Hili la wanaume kulelewa, Rais Magufuli aliona mbali

0
1175

Na MWANDISHI WETU

KUNA wakati Rais Dk. John Magufuli anapokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya watu au akiwa kwenye ziara zake huwa anatamka maneno ambayo kwa namna moja ama nyingine wapo wanayoyaona kama ni mzaha na wengine kuyachukulia kimasihara, lakini ukiyatafakari utabaini kuwa ni mambo ya msingi na yanayohitaji kufanyiwa kazi.

Moja kati ya kauli ambazo wapo walioona kama ni mzaha ni ile aliyoitoa wakati akizungumza na watendaji wa kata, akiwataka kuwasimamia vijana ili wapate ajira na kuweza kujikimu kimaisha hatimaye wamudu kutoa mahari.

Rais Magufuli pamoja na mambo mengine, katika mazungumzo yake aligusia suala la vijana kupenda kujihusisha na mapenzi na wanawake wenye fedha ili wasaidiwe mambo mbalimbali.

Rais anasema ameambiwa kwamba siku hizi wanawake wanawatolea mahari wapenzi wao ili waolewe.

Kwa sabababu hiyo, akasema kwa kuwa watendaji kata ndio wenye jukumu la kuwasimamia vijana katika kata zao, kwa kuwadhamini kwa saini zao wanapohitaji kujiendeleza kwa shughuli zao, hawana budi kuwakwamua ili waondokane na aibu hiyo.

Anasema matokeo ya vijana kulelewa ni kutokana na kukosa ajira hivyo, wameamua kuwa tegemezi kwa wanawake wao.

“Vijana wakifanya kazi mbaya athari yake itakuwa ni kubwa, ila akifanikiwa basi ataweza hata kujenga nyumba kubwa, hata kama atakuwa hajaoa ataoa mwanamke anayemtaka na si kwa sababu ya fedha zake.

“Siku hizi nasikia wanawake wanawatolea mahari wanaume, nasema uongo jamani? nasema uongo kina mama?

“Inawezekana siku hizi ukimpenda mwanamke na huna hela ya kumtolea mahari basi anajitolea mwenyewe, ndio maana naambiwa vijana wa siku hizi wanapenda wanawake wenye magari.

“Hahaah…huo ndio ukweli, ili kusudi mwanamama akienda kazini yeye awe anaendesha hilo gari,” anasema Rais Dk. Magufuli.

Anaongeza: “Kwahiyo, inawezekana watendaji kata kina mama wenye magari wana vijana huko wanacheza nao.” Kauli hiyo iliwaacha hoi watendaji wa kata na kujikuta wakiangua kicheko.

Sasa basi, inawezekana kabisa kuwa watu waliona ni mzaha, lakini ukweli ni kwamba vijana wa siku hizi wanapenda maisha ya mteremko. Utamkuta kijana wa kiume mtanashati lakini hana kazi anategemea mwanamke akatafute fedha amtunze.

Hii ni aibu kwa wanaume, hata kama ajira hakuna, kuna haja ya kutafuta njia za kujiajiri ili angalau mpate fedha za kutekeleza majukumu ya kifamilia.

Katika hali ya kawaida, mwanamume unapokuwa tegemezi ndani ya nyumba, au mahari imetolewa na mwanamke ndipo ukamuoa, usitegemee mwanamke huyo akakuheshimu, ni lazima aatakuwa akifanya vile anavyofanya akiamini kuwa huwezi kumfanya chochote kwa sababu yeye ndio anakutunza hivyo, ameshika nafasi ya baba ndani ya nyumba.

Vijana wa kiume kuna haja ya kubadilika, huko mnakoelekea ni kubaya kutaharibu heshima yenu ya kuwa baba ndani ya nyumba.

Hata hivyo, kauli nyingine ambayo iliwahi kutolewa na Rais Dk. Magufuli ni ile ya aliyoitoa mwaka 2017, akisema chini ya uongozi wake watoto watakobeba mimba shuleni hatawapa nafasi ya kurudi shuleni.

Kauli hii aliitoa akiwa kwenye mkutano wa hadhara Chalinze. Ambapo baada ya hapo iliibuka mijadala mbalimbali kutoka kwa wanasiasa, wanaharakati na makundi ya kijamii, wengine wakiunga mkono na wapo ambao hawakukubaliana nayo wakisema inamkosesha haki ya msingi ya mtoto wa kike kupata elimu.

Msimamo wa Rais Dk. Magufuli ulikuwa kwamba mwanamume ambaye atapatikana na hatia ya kumpachika mimba mtoto wa shule, atafungwa jela miaka 30 na kutumia nguvu alizotumia kumpachika mimba msichana huyo, kufanya kilimo akiwa gerezani.

“Mashirika haya yasiyo ya serikali yanastahili kwenda kufungua shule za wazazi, lakini hayastahili kuilazimisha serikali kuwarejesha shuleni.

“Ninatoa elimu ya bure kwa wanafunzi ambao wameamua kusoma, na sasa mnataka niwaelimishe wazazi,” alisema.

Hata hivyo, walipingana na kauli hiyo walidai kwamba wanaopata mimba wakiwa shuleni si wote wanapenda, wengine hubakwa na ndugu zao au kwa wale waishio vijijini basi huwa ni vishawishi wanavyokumbana navyo njiani wakati wa kwenda shule au kurudi nyumbani.

Ripoti ya Shirika la Human Rights Watch, limebaini kuwa hapa nchini takriban wasichana 8,000 huacha shule kila mwaka kutokana na kupata ujauzito.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here