22 C
Dar es Salaam
Sunday, May 28, 2023

Contact us: [email protected]

HECHE: NATISHIWA KUUAWA, KUBAMBIKWA KESI

GABRIEL MUSHI Na RAMADHAN HASSAN


MBUNGE wa Tarime Vijini (Chadema), John Heche, amedai kwamba amekuwa  akitishiwa  uhai wake kutokana na msimamo wake wa kuikosoa Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dodoma jana, Heche alidai imekuwa kawaida mtu akiikosoa Serikali anatengenezewa mizengwe ikiwa ni pamoja na kutishiwa maisha.

Alisema vitisho hivyo alianza kuvipokea Februari mwaka huu alipozungumza bungeni kuhusu kupanda bei za vitambulisho vya taifa na utata kwenye gharama za mradi wa hati za kusafiria za  elektroniki.

Alisema   baada ya kuzungumza, alipokea vitisho  huku akidai baadhi ya watu walimwambia amegusa sehemu ambayo ni hatarishi.

“Imekuwa kawaida sasa ukiikosoa Serikali unatengenezwa mizengwe ya kuumizwa, kuwekewa sumu…ajali.

“Kama juzi ndugu Selasini (Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini) gari yake ilifunguliwa stadi za miguu, akaenda kuripoti polisi.

“Februari 2 bungeni, nilizungumza ufisadi wa vitambulisho vya taifa, upandaji wa bei ya vitambulisho na  kuhusu utengenezaji wa passport, e viza, border na mambo yanayohusiana na hayo.

“Baada kuzungumza hayo nilipata vitisho na baadhi wakaniambia nimegusa sehemu ambayo inahatarisha maisha yangu naweza kutengenezewa kesi.

Alisema   baada ya kuzungumza hivyo Februari 5 gazeti mojawapo   la kila wiki lilimhusisha na shambulio  la tindikali dhidi kijana mmoja,   Mussa Tesha.

“Nilisema Februari 3, ila Februari 5 gazeti lilinihusisha na shambulio la kumwagia mtu tindikali.

“Tarehe hiyo nikaandikwa na gazeti jingine la kila  wiki kuhusu wabunge wa Chadema katika kashfa nzito kwamba nimehongwa rushwa Sh milioni 100 na makampuni.

“Kuhusu ile e- passport, nikataka kushtaki ila nikaaamua kuwapuuza, ila Februari hiyo hiyo tukiwa kwenye kampeni za uchaguzi Kinondoni, tulitoka kula pale Break point.

Nilikuwa na Msigwa (Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter)  na Silinde (Mbunge wa Momba, David Silinde, wote Chadema) nikakutana na (ataja jina la mmiliki wa gazeti lililomwandika) akaniambia nitapotezwa, nikamwambia sipotezwi wala sitishwi.

“Aprili mwaka huu kimeanza kusambaa kipande cha video kikionyesha kwamba nimemwagia tindikali huyu Musa Tesha, lakini suala la tindikali kuna watu walishtaki, kesi ilienda hadi mahakama ya rufaa sikutajwa popote ila ghafla tu nimetajwa.

“Lakini anasema alinasa sura kipindi hicho ingawa tangu mwaka 2011 hakutambua jina langu licha ya umaarufu mpaka 2018 eti amekumbuka kuwa hii sura ni ya mtu alikuwa Heche,” alisema.

Mbunge huyo alisema ameona awaambie Watanzania suala hilo kwa sababu hali ni mbaya kama ilivyotokea kwa Meya wa Ubungo  (Chadema), Boniface Jacob.

“Viongozi wetu wanakamatwa ovyo wakiwamo madiwani wanahusishwa na maandamano ya tarehe 26 na wanaambiwa wataachiwa baada ya Muungano.

“Mimi ni mbunge nafanya kazi zangu za ubunge kwa usahihi, niwaambie hakuna mtu anaweza kunitikisa nisifanye kazi yangu, ni bora niache huo ubunge.

“Kama wanafikiri wanatengeneza kunitishia ni aibu kwa sababu kosa la miaka saba ndiyo unitambue leo wakati nilikuwa mwenyekiti wa Bavicha nimezunguka Igunga hajawahi kunitambua.

“Hii picha imetengenezwa kitaalamu kwa sababu imeandaliwa kutengeneza saikolojia kwa watanzania kuwa mimi ni mtu mnyama, hatari. Hivyo nimeona ni vema niwaambie Watanzania kuhusu hili,”alisema na kuongeza:

“Huwezi kuchukua kesi ya nyani umpelekee ngedere kwa sababu mambo mengi tumeripoti polisi hayajafanyiwa kazi”.

Alisema licha ya vitisho hivyo kamwe hawezi kujificha  kwa sababu mambo ya uongo hayawezi kudumu.

“Siwezi kujificha, nipo hapa, sitajificha kwa lolote hata nifungwe miaka 100 kwa sababu mambo ya uongo hayawezi kudumu,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,167FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles