31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Ndoto mtoto wa Mkuu wa Majeshi kurusha ndege kubwa ilivyozima

Andrew Msechu -Dar es salaam

NDOTO ya mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo, kurusha ndege kubwa imezimika ghafla baada ya kufariki  dunia kwa ajali ya ndege juzi.

Siri hiyo imefichuliwa na kaka yake, Dennis Mabeyo ambaye alisema mdogo wake, Nelson Mabeyo alikuwa na ndoto ya kurusha ndege kubwa duniani.

“Familia imepoteza kiungo muhimu cha upendo, marehemu alikuwa na ndoto za kurusha ndege kubwa duniani, sasa imezima ghafla,” alisema.

Alisema pamoja na kuzimika ndoto hiyo, japokuwa Nelson alikuwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watano, akiwa na umri wa miaka 24, familia ilimtegemea kwa ushauri, kwa kuwa alikuwa na sifa za kipekee zilizomfanya kuwa nguzo ya upendo kwao.

Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam jana, Dennis alisema Nelson aliyezaliwa mwaka 1995, alikuwa kijana mwenye bidii, maono, mpole na asiyependa ugomvi.

Alisema mara nyingi pale alipoudhiwa, alichagua kukaa kimya na kuendelea na mambo yake kuliko kuendeleza ugomvi.

“Kwa kweli, mimi ni kaka yake, nilichokuwa nikikijua kwa Nelson, alikuwa mtu mwenye upendo na familia ilitambua hivyo, hata marafiki na majirani.

“Nelson alikuwa mtu wa kupenda amani wakati wote, hata ukimkwaza hakuwa mtu wa kulalamika, mara nyingi alikuwa akiamua kukaa kimya.

“Lakini zaidi alikuwa mtu mchangamfu, alipenda kusaidia, kujitoa kwa ndugu na hata kwa marafiki, alikuwa mtu mwenye upendo.

“Ndiyo maana pamoja na kwamba yeye ni mtoto wa mwisho kwenye familia, mimi ambaye ni kaka yake wa pili kuzaliwa pamoja na dada zake wote, kila mmoja alikuwa akikwama mahali alikuwa akimshirikisha na alisaidia kutoa mwelekeo,” alisema.

Akifafanua, alisema katika familia ya watoto watano wa Jenerali Mabeyo, wawili, yaani yeye Dennis na dada yake, Kapteni Neema, wote ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Wengine ambao ni Fausia, Hilda na Nelson ndio waliochukua fani tofauti.

Alisema Nelson alijaliwa vipawa ambavyo wengine katika familia hawana, kwa hiyo hata yeye kama kaka mkubwa, anajiona anapata changamoto mpya kutokana na kuondoka ghafla mdogo wake.

Dennis ambaye kwa mujibu wa taratibu ndiye msemaji wa familia, alisema tangu Nelson akiwa mtoto, alipendelea fani ya urubani, hasa wa ndege kubwa na wiki mbili zilizopita, wakati yeye akiwa nchini Lebanon, alimpa taarifa kuwa amepata fursa ya kupata mafunzo kuhusu ndege za aina ya Bombadier nchini Canada.

“Nilipopata taarifa hiyo, ambayo alinieleza anatakiwa kwenda kwenye mafunzo mwezi ujao, nilifurahi sana, nilitamani nimuone ana kwa ana ili nimpe pongezi zake, nilikuwa safarini, nilijua nikirejea nitamuona tu.

“Nimerejea wiki iliyopita, na hatukuweza kuonana moja kwa moja kwa sababu ya majukumu, tukaendelea kuwasiliana kwenye simu na aliniambia atarejea wiki hii, nikaendelea kutarajia kuonana naye. Kwa bahati mbaya, jana (juzi) ndiyo zikaja hizi taarifa nyingine za ajali na umauti,” alisema.

ELIMU YAKE

Akizungumzia elimu yake, Dennis alisema Nelson alipata elimu ya msingi kuanzia nchini Rwanda ambako baba yake aliwahi kuishi akitekeleza majukumu yake, kisha kurejea nchini na kuhitimu elimu hiyo Shule ya St Laureate iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Alisema baada ya kuhitimu, alijiunga na elimu ya sekondari Shule ya Sekondari Christ the King iliyopo Tabata, Dar es Salaam ambako alifaulu kwa kupata daraja la tatu.

Dennis alisema mdogo wake hakutaka kuendelea na masomo ya juu ya sekondari, bali aliamua kujiunga na Chuo cha Ufundi wa Ndege (Tanzania Civil Aviation College) kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa kozi ya diploma katika uhandisi wa ndege.

Alisema baada ya kuhitimu chuo mwaka 2015, aliendelea na mafunzo kwa vitendo Kampuni ya Auric Air na mwaka 2016 alikwenda nchini Marekani kwa mafunzo ya mwaka mmoja ya kurusha ndege katika chuo kilichopo katika Jimbo la Florida.

“Kama nilivyosema, alirejea mwaka juzi na kuendelea na majukumu yake ndani ya Kampuni ya Auric Air hadi aliponipa taarifa amepata ufadhili wa kwenda Canada kupata mafunzo maalumu ya kuendesha ndege aina ya Bombadier kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambayo alitakiwa kuyaanza mwezi ujao,” alisema.

AURIC AIR WAZUNGUMZA

Akizungumzia maisha ya Nelson tangu alipokutana naye kwa mara ya kwanza, Ofisa wa Operesheni wa Kampuni ya Auric Air, Rejoice Rukyaa, alisema wamepoteza mtu wa muhimu waliyemtegemea.

Alisema kwanza hakuamini na hadi sasa inamuwia vigumu kuamini kama Nelson hayupo duniani, japokuwa amejitahidi kufika hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Jeshi ya Lugalo juzi usiku na kuona jeneza lililoubeba mwili wake.

“Ninavyokwambia, Jumamosi tulikuwa pamoja, Jumapili ilikuwa siku yangu ya mapumziko  tukaonana, nikijua ana zamu ya kutekeleza majukumu yake. Jumatatu asubuhi ninapigiwa simu kuelezwa kuhusu ajali iliyotokea na kuhusisha ndege yetu, lakini nilipata mshtuko zaidi niliposikia kuwa aliyekuwepo ni Nelson na amefariki dunia,” alisema Rukyaa.

Alisema alikutana na Nelson baada ya kumpokea mwaka 2015 kama mhandisi wa ndege aliye mafunzoni na alikuwa kijana mwenye juhudi na aliyependa kazi.

Rukyaa alisema baada ya muda mfupi Nelson alionyesha kuvutiwa zaidi kujifunza kuhusu urushaji wa ndege na si ufundi tu, na alipomaliza muda wake wa mafunzo ya ufundi ya ndege mwaka 2016, alikwenda kujifunza kurusha ndege, kisha kurejea kuungana nao.

“Alikuwa mtu asiye na makuu, alikuwa muwazi, asiye na maneno mengi. Alionyesha ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yake katika nyanja zote za kiutendaji.

“Lakini wengi tulimshangaa baada ya kujua nafasi ya familia yake, hasa kwa kuwa hakuwahi kutumia nafasi ya familia kuonyesha majivuno, alikuwa mtu mwema, aliyejishusha, hakutaka hata kujulikana kwa msingi wa ubora wa familia yake, zaidi alikuwa akihamasisha vijana wenzake kuchangamkia fursa kila zinapojitokeza,” alisema Rukyaa.

Alisema alimuona ni mtu mwenye ndoto za kwenda juu zaidi ya kurusha ndege za abiria 14 za Kampuni ya Auric Air na hivi karibuni alionyesha kwa vitendo baada ya kuwaeleza mwezi ujao (Oktoba), alikuwa aende kwenye mafunzo rasmi ya kurusha ndege kubwa.

RUBANI MSIMAMIZI

Rubani Msimamizi wa Auric Air ambaye ndiye aliyempokea Nelson na kumpa mafunzo ya awali hadi kumthibitisha kurusha ndege, Kassim Ngayahika, alisema kijana huyo alikuwa miongoni mwa marubani vijana, ambao walikuwa wa kutumainiwa.

Alisema kutokana na sifa hiyo, ndiyo maana aliweza kufanya mazoezi kwa mwaka mmoja tu tangu aliporejea kutoka mafunzoni, kisha kuthibitishwa kurusha ndege ya abiria.

“Alipotoka mafunzoni mwishoni mwa mwaka juzi, tulimpokea na kuendelea kumpa mazoezi ya kurusha ndege, ilipofika Julai, mwaka jana alithibitishwa rasmi kurusha ndege zetu za abiria, kwa hiyo tangu kuthibitishwa hadi sasa ni kama mwaka mmoja na karibu miezi miwili,” alisema.

Alisema Nelson alikuwa ni kijana asiyekuwa na majivuno na hata mara nyingine wakati akijitambulisha kwa abiria kabla ya kurusha ndege, abiria ndio walioanza kuhoji na kutafuta wasifu wake.

Nelson ni miongoni mwa watu wawili waliofariki dunia katika ajali ya ndege yenye namba 5H-AAM inayomilikiwa na Kampuni ya Auric Air iliyotokea Uwanja wa Soronera uliopo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Jumatatu asubuhi.

Kamishna Msaidizi wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete, alithibitisha kutoka kwa ajali hiyo na kwamba watu wawili walipoteza maisha.

Jana kutwa nzima viongozi mbalimbali wa Serikali walifika nyumbani kwa Jenerali Mabeyo kutoa pole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles