24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

HOTUBA YA MKAPA YA KUKUMBUKWA; Hotuba hii aliitoa kwenye sikukuu ya Wafanyakazi , Dar es Salaam, Mei Mosi, 2001

“Ninayo furaha kubwa kuungana nanyi wafanyakazi wote katika kusherehekea Sikukuu ya

Wafanyakazi. Nawashukuruni sana viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kwa kunialika kwa

mara nyingine kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei Mosi. Mwaliko huu ni kielelezo

cha dhamira yenu kushirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya

wafanyakazi, na ya nchi yetu. Ahsanteni sana.

Ndugu Wafanyakazi,

Baadhi yenu mlisimamia Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Kwa sehemu kubwa sana

uchaguzi ulikwenda vizuri; na ninawapongeza na kuwashukuru wafanyakazi wote waliohusika.

Najua kura za wafanyakazi nazo zilichangia ushindi wangu mkubwa. Walionipigia kura

nawashukuru sana; na waliowapigia wagombea wengine nao nawashukuru kwa kuleta uhai

katika demokrasia yetu ya vyama vingi ambayo bado tuna kazi kubwa ya kuirutubisha, kuilea na

kuikomaza. 

Naushukuru uongozi wa vyama vya wafanyakazi uliopita chini ya Muungano wa Vyama

vya Wafanyakazi (TFTU), na wafanyakazi wote, kwa mahusiano mazuri tuliyokuwa nayo. Hata

pale tulipohitilafiana, tulizungumza, kwa uwazi na ukweli, kisha tukaendelea kujenga nchi, si

kuibomoa. Mahusiano mazuri kati ya wafanyakazi na Serikali, na utendaji wa wafanyakazi

mbalimbali, ni moja ya mambo muhimu yaliyochangia mafanikio makubwa tuliyopata katika

kurekebisha mfumo wa uchumi wetu hadi tukasifiwa duniani kote. Leo napenda katika hadhara

hii, na kupitia vyombo vya habari, niwashukuru sana wafanyakazi wa Tanzania. Naomba

tuendelee kushirikiana hivyo, kwa manufaa ya taifa na wananchi wote.

Aidha, uvumilivu na utulivu wenu ulitupa fursa ya kushughulikia matatizo makubwa ya

uchumi yanayoikabili nchi yetu. Siku zote nimekuwa muwazi na mkweli kwenu na kwa

wananchi wote. Nashukuru mmenielewa kuwa nia yangu ni njema, na kwamba kuzungumza

matatizo ya taifa letu kwa uwazi na ukweli ndiyo mwanzo wa kukubaliana juu ya ufumbuzi

endelevu.

Namshukuru Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), kwa salamu zake na kwa

misaada na ushirikiano wao kwa Vyama vya Wafanyakazi na vya Waajiri, na katika kukuza na

kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali, waajiri na wafanyakazi. Nazishukuru pia Serikali za

Denmark na Marekani wanaotusaidia kuboresha utendaji katika sekta hii ya kazi.

Natoa shukrani vile vile kwa Mwakilishi wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kwa

hotuba yake nzuri na kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na Serikali, na Vyama vya

Wafanyakazi.

Hivi punde nimetoa zawadi kwa wafanyakazi bora. Naungana nanyi katika kuwapongeza

sana, na kuwaomba waendelee na kazi yao nzuri ili wengine wajifunze kutoka kwao.

Pongezi na shukrani zangu za mwisho ni kwa viongozi na wananchi wa Dar es Salaam

kwa kuubeba vizuri sana mzigo wa kuwa wenyeji wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu.

Nakipongeza pia Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia,

Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU) kilichosimamia na kuratibu maandalizi ya Mei Mosi

hii. Wamefanya kazi nzuri, na ninawashukuru sana.

Vyama Huru vya Wafanyakazi

Ndugu Mwenyekiti,

Mei Mosi ya mwaka huu ni ya kihistoria, iliyoandaliwa na kusimamiwa na uongozi

mpya, wa vyama vipya vya wafanyakazi, vilivyo huru kabisa. Vyama huru vya wafanyakazi ni

sehemu muhimu sana ya demokrasia, na vikifanikiwa vitachangia sana kuimarisha uelewa,

uwajibikaji, na utekelezaji wa haki za wafanyakazi.

Nawapongezeni nyote kwa kuunda vyama vyenu vya wafanyakazi, na Shirikisho la

Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania, (Trade Unions Congress of Tanzania) na kuchagua

viongozi wake. Natoa pongezi za dhati kabisa kwako Mama Margaret Sitta kwa kuchaguliwa

kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Shirikisho, na kwa imani kubwa wenzako waliyoionyesha 

kwako. Hongera sana, na ninakuhakikishia ushirikiano wa dhati unapoanza kutekeleza

majukumu yako.

Nakupongeza pia Katibu Mkuu mpya, Ndugu Nestory Ngula, pamoja na nyote

mlioaminiwa na wenzenu na kupewa uongozi. Hongereni sana, na ninawahakikishieni

ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini.

Hata hivyo napenda kuwatanabahisha kuwa mwisho wa kuundwa kwa vyama, na

kuchagua viongozi, ndio mwanzo wa kazi yenyewe, katika mazingira magumu na matatizo

mengi ambayo hamuwezi kuyamaliza yote kwa mara moja. Nimepokea malalamiko yenu

kuwa Sheria iliyoanzisha vyama huru vya wafanyakazi ina mapungufu. Iwapo hoja ya

marekebisho itathibiti, tutakuwa tayari kukaa nanyi, pamoja na washika dau wengine, ili

kuirekebisha sheria hiyo kwa namna itakayozingatia maslahi ya kila upande. Maana, Serikali

lazima pia ijali maslahi ya washikadau wengine, wakiwemo waajiri, wawekezaji, na wananchi

kwa ujumla.

Ndugu Viongozi Wapya,

Katika mazingira haya mapya, na kwa kuzingatia ushindani mkali unaoletwa na

utandawazi, ninayo mambo matatu ya kushauri vyama vipya na huru vya wafanyakazi.

Kwanza, hakikisheni mikataba iliyopo sehemu za kazi, na sheria za nchi, inafuatwa na

waajiri wenu. Maana hakuna faida kutafuta haki mpya na maslahi mapya, kama hata yale ya

awali hayajatekelezwa kwa ukamilifu. Nitatoa mfano. Serikali imeweka kima cha chini cha

mshahara kisheria, lakini nasikia bado wapo wafanyakazi wanaolipwa chini ya kiwango hicho.

Ninyi mkiwa viongozi wao mnalo jukumu la kuwatetea.

Ninaambiwa pia wapo wafanyakazi ambao hawana barua na mikataba rasmi ya ajira.

Hilo nalo inabidi vyama vya wafanyakazi vilichunguze na kuchukua hatua. Nasikia waajiri

wengine wamegeuza ajira karibu yote iwe ya vibarua tu. Hoja ya vibarua inaeleweka, lakini ina

kikomo chake. Haiwezekani wafanyakazi karibu wote wawe vibarua. Fanyeni utafiti wa

kutosha na kisha kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa kushirikiana na Serikali na waajiri.

Pili, jijengeeni uwezo na utaalam wa kujua hali halisi ya uzalishaji katika kila sehemu ya

kazi, undani wa uzalishaji na biashara mnayoifanya, au huduma mnayoitoa, na kuelewa

mwenendo wake katika ulimwengu wa ushindani. Ujuzi huo utawawezesha kujiamini mnapokaa

na waajiri kuzungumzia mbinu za kuongeza uzalishaji na tija, na kuongeza uwezo wenu wa

ushindani katika soko huru, na baada ya kuongezeka kwa uzalishaji na tija, kupata nguvu, haki

na msingi wa kudai maslahi bora zaidi. Maana kama uzalishaji na tija haviongezeki, na kama

faida haiongezeki, madai ya maslahi bora zaidi yatahimiliwa na nini?

Tatu, zingatieni wajibu wa kujadiliana na waajiri juu ya hali bora za kazi. Mnapaswa

kujiimarisha kitaaluma kabla ya kukabiliana na waajiri ili muweze kujenga nguvu za hoja, si

kutumia tu hoja ya nguvu itokanayo na wingi wenu. Sheria ya Mahakama ya Kazi imeweka

utaratibu wa majadiliano ya pamoja kati ya waajiri na waajiriwa kupitia vyama vyao, ili kufunga

mikataba ya hiari ya hali bora za kazi. Sheria hii itaangaliwa upya wakati wa kurekebisha sheria 

zote za kazi. Lakini ni muhimu mikataba mtakayoifunga isaidie kuchochea uzalishaji, tija na

faida ili uwezo wa kuitekeleza mikataba hiyo upatikane.

Kamwe msisahau kuwa Serikali, na sekta ya umma kwa ujumla, sasa si mwajiri

mkubwa kama ilivyokuwa zamani. Wanachama wenu wengi sasa watakuwa kwenye sekta

binafsi. Na kwa kadri sekta binafsi inavyotwaa majukumu mengi zaidi ya kiuchumi na

utoaji wa nafasi za ajira, ndivyo wajibu na kazi za vyama vya wafanyakazi

zinavyoongezeka. Jiandaeni vizuri kuubeba mzigo huo, na Serikali itawasaidieni kwa

dhati.

Amani na Utulivu

Ndugu Mwenyekiti,

Tukumbushane umuhimu wa amani na utulivu kwetu sisi wafanyakazi. Maana ni rahisi

kudhani kuwa anayehusika na amani na utulivu ni Serikali na wanasiasa tu. Lakini ukweli ni

kuwa maslahi yenu kama wafanyakazi yanategemea sana hali ya amani na utulivu. Kwa sababu

hiyo, kila mfanyakazi ni mshika-dau katika kuhifadhi na kutetea sifa yetu kama kisiwa cha

amani na utulivu.

Tunaishi katika dunia ya ushindani kwenye kila jambo, ikiwemo ushindani katika kuvutia

mitaji na vitegauchumi, ushindani wa ajira, na ushindani wa biashara. Sifa moja inayotuongezea

uwezo wa ushindani katika Bara la Afrika ni hali yetu ya amani na utulivu. Mwekezaji binafsi,

ambaye sasa ndiye tunayemtegemea atoe nafasi za ajira, hawezi kuja kuwekeza Tanzania

tukipoteza sifa hiyo. Watalii tunaowategemea sana kwa ajira na mapato nao wataikwepa nchi

yetu.

Hivyo wafanyakazi wawe wakereketwa wa amani na utulivu. Kwanza, wao wenyewe

wasishiriki au kufumbia macho vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani na utulivu. Na pili,

washirikiane na Serikali katika kukemea tabia inayoanza kuota mizizi ya kutoheshimu sheria au

maelekezo mengine halali ya Serikali yenye lengo la kudumisha amani na utulivu.

Inawezekana wapo wanasiasa wanaofikiri kuwa ghasia, fujo na vurugu kwao ni mtaji wa

kisiasa; lakini kwako mfanyakazi wa Tanzania ujiulize utapata faida gani nchi hii ikianza

kukwepwa na wawekezaji na watalii.

Umaskini na Maendeleo

Ndugu Mwenyekiti,

Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani, na sasa tumeazimia kuondokana

na aibu hiyo. Tumebuni Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayokusudia kutufanya tuwe taifa

ambalo watu wake walio wengi watakuwa na maisha bora; taifa lenye amani, utulivu, na umoja;

taifa linaloongozwa kwa misingi ya utawala bora, utawala wa sheria; taifa lenye watu

walioelimika na wanaoendelea kujielimisha; na taifa lenye uchumi unaohimili ushindani, uchumi 

unaokua na kutoa ajira na mapato, uchumi endelevu usioharibu mazingira yetu, na uchumi

utakaonufaisha washika-dau wote, na kuhimili matumaini yetu ya maisha ya kisasa.

Hayo ni malengo, lakini utekelezaji wake unategemea sana jasho na maarifa ya kila

Mtanzania, kila mfanyakazi, kila mkulima, kila mfugaji, kila mvuvi, na kila mfanyabiashara, wa

kike na wa kiume. Nchi yetu itaendelea kwa kazi, si kwa maneno matupu au tamaa ya maisha

bora. Hatuwezi kuendelea kwa kutegemea fadhila za mataifa mengine. Wao si ndugu zetu, na

wakati mwingine wanaweza kuwa na agenda zao ambazo si lazima zishabihiane na malengo

yetu. Na hata kama wangekuwa ndugu zetu, wahenga walishatuambia, “Mtegemea cha ndugu

hufa maskini”.

Haki za binadamu zinazungumzwa sana, lakini jambo ambalo halizungumzwi sana ni

ukweli kuwa adui mkubwa wa haki za binadamu ni umaskini. Kwa mtu ambaye hana

uhakika wa chakula, haki yake ya msingi ni chakula. Kwa mtu ambaye hana nguo, haki yake ya

msingi ni nguo. Na kwa yule ambaye hana mahali pa kuishi haki yake ya kwanza ni kujiwezesha

kupata makazi.

Umaskini, na unyonge unaotokana na umaskini na utegemezi, ndiye adui mkubwa sana

wa nchi yetu. Tusipokuwa waangalifu, tunaweza kuondolewa kwenye mkazo unaostahili

kwenye umaskini, tukang’ang’ania mambo yapitayo ambayo hayampi shibe mwenye njaa,

hayamvishi aliye uchi, na hayampi makazi asiye na mahali pa kuishi, sisemi kumpeleka mwanae

shule au kumtibu akiugua.

Hivyo ni muhimu sana kwa wanasiasa wote – katika Chama Tawala na katika Upinzani –

kuwajali zaidi wananchi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwenye vita dhidi ya umaskini.

Mwanasiasa katika nchi maskini kama yetu, iwapo anao uadilifu wowote wa kisiasa ndani yake,

ataona uchungu juu ya umaskini wa watu wetu, na ataunga mkono jitihada zote za Serikali

kupiga vita umaskini.

Lakini kama wapo wanaofikiri kuwa bidii ya kuandaa maandamano na mikutano ya

kudai mimi na Rais Karume tuwapishe Ikulu ndiyo njia sahihi ya kupiga vita umaskini, wanaota

ndoto za mchana. Mimi, na nina hakika Rais Karume, tutaendelea kuweka mkazo sahihi na

unaostahili katika kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi wote, ikiwemo kukuza ajira,

kuboresha maslahi ya wafanyakazi, kuboresha huduma za jamii, na hatimaye kufikia malengo

yetu ya kuondosha umaskini kwa faida ya wananchi wote.

Matokeo na Athari za Utandawazi

Ndugu Wafanyakazi,

Dunia yetu ya leo ina sifa mbili kubwa. Moja ni kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia,

na ya pili ni mageuzi makubwa katika mifumo ya kijamii na kiuchumi. Mabadiliko na mageuzi

hayo yanachochewa na utandawazi, ambao ni wimbi kubwa. Tunakabiliwa na chaguo ama

kuacha kubadilika tusombwe na wimbi hilo, na kuendelea kuserereka pembezoni mwa

maendeleo ya dunia ya karne ya 21; au tubadilike haraka kisera, kiutendaji, na kimtazamo, na 

kutafuta mbinu za kuhakikisha nasi tunafaidika katika mfumo huu mpya wa mahusiano duniani,

na hivyo kuwahami wafanyakazi wetu.

Utandawazi huu unafuta mipaka baina ya nchi na nchi, bara na bara. Mipaka ya

kijiografia haiwezi tena kuzuia maingiliano ya fikra, teknolojia, ujuzi, biashara na mitaji. Katika

hali hiyo ushindani unakuwa mkali sana, kwenye kila kitu; ushindani ambao sisi tunauingia

tukiwa dhaifu kuliko wenzetu.

Katika mazingira haya, uwekezaji mitaji ndio njia pekee ya kukuza uchumi, kupatikana

kwa nafasi za ajira, na kuboresha maisha ya wananchi. Ndiyo maana nchi zote, kubwa na ndogo,

tajiri na maskini, zinashindana kuvutia wawekezaji mitaji, kwa kushindana kuweka mazingira

mazuri ya uwekezaji kisera, kiutendaji, kisheria – ikiwemo sheria za kazi – na kwa kuboresha

miundo mbinu.

Iwapo sisi hatutabadilika, tutajipunguzia mvuto wetu kwa wawekezaji, wakati ambapo

sisi wenyewe ndani ya nchi hatuna uwezo wa mitaji na ujuzi kuzalisha bidhaa na kutoa huduma

za kushindana kwenye soko la kimataifa. Ni kweli baadhi ya hatua tunazolazimika kuzichukua

zinaweza kuathiri baadhi ya wafanyakazi, hasa kwa siku za mwanzo. Lakini, ingawa dawa siku

zote ni chungu, hatima yake ni kupona. Kinyume chake ni kukaribisha maradhi, na hata kifo.

Hata hivyo, napenda niwahakikishieni kuwa tunachukua, na tutaendelea kuchukua, kila

tahadhari ili kulinda na kutetea maslahi ya taifa letu, maslahi ya wafanyakazi na maslahi ya

wananchi. Hatufanyi mageuzi, na hatuchukui hatua za kuvutia wawekezaji, kwa mtindo wa

“bendera fuata upepo”. Tunakuwa makini, na kuona hoja ipi inakubalika, na ipi haikubaliki.

Kwa upande wa ushindani wa kibiashara tunayo kazi kubwa mbele yetu inayohitaji

ushirikiano mkubwa kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi. Kwanza, lazima tuongeze

uzalishaji na tija. Lazima tubadili mtazamo wetu kuhusu kazi, na tupende kufanya kazi kwa

kujituma zaidi kuliko kungoja kutumwa, tufanye kazi kwa bidii, kwa ubunifu na kwa maarifa.

Pili, lazima tuongeze ubora wa bidhaa tunazotengeneza na kuzifunga vizuri kama washindani

wetu katika soko la dunia wafanyavyo. Tatu, lazima tupunguze gharama za uzalishaji na

uendeshaji ili bei ya bidhaa zetu iweze kushindana katika masoko ya dunia. Nne, lazima

tupunguze gharama za kufanyia biashara. Na tano lazima tuwe hodari zaidi katika

kujitangaza na kutafuta masoko mapya, ikiwemo masoko yaliyo jirani nasi.

Na hapa napenda nirudie tena mwito wa kuwa na ushirikiano wa karibu sana kati ya

Serikali, waajiri, na wafanyakazi. Tusipokuwa kitu kimoja, na badala yake kuendekeza

malumbano na mivutano, hatutafanikiwa. Tuazimie kuanzia leo kuvuta pamoja, si

kuvutana.

Upo pia ushindani wa ujuzi na maarifa. Tanzania tuna maliasili nyingi, lakini dunia ya

leo, na hasa dunia ijayo, itatawaliwa na wenye maarifa, kwa maana ya sayansi, teknolojia, elimu

na ujuzi. Kuwa na maliasili peke yake haitoshi. Hatuna budi tujinoe kwa elimu na ujuzi, na hasa

elimu inayomfanya mtu aajirike au ajiajiri. 

Yapo malalamiko kuwa wawekezaji kutoka nje wanaajiri sana wageni. Tatizo hili

linakuzwa mno kuliko hali halisi ilivyo. Ukiacha sekta kama vile madini ambapo hatuna

wataalamu wa Kitanzania wa kutosha, kwenye sekta nyingine nyingi wawekezaji hao

hawaruhusiwi kuajiri zaidi ya wageni 5. Utafiti tulioufanya kwenye baadhi ya miradi unaonyesha

kuwa kwenye sekta ya viwanda, wageni walioajiriwa ni chini ya asilimia moja ya wafanyakazi

wote; kwenye utalii ni zaidi kidogo ya asilimia moja; kwenye madini ni karibu asilimia 15, na

kwenye huduma ni asilimia moja. Hivyo hali si mbaya sana, na itazidi kuwa nzuri siku zijazo.

Changamoto kwetu Watanzania ni kuhakikisha tunao wataalamu wa kiwango

kinachoweza kushindana na wataalamu wengine duniani, tukianzia na soko la ajira la Afrika

Mashariki.

Ndugu Mwenyekiti,

Tutaendelea kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani usiokuwa wa haki kutoka

bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizaji wa bidhaa kwa njia ya

magendo. Lakini katika dunia ya utandawazi, hoja ya kulinda viwanda vya ndani ni hoja ya

mpito tu wakati nchi changa zinajenga uwezo wa kuhimili ushindani. Hivyo utaratibu wa

kulinda viwanda lazima uende sambamba na juhudi za makusudi kuongeza uwezo wa

ushindani. Na hilo halitawezekana iwapo tutavilinda mno viwanda vyetu.

Kazi na Ajira

Ndugu Wafanyakazi,

Leo napenda pia nizungumzie dhana ya kazi kwa upande mmoja, na dhana ya ajira kwa

upande mwingine. Lazima tujifunze kubadili uelewa wetu wa kazi, na uelewa wetu wa ajira.

Maana si lazima kila penye kazi pawe na ajira, na si lazima kila penye ajira kuwe na kazi.

Mfano mzuri wa kazi bila ajira ni kina mama. Wanafanya kazi kubwa na muhimu katika

familia. Lakini hawana ajira, wala hawalipwi mshahara. Kwa upande mwingine, na hasa

kwenye sekta ya umma, wapo watu wana ajira, lakini hawana kazi, au wanagawana kazi ambayo

ingeweza kufanywa na mtu mmoja tu. Wapo wanaolipwa mshahara kamili kwa nusu kazi, au

robo kazi, na wapo hata wanaolipwa kwa vile tu wameajiriwa, hata kama hawakufanya kazi

yoyote.

Tatizo la baadhi ya watu kupenda kulipwa bila kufanya kazi inayolingana na malipo si

letu peke yetu. Ipo hadithi ya bwana mmoja kutoka nchi tajiri mojawapo ambaye alikuwa na

tabia hiyo. Yeye alikuwa amepunguzwa kazi na akawa analipwa fedha za kujikimu kwa vile

alikuwa hana kazi. Ikafika wakati utaratibu huo wa kulipwa bila kazi ukafutwa, akalazimika

kutafuta kazi. Akamwendea mwenye nyumba mmoja na kumwomba kazi ya kufyeka majani

kwenye bustani yake.

Mwenye nyumba akamwambia, “Kwa kawaida anakuja kijana wa jirani yangu kufanya

kazi hiyo, na ninamlipa sh.20,000/=. Lakini kwa vile nakuona una shida ya kazi, wewe

nitakulipa sh.25,000/=.” 

Yule bwana akamjibu, “Tafadhali mwache kijana aendelee na kazi yake; wewe nipe tu

hizo sh.5,000/=.”

Ndugu Wafanyakazi,

Mengine haya yanachekesha, lakini kujenga uchumi wa kisasa, unaohimili ajira kubwa,

na maslahi bora zaidi, si jambo la lelemama, au jambo la kuchekesha. Tupende tusipende,

tunakabiliwa na ushindani mkubwa sana, na tukiendelea na tabia hii hatutaweza kuuhimili

ushindani huo; viwanda vitafungwa; na ajira ama itahamia nchi za nje, ikiwemo nchi jirani, au

wao watakuja nchini kuchukua kazi zetu.

Katika uchumi unaohimiliwa na sekta binafsi ajira na maslahi ya wafanyakazi

havipatikani kwa amri ya Serikali, bali kwa uwezo wa kuzalisha, kushindana, na kupata faida.

Kama tunataka uchumi ukue, uweze kushindana na kuvutia wawekezaji wengi zaidi, lazima

tujenge ushirikiano na kuaminiana zaidi kati ya Serikali, wawekezaji, wananchi na wafanyakazi.

Tuunde ubia wa kuhakikisha taifa linafanikiwa, wawekezaji wanafanikiwa, na wafanyakazi nao

wanafanikiwa.

Mwaka hadi mwaka tunalalamika kuwa wapo vijana 600,000 – 700,000 wanaoingia

katika soko la ajira, wakati sekta rasmi inaweza kuajiri kiasi cha 25,000 tu kwa mwaka. Lakini

pia tujiulize hao vijana 600,000 wanaweza kufanya kazi gani ya kuajiriwa? Wana ujuzi gani

wenye soko katika hali halisi ya uzalishaji na utoaji huduma nchini? Ukweli ni kuwa wengi wao

hawaajiriki kwa urahisi.

Lazima tukubali pia kuwa tunaposema uti wa mgongo wa uchumi wetu ni kilimo, ufugaji

na uvuvi, maana yake ni kuwa uti wa mgongo wa uhakika wa ajira ni kilimo, ufugaji na uvuvi,

pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya sekta hizo. Tunasema hakuna ajira, lakini tunayo

ardhi tele inayofaa kwa kilimo na ufugaji, na tunayo bahari, mito na maziwa yenye samaki. Kwa

vyovyote vile haitawezekana kwa sekta rasmi kuajiri wote watafutao kazi. Kwa Watanzania

wengi, ajira maana yake ni kujiajiri katika kilimo, ufugaji na uvuvi. Huo ni ukweli ambao hatuna

budi sote kuukubali.

Ndugu Wafanyakazi,

Ni kweli Serikali ina wajibu wa kufuatilia wawekezaji ili kuhakikisha wanatekeleza

masharti ya mikataba na maelewano yetu, na kufuata sheria za nchi. Tutaendelea kutekeleza

jukumu hilo, na kuongeza uwezo wa ukaguzi. Vyama vya wafanyakazi navyo viwe macho. Kwa

upande wake, Serikali imeamua kukifanya Kitengo cha Afya na Usalama wa Wafanyakazi kuwa

Wakala wa Serikali ili kiweze kujiendesha kwa ufanisi na kutoa huduma bora zaidi kwa

wafanyakazi na waajiri.

Ipo pia mipango mingi ya kuimarisha uwezo wa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana

na Michezo, kwa msaada wa wahisani mbalimbali. Tunao mradi wa kuimarisha Idara ya Kazi

unaofadhiliwa na Serikali ya Denmark. Lengo ni kuweka mazingira bora zaidi ya kisera na

kisheria katika mahusiano ya kikazi, kuwa na sheria za kazi zinazoenda na wakati na kuvutia 

uwekezaji zaidi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, kuongeza uzalishaji na tija za

wafanyakazi, na kujenga maelewano mazuri sehemu za kazi.

Mradi mwingine, ambao huu unafadhiliwa na Serikali ya Marekani, ni wa kuanzisha

Soko la Ajira. Kazi iliyoanza Aprili mwaka jana ya kukusanya takwimu za msingi kuhusu ajira

inatazamiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu. Kituo cha kwanza cha Soko la Ajira

(Employment Exchange Centre) kitaanzishwa hapa Dar es Salaam, na baadaye mikoani.

Miongoni mwa majukumu ya vituo hivyo itakuwa kutoa ushauri nasaha kwa wanaotafuta kazi,

kusaidia kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri, na kukusanya na kutoa takwimu za hali ya

soko la ajira kwa ujumla. Huduma hii itawarahisishia waajiri kutafuta wafanyakazi, na

wanaotafuta ajira kujua kazi ambazo wana ujuzi nazo zinapatikana wapi.

Ndugu Wafanyakazi,

Tunalo pia bado tatizo la unyanyasaji na ubaguzi wa wanawake katika jamii zetu, katika

shule na vyuo, na katika ajira. Kutokana na jitihada zinazochukuliwa na Serikali tatizo

linapungua, lakini halijakwisha. Natoa tena wito kwetu sote kufuta aibu hii ya kunyanyasa au

kubagua wanawake.

Serikali pamoja na wabia-jamii, kwa msaada wa Shirika la Kazi Duniani (ILO),

tumetekeleza mradi wa kuangalia upya hali ya ajira kwa wanawake katika mazingira ya mageuzi

ya uchumi. Tayari ripoti imekamilika na imetupa mahali pa kuanzia katika kutetea na kulinda

maslahi ya wanawake. Ikibidi tutabadili sheria na taratibu. Lakini, kazi kubwa zaidi ni kubadili

fikra, mazoea, mila na desturi zinazokwamisha ukombozi wa kweli wa wanawake. Kazi hiyo si

ya Serikali peke yake; ni ya jamii nzima. Na hapa tena navipongeza vyama huru vya

wafanyakazi kwa kuonyesha njia, na kumchagua Mama Sitta awe Mwenyekiti wa kwanza wa

Shirikisho lao. Hiyo ni ishara kuwa tutashirikiana vizuri kutetea haki na maslahi ya wanawake

sehemu za kazi.

Sheria na Mikataba

Ndugu Mwenyekiti,

Serikali inatambua umuhimu wa kuridhia Mikataba ya ILO kuhusu malipo sawa kwa kazi

sawa, kuondosha ubaguzi katika ajira, na kupiga marufuku ajira mbaya sana ya watoto.

Mikataba hiyo pia inahusu haki za msingi za binadamu ambazo zimo ndani ya Katiba yetu.

Hivyo tatizo si nia ya kuridhia, bali utaratibu tu wa kufanya hivyo. Na hivi sasa hatua za

kuridhia mikataba hiyo karibu zitakamilika.

Kuhusu ajira ya watoto, tangu mwaka 1994 Tanzania imetekeleza Mpango wa Kimataifa

wa Kuondosha Ajira ya Watoto kwa kushirikiana na waajiri na wafanyakazi. Juhudi hizo

ziliipelekea Tanzania kuwa kati ya nchi tatu duniani zitakazotekeleza mpango wa muda maalum

kumaliza ajira mbaya sana ya watoto. Tunatambua pia kuwa umaskini ndicho chanzo na

kishawishi kikubwa cha ajira ya watoto. Hivyo juhudi zote za Serikali za kuondosha umaskini

zinalenga pia kuondosha tatizo la ajira ya watoto. 

Nia ya Serikali ni kuwa na sera na mfumo wa sheria za kazi zinazolinda maslahi ya

wafanyakazi, na maslahi ya waajiri, ili mahusiano mema kazini yawe yale ambayo msingi wake

ni kuheshimu haki na maslahi ya wafanyakazi na waajiri, yenye tija katika uzalishaji,

yanayowezesha ushindani, na kwa hiyo kuleta maendeleo na maisha bora.

Mikopo ya Nyumba kwa Wafanyakazi

Ndugu Mwenyekiti,

Mojawapo ya matatizo ya wafanyakazi wengi ni kukosa uhakika wa nyumba za kuishi

wakiwa kazini, lakini hasa baada ya kustaafu. Kumiliki nyumba kunatosheleza hitaji muhimu la

mwanadamu; na kumpa heshima na utulivu wa fikra na maisha.

Katika miaka 10 ya kwanza baada ya uhuru, kulikuwa na mfuko wa mikopo ya nyumba

kwa watumishi wa umma. Mfuko huo uliwasaidia watumishi wa umma wakati huo kujijengea

nyumba. Leo hakuna mfuko kama huo wenye uwezo wa kutosheleza kujenga nyumba za

watumishi kwa mkopo. Matokeo yake, na kwa vile mfumo wa ukopeshaji fedha kwa ajili ya

kujenga nyumba kwenye benki zetu bado haujaimarika, inabidi wananchi walio wengi wajenge

nyumba kwa fedha kutoka mifukoni mwao.

Ujenzi wa namna hiyo ni ishara ya kuwa nyuma sana kimaendeleo, na kwa watumishi wa

umma ni chanzo, kichocheo na kishawishi kikubwa sana cha rushwa. Dunia ya leo watu

hawajengi hivyo; na ni matumizi mabaya ya fedha hata kwa wale ambao wanazo. Kwa vile

nyumba ni mali isiyohamishika, hakuna sababu ya kujenga kwa fedha kutoka mfukoni; na wala

hakuna sababu kwa benki zetu kutaka mkopaji arejeshe mkopo katika muda mfupi. Kwenye

nchi zilizoendelea mikopo ya nyumba inalipwa kwa hata zaidi ya miaka 25.

Kwa sababu hiyo nimeamua, kwa kuzingatia sera ya Chama changu, kuwa tuanzishe

mfumo ulio wazi wa mikopo ya nyumba na uwekaji nyumba rehani kwa jumla; na pia kuwa na

utaratibu mwingine maalum kwa watumishi wa umma.

Hivi sasa Serikali inashauriana na washika-dau mbalimbali, pamoja na benki zetu, kuona

namna bora ya kutekeleza jambo hili kwa haraka, lakini kwa makini sana, maana hatutaki yale

yaliyoisibu Benki ya Nyumba yarudiwe tena. Lazima nitoe tahadhari. Mkopo ni mkopo, na

lazima urejeshwe kulingana na makubaliano kati ya mkopaji na mkopeshaji. Ujanja wa kukwepa

wajibu wa kulipa hauwezi kupewa mwanya tena kwenye sheria zetu.

