28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

JPM:  KUNA KUTOAMINIANA EAC

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, amesema bado kuna vikwazo vya  biashara na uwekezaji na kutoaminiana ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akihutubia Bunge la Afrika Mashariki (EALA)  Dodoma jana, alisema kuna matatizo ya migogoro katika baadhi ya maeneo ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu wengi.

Alisema wabunge wa bunge hilo wanatakiwa kuzishughulikia haraka changamoto hizo huku wakiendelea kudumisha umoja na mshikamano.

“Ninyi wabunge wa Afrika Mashariki mnatakiwa kuanza kuzishughulikia mapema, umoja wetu unatakiwa uwe kama tulivyo marais, mawaziri, wabunge, watendaji hadi wananchi.

“Tupendane na tujione kama ndugu. Tukianza kuwa na ‘challenge’ (changamoto) tutashindwa kuwasaidia wananchi, Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ya wananchi si ya viongozi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa viwanda na kusababisha kuuza nje rasilimali zikiwa ghafi.

“Soko la watu milioni 170 ni kubwa, kama tuna mifugo mingi kwa nini tununue viatu kutoka Ulaya, na sisi sote tuliomo humu (bungeni) pamoja na wewe spika, kiatu chako hakikutengenezwa Afrika Mashariki.

“Kwa nini tununue nyama kutoka nje wakati tuna mifugo mingi?  Kwa nini tununue samaki wakati tuna bahari, maziwa na mito kila mahali? Maswali haya lazima tujiulize vizuri ili tuwasaidie wananchi wetu,” alisema.

Rais Magufuli alisema pia changamoto nyingine ni za miundombinu ya usafiri na   umeme na kwamba kwa nchi zote sita za Afrika Mashariki zina megawati 6,500 kiwango ambacho ni kidogo kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi.

SPIKA EALA

Naye Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Dk. Martin Ngoga, alisisitiza nia ya bunge hilo kutumia   Kiswahili na kutaka marekebisho ya mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo yafanyike haraka   iweze kutumika.

“Kuendelea kutumia lugha za wageni kunaifanya jumuiya na wale waliopewa nafasi ya kuiendesha waonekane kama ni tabaka fulani ambalo halina uhusiano wowote na wananchi tunaowatumikia.

“Hivyo hatujisikii vizuri hata kidogo tunapokwenda katika mikutano ya Umoja wa Afrika (AU) tunakikuta Kiswahili lakini tukiwa nyumbani tunazungumza  Kiingereza,” alisema Dk. Ngoga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles