HATOKI MTU

0
931

Winfrida Mtoi –Dar es salaam

YANGA inashuka dimbani leo kuumana na timu ya Zesco ya Zambia, katika mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika michuano hiyo, walitinga hatua hiyo baada ya kuifurusha  Township Rollers ya Botswana kwa ushindi wa jumla wa bao 2-1.

Yanga ilianza kulazimishwa sare ya bao 1-1 , katika mchezo uliochezwa  Agosti 10, Uwanja wa Taifa kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano jijini Gaborone, Botswana.

Kikijiweka sawa kabla ya kushuka dimbani leo, kikosi cha Yanga kilipiga kambi ya wiki moja jijini Mwanza na kucheza mechi mbili za kirafiki, ikianza kuivaa Pamba na kulazimisha sare ya bao 1-1 kabla ya kuitungua Toto Africans  mabao 3-0.

Wapinzani wa Yanga, Zesco ilifuzu hatua hiyo, baada ya kuitoa mshindanoni Green Mamba ya Eswatini kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.

Zesco ilianza kushinda mabao 2-0 ugenini kabla ya kurejea nyumbani Zambia na kutakata kwa bao 1-0.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na sababu kuu moja nayo ni mabenchi ya ufundi ya timu hizo kufahamiana.

Ikumbukwe kwamba, Kocha Mkuu wa Zesco, George Lwandamina aliwahi kuinoa Yanga kabla ya kuikacha na kurejea katika kikosi chake cha sasa.

Baada ya Lwandamina kutimka, Yanga ilimkabidhi makujumu Mwinyi Zahera, ambaye anawanoa vijana hao wa Jangwani kwa sasa.

Kwa upande mwingine, Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila aliwahi kufanya kazi na Lwandamina wakati huo akiwafundisha mabingwa hao mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hii ina maana kwamba,  kwa kiasi kikubwa Lwandamina na Mwandila ambao wote ni raia wa Zambia, kila mmoja atakuwa anamfahamu mwenzake.

Timu hizo zitakutana zikiwa na rekodi tofauti katika michuano hiyo.

Mafanikio ya juu kabisa ya Yanga katika michuano hiyo ni kufika hatua ya makundi mwaka 1998, wakati kwa upande wa Zesco ilitinga robo fainali mwaka 2017.

Zesco imeshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa mara tano, tangu ilipoanzishwa mwaka 1974, wakati Yanga imefanya hivyo mara 11, tangu ilipoanzishwa mwaka 1935.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa leo, Zahera, alisema anafahamu Zesco ina rekodi bora zaidi yao katika michuanoa hiyo, lakini yeye ni mwalimu anajua njia gani atapita kupata ushindi.

“Nimekaa na wachezaji wangu na kupitia video za wapinzani, tulifanya hivyo pia  kwa Township Rollers, naamini maandalizi yametosha,” alisema Zahera na kuongeza.

“Kikosi chetu kilikuwa na udhaifu katika kufunga mabao, lakini nafasi tunatengeneza nyingi, nimefanyia kazi naamini sasa hawataniangusha.”

Kwa upande wake Lwandamina alisema  licha ya kuwahi kuinoa Yanga, lakini hilo haimfanyi kujiamini kwamba watashinda kirahisi badala yake wanatakiwa kupambana.

“Tunaingia katika mchezo kutafuta ushindi, niliwahi kuwa mwalimu wa Yanga lakini hilo peke yake haliwezi kutusaidia zaidi ya kupambana kwa dhati,” alisema Lwandamina.

Yanga leo inaweza kuanza hivi; kipa Farouk Shikalo, Feisal Salum, Papy Tshishimbi, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Ally Mtoni, Mapinduzi Balama, Juma Balinya, Sadney Urikhob  ,Abdulazizi Makame na Patrick Sibomana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here