Maandalizi ya kisera na kisheria yanaendelea. Karibu tunakamilisha Kanuni za Sheria ya

Ardhi ya mwaka jana kwa kushirikiana na washika dau wengine ili kuvutia benki kukopesha kwa

ajili ya ujenzi wa nyumba. Serikali pia itaendeleza sera za jumla za uchumi zitakazosaidia

kuweka mazingira bora kwa ukopeshaji wa muda mrefu, kama vile kuendelea kushusha

mfumuko wa bei, na riba za benki.

Nawaombeni viongozi wa vyama vya wafanyakazi nanyi mhamasishe wafanyakazi

kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa, na kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, muanzishe ushirika 

wa nyumba. Tatizo la nyumba ni kubwa, na ufumbuzi wake lazima utuhusishe na kutushirikisha

wote.

Rushwa na Ubadhirifu

Ndugu Wafanyakazi,

Nizungumzie kidogo kuhusu rushwa na ubadhirifu. Wote wawili hawa ni maadui

wakubwa wa maendeleo na ustawi wetu. Ipo rushwa inayopotosha haki, na kuifanya iwe bidhaa

ya kuuzwa na kununuliwa. Na ipo rushwa inayopotosha maamuzi ya kiutendaji na kuliingizia

taifa au taasisi yoyote ile hasara kubwa. Mfano ni pale ambapo barabara ambayo ingeweza

kujengwa kwa sh.5 bilioni, inaishia kujengwa kwa sh.10 bilioni, na mzigo huo unabebwa na

uchumi wa taifa, na hatimaye wananchi. Dhahiri rushwa ni kitu kibaya sana katika jamii na

lazima tupigane nayo bila kuchoka au kukata tamaa.

Na rushwa si janga la Tanzania peke yake. Hakuna nchi yoyote duniani inayoweza

kuthubutu kusema kuwa wao ni watakatifu kabisa katika suala hili. Tofauti zilizopo ni aina ya

rushwa baina ya nchi na nchi, kiwango cha rushwa, na uwazi uliopo katika kujadili uwepo wa

rushwa katika jamii na taifa.

Tanzania tumekuwa wazi sana kuhusu rushwa. Sijui ni nchi ngapi zimeunda Tume kama

niliyounda mimi chini ya Jaji Warioba kutafiti rushwa kwa undani katika nchi yetu, kubainisha

chanzo chake, na kuweka mpango maalum na mkakati wa kuipiga vita rushwa. Na utekelezaji

unaendelea kwa kuziba mianya ya rushwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kuongeza

uwezo wetu wa kupokea, kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria kuhusu tuhuma zote za

rushwa. Upo mkakati wa kitaifa, na upo mkakati kwa kila sekta na kila Wizara.

Kazi ya kupiga vita rushwa ni ngumu sana, hasa ikijipenyeza pia kwenye vyombo

vinavyosimamia sheria na haki. Nyote ni mashahidi kuwa kesi za rushwa zinachukua muda

mrefu mno. Wakati mwingine ni vigumu kupata ushahidi utakaothibiti mahakamani, hasa pale

wale wenye taarifa za ndani na ushahidi hawako tayari kushirikiana na Serikali.

Siwezi kuwalaumu wananchi wanapoishiwa na subira. Wakati mwingine hata mimi

natamani ningekuwa na uwezo wa kutia watu ndani pale tuhuma nzito dhidi yao zinaponifikia.

Lakini zama hizo zimepita. Leo dhana inayoshamiri ni ya utawala wa sheria, ambapo

mtuhumiwa anahesabika hana hatia hadi mahakama itakapoamua kesi inayomkabili.

Hali hiyo inaiweka Serikali katika hali ngumu sana. Vyombo vya habari vinaandika

tuhuma za rushwa, na kuifanya jamii iamini kuwa yanayotajwa ni kweli, na hivyo wanataka

wasikie kesho yake mtuhumiwa kafungwa au kafilisiwa. Hata marafiki zetu kutoka nchi za nje

nao wanakosa subira. Lakini hao hao, na waandishi wa habari hao hao, ndio wa kwanza kutupa

darasa juu ya haki za binadamu, utawala bora, na utawala wa sheria!!

Napenda niwahakikishieni, Ndugu Wafanyakazi, kuwa dhamira na utashi wa kisiasa wa

kupiga vita rushwa sio tu upo pale pale, bali unaongezeka. Ambacho nina uhakika hakiongezeki

ni ushirikiano wa wafanyakazi katika kupiga vita rushwa na ubadhirifu. Mimi ninaelewa 

wananchi wa kawaida wakinyoshea kidole Serikali na taasisi zake. Lakini napata taabu

nikiambiwa wafanyakazi wanalalamikia rushwa. Maana, hakuna mtu anayeitwa Serikali

anayepokea rushwa. Mpokea rushwa si Serikali; ni mfanyakazi mwenzetu, tunamjua, lakini

tunaoneana haya. Huo ndio ukweli, na unafanya kazi yetu iwe ngumu sana.

Huko mikoani niliwahi kuwataka wananchi wafanye mikutano ya hadhara na kupiga kura

ya maoni kuhusu wanaowatuhumu kula rushwa. Najua huu si utaratibu mzuri sana, lakini

ulitupa pa kuanzia kwa kuwajua wanaotuhumiwa, na kuanza kuwachunguza.

