25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MKUDE, SIMBA MAMBO SAFI, SASA YAMWANIA MFUNGAJI BORA WA ZAMBIA

JENNIFER ULLEMBO Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

VIGOGO wa klabu ya soka ya Simba wamefanikisha kumbakisha kiungo wao mahiri, Jonas Mkude, kwa kufikia hatua ya mwisho ya makubaliano ya kusaini mkataba mpya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya klabu hiyo zililipasha MTANZANIA jana kuwa, mazungumzo kati yao na Mkude yameshafanyika na tayari ameshakabidhiwa mkataba ili akaupitie kabla ya kufikia hatua ya mwisho ya kumwaga wino.

Awali Mkude ambaye ni nahodha wa timu hiyo, alikuwa katika mvutano mkubwa na viongozi wa klabu hiyo ambao walimtaka asaini mkataba mpya, huku ikielezwa kwamba chanzo ni kutofautiana kwenye dau la kusaini.

Wakati Mkude alikuwa analilia dau la Sh milioni 60, klabu hiyo ilifikia kikomo cha kumpatia Sh milioni 40 tu, hali iliyozua sintofahamu kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wakihofia kwamba anaweza kuachana na timu hiyo huku wakiwa bado wanahitaji huduma yake.

Kwa kufikia makubaliano hayo, inamaanisha wazi kwamba sasa Mkude atasaini mkataba mpya na klabu hiyo siku yoyote kuanzia leo.

Akithibitisha taarifa hizo, Mkude aliweka wazi kukutana na viongozi wa Simba na kukubaliana mambo kadhaa ya msingi na kwamba tayari wameshamkabidhi mkataba kwa ajili ya kuupitia ili kujiridhisha kama waliyokubaliana yamo.

“Kweli mazungumzo yalifanyika na tupo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba. Kwa sasa ninaupitia kwanza mkataba niliopewa kabla sijasaini,” alisema Mkude.

Mkude pamoja na wachezaji wenzake wawili maarufu waliobatizwa jina la ‘mapacha watatu’ yaani Ibrahim Ajib na mlinzi Abdi Banda, waliigomea klabu hiyo kusaini mkataba mpya kwa dau dogo.

Hata hivyo, chanzo chetu kinadai kuwa juzi kamati ya usajili ilikutana na Banda na kufikia makubaliano ambapo naye anatarajiwa kusaini mkataba wakati wowote, huku Ajib akiwa bado hajamaliza mazungumzo na viongozi wake.

Wakati huo huo, Simba inanyemelea saini ya mshambuliaji hatari wa timu ya Nkana inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia, Walter Bwalya, ili kuimarisha safu yake ya msimu ujao.

Bwalya ambaye ni mfungaji bora wa ligi ya Zambia kwa mara mbili mfululizo, alifunga mabao 24 msimu uliopita na inadaiwa kuwa atatua nchini hivi karibuni sambamba na Mganda, Emmanuel Okwi.

Taarifa za kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa mfanyabiashara maarufu na mdau wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘MO’ ndiye aliyefanikisha dili hilo kutokana na kumfuatilia nyota huyo kwa muda mrefu.

Hata hivyo, taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa klabu ya soka ya Lusaka Dynamos, Simata Sims, ilidai kuwa kibali cha Bwalya cha kucheza Ligi Kuu  ya Zambia kina utata.

“Hatuna tatizo na uraia wa Bwalya lakini barua yetu kwa Chama cha Soka cha Zambia (FAZ) ni kutaka kujua uhalali wake wa kucheza ligi, kwani hata wachezaji wa nyumbani wanaotoka kucheza nje ya nchi wakirudi wanapaswa kuwa na kibali,” alisema Sims.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles