25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wanazuoni: Kingunge alikuwa mtu huru

ANDREW MSECHU-DA ES SALAAM

WANAZUONI waliokusanyika Dar es Salaam jana, wamemwelezea marehemu Kingunge Ngombale Mwiru kuwa mfano wa kuigwa kutokana na misimamo na mitazamo yake wakati wa uhai wake, wakisema alikuwa mtu huru asiyetetereka.

Wakizungumza katika uzinduzi wa kitabu cha ‘Mazungumzo na “Kingunge” wa Itikadi ya Ujamaa’, kilichoandaliwa na Kavazi la Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam jana, walisema katika maisha yake alionesha dhamira ya utetezi wa watu wanaoonewa na hakuwahi kukubali jambo asiloliamini hata kama lingekuwa na matokeo yenye madhara kwake.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, mchapaji wa vitabu Walter Bgoya, alisema alimfahamu Kingunge kama msomi makini wa Sayansi ya Jamii, ambaye hakupenda majivuno wala kuonesha usomi wake, hivyo waswahili wengi kudhani ni mtu mwenye kipaji tu.

“Alikuwa rafiki yangu wa karibu tangu miaka ya 60, tulikua na tulifanya kazi pamoja muda mwingi, katika maisha yake alichukia sana kuona mtu akidhulumiwa. Katika mwenendo huo, alichukia sana hatua ya CCM kutopitisha jina la Lowassa (Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa) katika uchaguzi mkuu wa 2015.

“Aliumia sana kwa kashfa iliyomsababisha Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa kuwa aliamini alifanya hivyo si kwa akuwa alikuwa na kosa bali ili kuinusuru Serikali. Alijua ilipangwa kufanyika utaratibu wa kumsafisha ndani ya chama, lakini haukufanyika, suala hili liliongeza mzigo kwa Kingunge,” alisema.

Alieleza kutokana na mambo hayo, alipochukua uamuzi wa kujiweka kando CCM na kuingia upinzani ambako alikuwa miongoni mwa washauri wakuu, aliacha maswali mengi ambayo hadi leo hayajibiki. 

Akimzungumzia Kingunge, mwanahabari wa siku nyingi nchini, Jenerali Ulimwengu, alisema aliwahi kuwa karibu naye na anatambua kuwa alikuwa ni zao la makutano ya harakati tofauti katika kipindi kimoja, suala lililomjenga kuwa kiongozi wa aina yake.

Alisema kutokana na umahiri wake, Kingunge alikuwa kiungo hai kati ya matumaini na matarajio ya Watanzania na harakati za ukombozi zilizokuwa zikiendelea katika nchi za dunia ya tatu.

“Alikuwa mtu mwenye utashi na uwezo mkubwa wa kujieleza au kutetea jambo. Alikuwa mwanasiasa wa kipekee. Wengi wanaojiita wanasiasa na wanaofanya siasa leo si wanasiasa bali ni wanamipango wanaofanya mipangilio,” alisema.

Alisema Kingunge alikuwa mtu huru ndani ya mfumo uliokuwepo kwa kuwa alikuwa haogopi kusema na kutetea anachokifikiri na anachokiamini na kuchukua hatua inayofaa, tofauti na wanasiasa hawa wa mipango.

Mtaalamu wa lugha za kigeni, Profesa Martha Qorro, ambaye alielezea kumfahamu Kingunge kutokana na urafiki wake na Patrick Qorro, alisema alimuona kuwa kiongozi makini, shupavu na imara, mwenye ushawishi na uwezo mkubwa wa kufanya mambo.

Mwingine aliyemzungumzia Kingunge ni Profesa Hamudi Majamba ambaye alisema alimfahamu kama mume wa dada yake, lakini pia mlezi na mshauri aliyemsaidia katika vipindi vyote, hasa alipopata matatizo ya kufukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1991 kwa madai ya kumtukana Rais matusi ya nguoni.

Alisema katika yote, Kingunge ambaye alifariki akiwa upinzani, tangu alipochukua uamuzi wa kujiweka kando CCM, aliendelea kusisitiza kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na kukiukwa kwa kanuni walizokuwa wamejiwekea, hivyo aliamua kukaa kando kwa kuwa yeye si mkubwa kuliko chama.

Jaji Joseph Warioba, alisema alifahamiana na Kingunge walipoanzisha kikundi cha kujisomea cha TANU mwaka 1966 wakiwa na akina Bgoya, Lawrence Gama, Patrick Qorro na wengine na kuwa alimtambua kuwa mtu anayejiamini na aliyesema anachokiamini bila woga.

Alisema alipokuwa Waziri Mkuu, iwapo kuna jambo lililokuwa likimtatiza na kutaka watu watakaomwambia ukweli alikuwa akiwaita Kingunge, Qorro na Bgoya ambao waliweza kutofautiana kifikra hadi kupata suluhu ya jambo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles