Serikali yakiri uhaba waandishi wa sheria

0
2613

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

SERIKALI imekiri kukabiliwa na uhaba wa wataalamu wa uandishi wa sheria, hali inayotatiza ubora wa sheria ndogo zinazoandikwa baada ya kupitishwa kwa miswada ya mabadiliko ya sheria na Bunge.

Hilo lilithibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Aleldarus Kilangi mwishoni mwa wiki mjini Dodoma, alipokuwa akitoa maelezo baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kueleza kubaini dosari  nyingi katika sheria ndogo.

Muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa mkutano wa 16 wa Bunge Ijumaa iliyopita, Prof.  Kilangi, alikiri kwa kusema kuwa ni kweli kwamba kuna uhaba wa wataalamu wa uandishi wa sheria, ambao ofisi yake imeanza kutafuta namna ya kumaliza tatizo hilo.

“Katika hatua ambazo tumeanza kuchukua ni kuhakikisha kwamba wanasheria wetu wengi wanafanywa pia kuwa mawakili wa Serikali kimfumo na kimuundo na linalofuata ni kuwaboresha kwa kuwaongezea uwezo wa kuwa waandishi wazuri wa sheria.

“Tayari tumeshaandaa mpango wa mafunzo ya waandishi wa Sheria na yanatarajiwa kuanza ndani ya miezi mitatu ijayo. Mafunzo haya yatahusisha wanasheria wa Serikali na idara zake, bila kuwasahau waliopo katika Idara ya Mahakama,” alisema.

Alisema ofisi ya Mwanasheria Mkuu inamalizia mchakato wa kutayarisha mafunzo hayo kwa kuanzisha chuo au taasisi maalumu ya mafunzo itakayokuwa endelevu ili kuzalisha wataalamu wa kutosha katika uandishi wa sheria, kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo kwa siku zijazo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu tatizo hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Andrew Chenge alisema Idara ya Sheria ndiyo moyo wa Serikali hivyo haistahili kupuuzwa na inahitaji wataalamu waliobobea katika maeneo yote.

Alisema tatizo la waandishi wa sheria limekuwapo wakati wote japokuwa kuna wakati Serikali iliwekeza kwa kiasi kikubwa na kupata waandishi bora wa sheria, ambao wengi sasa wamestaafu na wengine wanaelekea kustaafu, hivyo kusababisha ombwe katika eneo hilo.

“Ninaishauri Serikali iwekeze sana katika eneo hili la mafunzo ya waandishi wa sheria, ni eneo muhimu sana. Kwa sasa tunao waandishi wa sheria wachache na iwapo uwekezaji usipofanyika tatizo hili la kuwa na dosari katika sheria zetu litazidi kutusumbua,” alisema.

Alisema ni wazi kuwa kuna wanasheria wenye vipaji vya hali ya juu na kinachotakiwa ni kutoa mafunzo zaidi na kutokuwa wachoyo, ili wale waliopo, wenye uwezo na weledi mzuri warithishe mambo hayo kwa wengine, ili walisaidie taifa kwa siku zijazo.

Awali, alipokuwa akisoma taarifa ya Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye mkutano wa 14 na 15 wa Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, William Ngeleja alisema tatizo hilo limesababisha baadhi ya sheria ndogo kukinzana na sheria mama au sheria nyingine za nchi.

Alisema ni vyema mamlaka zote zilizopewa jukumu la kutunga sheria ndogo zifanye kazi kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa utungaji sheria hizo, kwa lengo la kuondoa dosari zinazojitokeza katika sheria hizo.

Ngeleja alisema Ofisi ya Mpiga Chapa wa Serikali pia inatakiwa kufanya uhariri kwa pamoja na mamlaka zinazohusika na sheria ndogo kabla ya hatua ya uchapaji kwa lengo la kuondoa dosari zinazojitokeza.

“Kamati inashauri Serikali kuchukua hatua za haraka kuzifanyia marekebisho sheria ndogo zenye dosari baada ya marekebisho hayo kufanyika na kuchapishwa katika gazeti la Serikali. Sheria ndogo hizo ziwasilishwe bungeni kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Alisema tatizo la dosari hizo za kiuandishi zinazosababisha kukinzana ni kwenda kinyume na masharti ya Kifungu cha 36 cha Sheria ya Tafsiri za Sheria, kinachotoa sharti kwa sheria ndogo kutokwenda kinyume na sheria mama.

Alieleza kuwa kukinzana huko kunaifanya kanuni husika kuwa batili kwa kiwango ilichokinzana, hivyo wizara zilizohusiaka zinatakiwa kuzifanyia marekebisho ili kuondoa vifungu vinavyokwenda kinyume na masharti ya sheria mama na sheria nyingine za nchi.

Alisema uchambuzi uliofanywa na kamati umebainisha kuwa dosari za kiuandishi zilizobainika zimesababisha mantiki na madhumuni yaliyokusudiwa katika vifungu husika kutofikiwa na hivyo kuleta changamoto katika utekelezaji wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here