29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Hatima ya Mbowe, Matiko leo Dar

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

HATIMA ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kuwa nje kwa dhamana ama kuendelea kusota rumande, inatarajiwa kujulikana leo wakati Mahakama Kuu itakapotoa hukumu baada ya kusikiliza rufani ya kupinga kufutiwa dhamana.

Uamuzi huo ulitolewa jana mbele ya Jaji Sam Rumanyika, baada ya kusikiliza rufaa iliyokatwa na kina Mbowe dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.

Warufani waliwakilishwa na jopo la mawakili wakiwamo Peter Kibatala na Jeremaya Ntobesya huku Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, Paul Kadushi, Wakili wa Serikali Jackline Nyantori, Simon Wankyo na Salim Msemo.

Sababu ya kwanza warufani wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kufuta dhamana kwa washtakiwa wakati wao wenyewe walifika mahakamani Novemba 12, 2018 na walikuwepo Novemba 23, 2018 dhamana yao ilipofutwa.

Wanadai sababu ya pili ni kwamba mahakama ilikosea kufuta dhamana kwa washtakiwa bila kuwapa wadhamini nafasi ya kuonesha kwanini dhamana yao ya maandishi isifutwe.

Wakiwasilisha hoja hizo za rufaa, Wakili Kibatala aliomba mahakama ione rufaa yao ina mashiko, itengue uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kwa sababu ilikosea kufuta dhamana kwa washtakiwa, na hapakuwa na sababu yoyote ya msingi ya kufanya hivyo.

Alidai siku ambazo washtakiwa hawakuwepo mahakamani, wadhamini wao walikuwepo na walitoa taarifa na kwamba ilikuwa makosa kisheria Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainabu Mangu aliyekuwa akiendesha kesi hiyo kuapa kwa ajili ya kuithibitishia mahakama kwamba washtakiwa wameruka dhamana hivyo wafutiwe.

“Warufani hawakupewa nafasi ya kuwasilisha kiapo kinzani, ilikuwa si sahihi kwani kiapo hicho kiliathiri maelezo ya washtakiwa kuonekana ya uongo,” alidai Kibatala.

Akiongezea Wakili Ntobesya alidai badala ya mahakama kuwafutia dhamana warufani, ilitakiwa kuchukua dhamana za maandishi walizosaini wadhamini kwani waliingia mkataba na mahakama kuhakikisha washtakiwa wanahudhuria katika kesi.

Akijibu Wakili Nyantori alidai hakuna sababu za msingi za kuifanya rufaa hiyo ikubaliwe, dhamana ilifutwa kwa sababu kulikuwa na ucheleweshaji wa makusudi wa kesi.

Alidai adhabu ya mdhamini haihusiani na adhabu ya mshtakiwa kwani kila mmoja anabeba msalaba wake na kwamba uvunjaji wa masharti ya dhamana unaondosha haki ya dhamana kisheria.

“Wakata rufani walijiondolea haki yao wenyewe kwa kuvunja masharti ya dhamana, haki ya kusikilizwa kabla ya kufutwa waliipata,” alidai Nyantori.

Wakili Nchimbi alidai kiapo kilipowasilishwa mahakamani Kibatala hakuomba kuwasilisha kiapo kinzani, rai ya Jamhuri kwamba rufaa hiyo haina mashiko itupiliwe mbali na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uachwe uendelee kusimama.

Wakili Kibatala akiwasilisha hoja za nyongeza alidai aliomba kuwasilisha kiapo kinzani, lakini hakujibiwa na badala yake hoja nyingine zilisikilizwa na uamuzi wa kufutwa dhamana ya warufani ukatolewa.

Jaji Rumanyika baada ya kusikiliza pande hizo mbili, aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa saba mchana kwa ajili ya kutoa hukumu.

Mbali na Mbowe na Matiko, washtakiwa wengine wanaoshtakiwa nao katika kesi ya jinai namba 112 ambao wote ni viongozi wa Chadema ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16 mwaka 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles