu kinyongo, mie sio wa aina hiyo, kwa hiyo niwaombe ushirikiano,” alisema IGP Sirro.

Alipoulizwa kuhusu kauli ya IGP Sirro, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Taibu, alisema kuwa anafikiri kwamba alitumia jina lake kama njia ya kufikisha ujumbe kwa watu waliorushiwa kombora hilo.

“Hakika hii ni nondo kwa watu waliopigwa hapa, na kunitaja mimi ilikuwa ni njia tu ya kufikisha ujumbe kwa baadhi ya watu. Na ujumbe kwao umefika vema,” alisema Kamanda Taibu.

IGP Sirro aliteuliwa Mei 28, mwaka juzi kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Ernest Mangu aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda.

“Sina ubaya na askari yeyote na najua nikimuwekea mtu kinyongo nitakosa raha kwani hii ni kazi ya utumishi wa umma, leo nipo kesho sipo, kinachotakiwa ni kufuata mwongozo na utekelezaji wa kanuni za Jeshi la Polisi,” alisema IGP Sirro.

Mbali na hayo, IGP Sirro alisema bado jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kumomonyoka maadili katika utendaji wa kazi pamoja na kudhoofu kwa utekelezaji wa  mpango mkakati wa jeshi la polisi.

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, IGP Sirro aliwataka askari polisi kuongeza umakini katika utendaji wao wa kazi kuelekea uchaguzi huo.

Hata hivyo alikumbusha vifo vya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa Februari 17, mwaka jana wakati wa maandamano ya wafuasi wa Chadema kwenda kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni kudai viapo vya mawakala.

Katika maandamano hayo inaelezwa kuwa polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakiandamana.

Mbali na hilo, pia IGP Sirro alizungumzia kifo cha mwanahabari Daudi Mwangosi, ambaye alifariki dunia kwa kulipuliwa na bomu Septemba 2, 2012 katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi wakati wa ufunguzi wa tawi la Chadema.

 “Mkutano huu utakuwa ni kujipanga kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Ndugu zangu mtakumbuka kesi ya Akwilina na Mwangosi.

“Sasa tunakwenda katika uchaguzi, hauwezi kupuuza, ili uweze kwenda vizuri lazima kuwa na mpango mkakati wa kuzuia na kupambana na wale watakaoleta uhalifu wa kuvuruga,” alisema IGP Sirro.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa umakini zaidi ikiwa pamoja na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na amani iliyopo inaendelea kudumu.

RUSHWA POLISI

IGP Sirro aliwataka makamanda wa polisi wa mikoa na vikosi vya jeshi hilo kujiepusha na vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu pamoja na kushiriki kikamilifu kuunga mkono jitihada za Serikali kufanikisha Tanzania ya viwanda.

Alisema wapo baadhi yao wachafua sifa ya jeshi hilo jambo ambalo ni lazima lipingwe ili kuendelea kulinda hadhi yao.

IGP Sirro alisema lazima Jeshi la Polisi liendelee kulinda usalama wa raia na mali zao na hatarajii kuona linakuwa chanzo cha migogoro kati yake na wananchi.

“Kuna baadhi ya askari polisi bado wanaendeleza vitendo vinavyoashiria kuomba rushwa kwa wenye kutenda makosa na hasa barabarani.

“Jeshi la Polisi halitaki kuona rushwa kwa watumishi wake na hivyo wenye tabia ya kujihusisha na rushwa waache mara moja,” alisema.

Aliwataka makamishna na makamanda wote wa polisi nchini kuhakikisha wanasimama kidete kukomesha rushwa na kuwataka kila mmoja kwa nafasi yake kukemea vitendo hivyo.

“Kuna askari polisi wanachukua rushwa hadharani wanaposimamisha mabasi na ninyi makamanda wa mikoa mpo,” alisema.

Pia aliwataka makamishna na makamanda wa mikoa kuwaandaa askari vijana ambao watashika nafasi zao ili wao kurejea makao makuu kwa utungaji wa sheria na ushauri.

“Ni vyema kuwa na damu changa itakayoweza kufanya kazi kwa nguvu zaidi kuliko kung’ang’ania nafasi hizo za ukamishna,” alisema.

SARE ZA POLISI

Pia IGP Sirro alitolea ufafanuzi kuhusu sare za jeshi hilo akisema kila sare ivaliwe sehemu yake husika na kwa tukio maalumu.

“Utamkuta askari mkubwa amevaa sare za mapambano, amezivaa sehemu ambayo si husika kama vile kwenye mikutano ya vyombo vya habari au amevaa akiwa ofisini akifanya kazi za utendaji, vazi lile halitakiwi katika shughuli kama hizo,” alisema.

IGP Sirro aliwashangaa pia baadhi ya askari kutojua kuimba wimbo wa maadili ya Jeshi la Polisi, na kusisitiza kila askari anatakiwa kujifunza kuuimba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here