23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Hongera Simba, mnastahili pongezi 

WAWAKILISHI pekee nchini katika michuano ya kimataifa, timu ya Simba, wameanza vyema hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, baada ya kuifunga JS Saoura ya Algeria mabao 3-0, katika mchezo wa awali uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kabla ya Simba kutinga hatua hiyo ya makundi, iliiondosha timu ya Nkana Red Devil ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3, kufuatia kufungwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza mjini Kitwe, Zambia, kisha kuinyuka timu hiyo mabao 3-1, katika mchezo wa marudiano, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo wa Simba katika mchezo huo wa kundi D, unaipa nafasi ya kuongoza kundi hilo, wakiwa na pointi tatu sawa na Al Ahly ya Misri, ambao juzi waliifunga timu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mabao 2-0.

Baada ya mchezo huo wa juzi, Simba itasafiri kuwafuata AS Vita mjini Kinshasa, utakaochezwa Januari 19 mwaka huu katika Uwanja wa Stade des Martyrs, huku JS Saoura ikiwa nyumbani ikiikaribisha  Al Ahly Januari 19.

Simba itakamilisha mzunguko wa kwanza wa michuano hiyo itakapovaana na Al Ahly, Februari Mosi, mwaka huu.  

Timu hiyo imeanza kuonyesha makali yake katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa na dhamira ya kufika mbali zaidi katika michuano hiyo, inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Sisi MTANZANIA tunaipongeza Simba kwa hatua iliyofikia na ushindi waliopata dhidi ya JS Saoura, lakini pia tukiwatakia mafanikio katika michezo yao inayofuata.

Mafanikio ya ushindi wanaopata Simba ni matokeo ya umoja na mshikamano baina ya viongozi na benchi la ufundi na hakika bila kusahau nguvu wanayoipata kutoka kwa mwekezaji wao, Mohammed Dewji ‘Mo’, ambaye amekuwa bega kwa bega kuhakikisha timu hiyo inakuwa tishio barani Afrika.

Bado Simba ina uwezo wa kufanya vizuri zaidi na hata kufika fainali ya michuano hiyo, ikiendelea kujipanga vyema na kuhakikisha inapata matokeo mazuri.

Ni wakati wa viongozi na benchi la ufundi la Simba kuendelea kuwa na umoja na ushirikiano katika kuiandaa vyema timu ili iweze kufikia mafanikio ambayo wamedhamiria katika michuano hiyo.

Ni jukumu la mashabiki wa Simba na watanzania kwa ujumla kuipa nguvu timu hiyo kwa kufika uwanjani kuishangilia ili iweze kushinda michezo yake na kuitangaza Tanzania katika medani ya kimataifa.

Lakini pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali kwa ujumla kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Dk. Harrison Mwakyembe, wanapaswa kuwa bega kwa bega na viongozi wa Simba katika kuwapa ushirikiano wanapokwenda kucheza nje ya nchi ili kukwepa hujuma za wenyeji.

Ni wakati wa Simba sasa kuonyesha ubora wao katika michuano hiyo kwa kujivunia uwekezaji mkubwa waliofanya, kwa kuwa timu bora barani Afrika na kuzipiku timu kama TP Mazembe, Al Ahly na nyinginezo, ambazo zimekuwa zikitamba katika soka la ukanda huu kwa muda mrefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles