Van der Sar awafungulia milango United

0
552

Manchester,England

MLINDA mlango wa zamani wa timu ya Manchester United, Edwin van der Sar, ameifungulia milango timu hiyo kuja kumpa nafasi ya uongozi mara baada ya kumaliza mkataba wake ndani ya Ajax.

Kipa huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 48, kwa sasa ni Mkurugenzi wa michezo wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Uholanzi, Ajax.

Miezi kadhaa iliopita kulikuwa na taarifa kwamba mchezaji huyo anawindwa na Manchester United ili kuja kuiongoza timu hiyo, lakini alikanusha na kudai hakuna ukweli wowote juu ya habari hizo, ila kwa sasa amedai yupo tayari kukaa mezani mara baada ya kumaliza mkataba wake Ajax.

“Kwa sasa hauwezi kujua, najua Ajax ina utaratibu wake na nimetenga muda wangu wote kwa ajili ya timu hii, lakini chochote kinaweza kutokea hapo baadae.

“Kwenye maisha ya soka unatakiwa kukubali kujifunza mambo mengi, hapa nilipo nimejifunza na ninaendelea kujifunza, kuna maisha baada ya hapa hivyo chochote kinaweza kutokea.

“Wakati ninacheza mpira nilipita kwenye klabu mbalimbali kwa ajili ya kujifunza pia ni sehemu ya maisha yangu, hivyo kazi ambayo ninaifanya Ajax ninaweza kwenda kufanya sehemu yoyote mara baada ya hapa.

“Tumepambana kuhakikisha Ajax inasimama na kuwa moja kati ya timu bora duniani hasa kwenye michuano ya Ulaya, tumefanya hivyo msimu uliopita na tunaamini tutafanya hivyo tena,” alisema Van Der Sar.

Mchezaji huyo aliongeza kwa kuwataka Manchester United wapambane ili kuhakikisha mlinda mlango wake David de Gea anasaini mkataba mpya wa kumfanya awe hapo kwa kipindi kirefu.

“Wapo walinda milango ambao wanaweza kuziba nafasi ya David de Gea, lakini sio kazi rahisi, litakuwa pigo kubwa kwa Manchester United endapo watakubali kumuacha mchezaji huyo akiondoka.

“Ninaamini mazungumzo bado yanaendelea kuhakikisha anasalia, lakini wakishindwa kufanya hivyo lazima wapambane kutafuta kipa ambaye ataziba nafasi hiyo,” aliongeza Van Der Sar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here