Sasa niambieni. Ni mara ngapi mmesikia kuwa katika Wizara au Taasisi fulani

wameitisha mkutano wa wafanyakazi wote kwa lengo la kupiga kura ya maoni, ya siri, ya

kuwafichua wenzao wanaowajua kuwa ni wala rushwa? Maana haiwezekani awepo muuguzi

katika hospitali anayedai rushwa kutoka kwa wagonjwa, halafu wenziwe wasimjue. Vivyo hivyo

kwenye Jeshi la Polisi, Mahakama, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Elimu, na

kadhalika.

Nakubali wito wenu kuwa vita dhidi ya rushwa izidi kuongezwa nguvu na kasi. Lakini

nasema nafasi bado ipo kubwa kwa wafanyakazi kusaidia vita hivyo pale walipo, kwa wenyewe

kuacha rushwa na ubadhirifu, na kwa kutoa taarifa za wenzao wanaochafua jina la mahali pao pa

kazi kwa kupanukisha rushwa. Zama za ukimya wa kulindana sasa ziishe. Na wakati mwingine

kunyosheana vidole baina ya sekta na sekta, wizara na wizara, idara na idara, haisaidii sana kama

watu wasipoanza kusafisha rushwa pale walipo. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam yupo hapa.

Yeye hupenda kusema, “Mkia wa mbuzi ni mfupi; unasafisha pale alipolala.”

Na sisi sawia. Mfanyakazi wa Wizara ya Elimu anakuwa mwepesi kulaumu rushwa

aliyopambana nayo alipoenda mahakamani, lakini ile rushwa mtumishi wa mahakama

aliyopambana nayo katika kumwandikisha mtoto wake shule haioni.

Natoa wito kwa vyama vipya vya wafanyakazi vione kuwa mojawapo ya kazi zao ni

kusafisha jina la sehemu yao ya kazi, na jina la taaluma zao. Vyama vya wafanyakazi vione

haya, na kuchukua hatua, pale jamii inapowanyooshea vidole kuwa ni wala rushwa au

wabadhirifu. Vibuni mikakati ya kujisafisha, na ikibidi viombe msaada wa Taasisi ya Kuzuia

Rushwa katika kupanga na kutekeleza mikakati hiyo. Lazima pia, wote kwa pamoja, kujenga

utamaduni wa kuona rushwa na ubadhirifu kuwa ni jambo la aibu, na kuwa mali isiyotokana na

jasho, mali inayonuka rushwa, ubadhirifu na wizi, ni aibu na fedheha kubwa!

UKIMWI

Ndugu Wafanyakazi,

Nimefarijika kusikia risala yenu ikieleza kutambua kwenu kuwa janga la UKIMWI

linahitaji elimu kwa jamii yote pamoja na waajiri ili kufanikisha mapambano dhidi yake.

Mmetoa mwito pia kuwa wafanyakazi walioathirika wasitengwe au kunyanyaswa mahali pa

kazi. Nakubali na ninaungana nanyi kabisa katika hoja yenu hiyo. 

Ningependa sote tujiulize tena maswali magumu bila aibu na tuchukue hatua bila ajizi.

Je, tangu mwaka huu uanze tumeshiriki kiasi gani kuzuia kuenea kwa UKIMWI? Je, wewe

umekwisharekebisha mwenendo wako na kuacha tabia zinazochangia kuenea kwa UKIMWI?

Je, hapo kazini pamekuwa na mwamko mpya wa kupambana na UKIMWI? Wewe mfanyakazi

unashiriki vipi?

Ndugu Wafanyakazi,

Kila mmoja atafakari kwa dhati moyoni mwake na achukue hatua. Nawaomba pia

waajiri wawe mstari wa mbele katika vita hivi na wawasaidie wafanyakazi wao kwa kila hali

kuweza kujikinga, na kwa walioathirika tayari kuwatendea haki bila ubaguzi. Kila sehemu ya

kazi sasa iwe na utaratibu wa kukumbushana mara kwa mara juu ya UKIMWI, na mkakati

mahususi wa kuzuia kuenea kwa virusi vya UKIMWI.

Hitimisho:

Ndugu Wafanyakazi,

Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuwakumbusha kuwa njia ya maendeleo imejaa

jasho na vumbi. Tuzingatie utamaduni wa kupenda kufanya kazi kwa bidii, maarifa, ubunifu na

kujituma. Lawama ni tamu ikitoka mdomoni, lakini peke yake haitapeleka mkono kinywani. Na

katika kujituma kila mfanyakazi akumbuke kuwa la muhimu si muda anaotumia kufanya kazi,

bali kiasi cha kazi anayoweza kuifanya katika muda aliopewa.

Wenzetu majirani na duniani kote wanajishughulisha, usiku na mchana, kuongeza

uzalishaji na kunoa uwezo wao wa tija na ushindani. Na sisi tuamke. Nina matumaini makubwa

nanyi viongozi wapya wa vyama huru vya wafanyakazi kwamba mtashirikiana vizuri na Serikali

na waajiri ili nchi yetu ijikomboe kiuchumi na kuleta ustawi kwa wananchi wake. Hakuna njia

ya mkato, isiyo na machungu. Tuwaongoze wafanyakazi kujua na kuzingatia jambo hilo. Na

tuwashirikishe kama tunataka kushinda vita hivi.

Bwana mmoja aliwahi kusema, “Mtu akikwambia ametajirika kutokana na kazi nzito,

muulize, kazi hiyo nzito ameifanya nani?”

Na sisi sote tunatamani maisha bora, ya kisasa. Tunajua pia kuwa utajiri na maisha bora

chanzo chake ni kazi nzito. Swali. Kazi hiyo nzito aifanye nani?

Nawatakieni Sikukuu njema.

Ahsanteni kwa kunisikiliza

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles