HIMID MAO KUVUNJA MKATABA AZAM FC

0
862
KIUNGO wa timu ya Azam FC, Himid Mao

Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

KIUNGO wa timu ya Azam FC, Himid Mao, amesema yupo mbioni kuvunja mkataba na klabu yake hiyo ili kukamilisha mipango yake ya kwenda kucheza soka la kulipwa.

Mao anatajwa kuwa katika mikakati ya kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, lakini aligoma kuweka wazi ukweli wa jambo hilo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mao alisema mkataba wake na Azam utamalizika Novemba mwaka huu, lakini mipango ya sasa ambayo wamejiwekea na wakala wake ni kucheza soka nje ya nchi.

Alisema wakala wake tayari ameanza mazungumzo na Azam ili wavunje mkataba na pia anapambana kufanikisha mikakati ya kumtafutia maisha mengine ya soka nje ya nchi.

“Nitaondoka Azam lakini sitasajiliwa Tanzania, mkataba wangu na Azam unatarajia kumalizika Novemba mwaka huu na sasa tumeanza mazungumzo ya kuuvunja.

“Nataka niondoke kama mchezaji huru ili nitakaposajiliwa na klabu nyingine nisifungamane na upande wowote,” alisema Mao.

Aidha, Mao aliongeza kuwa hakuna timu yoyote hapa nchini ambayo imefanya naye mazungumzo, huku akisisitiza kwamba hayupo tayari kufanya hivyo kwani anaangalia mbali zaidi kulingana na mipango yake.

Alisema bado ataendelea kuonekana na kikosi cha Azam hadi mipango yake itakapokaa sawa pamoja na mkataba wake kuvunjwa.

Kama kiungo huyo ataondoka, kikosi cha Azam kitazidi kubomoka kwani tayari kimeondokewa na wachezaji wake mahiri waliotamba msimu uliopita, John Bocco, Aishi Manula na Shomari Kapombe ambao wote wametua Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here