25.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 2, 2024

Contact us: [email protected]

Hasunga asema wizara yake haijafanya vizuri kutafuta masoko ya mazao

Mwandishi Wetu-Dodoma                                                                       

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema bado wizara na taasisi zake, hazijafanya vizuri kwenye kutafuta masoko ya mazao ya wakulima na hazijafanikiwa kufikia lengo la uzalishaji wenye tija na kuwezesha kilimo kiwe cha kibiashara.

Alisema hayo jana Dodoma wakati wa kikao kazi cha watendaji wa wizara, taasisi na bodi za mazao wakijadili taarifa za utekelezaji wa malengo ya mwaka 2018/19.

 “Takwimu zinaonyesha hatujafanya vizuri kwenye kusaidia upatikanaji wa masoko ya mazao ya wakulima nchini kwa kipindi cha mwaka 2018/19,” alisema Hasunga.

Alisema jukumu la wizara ni kuhamasisha uzalishaji na kuhakikisha mazao ya wakulima yanaongezwa thamani  ili kuwa na soko la uhakika.

Hasunga alisema changamoto ya masoko kwa mazao ya wakulima inahitaji kuwekewa mfumo mahususi wa utatuzi, hivyo ni jukumu la wataalamu kuja na mipango mizuri ya utekelezaji.

“Wizara yetu inasimamia aina 85 za mazao nchini, hii inafanya wizara kuhitaji weledi na utaalamu kupata ufumbuzi wa haraka wa changamoto za mazao haya,” alisema Hasunga.

Alitaja malengo sita ambayo Serikali ya awamu ya tano inatumia kupima utendaji kazi wa wizara hiyo kwa mwaka 2019/20, kwamba ni kuhakikisha nchi inazalisha chakula cha kutosha na kuwa na usalama wa chakula.

Pia kilimo kinachochangia upatikanaji wa fedha za kigeni, kilimo kinatoa mchango katika pato la taifa zaidi ya asilimia 30.

Alisema nyingine ni kujua malighafi kiasi gani inapatikana kwa matumizi ya viwandani, kiasi gani cha ajira kinazalishwa katika sekta ya kilimo na sita ni namna gani wizara inasimamia ushirika nchini kuwa na tija na kuondoa kero.

Katika hatua nyingine, Hasunga aliwapongeza watendaji waliopo chini ya wizara hiyo kwa utendaji mzuri uliofanikisha Tanzania kuongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kati ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2019.

“Nawapongeza wote waliosaidia nchi yetu kuzalisha mahindi kwa asilimia 103 na kuongoza Afrika Mashariki, hali iliyofanya nchi kuwa na utoshelevu wa chakula wa asilimia 119,” alisema Hasunga.

Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga, alisema katika mafanikio ya zao hilo hadi Septemba, tani 301,132 zimekusanywa toka kwa wakulima ikilinganishwa na tani 222,039 mwaka jana.

Alisema pia Bodi ya Pamba imefanikiwa kusambaza chupa milioni sita za viuatilifu kwa wakulima msimu huu wa 2019/20 ili kudhibiti magonjwa kwenye zao hilo.

Mtunga alisema zao la pamba linakabiliwa na changamoto ya soko kutokana na ukosefu wa wanunuzi wa uhakika.

“Tunaiomba Serikali iingilie kati suala la upatikanaji wa soko la uhakika la pamba, hususani katika Mkoa wa Katavi ambako mvua sasa imeanza kunyesha na wakulima bado hawajauza pamba yao,” alisema Mtunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles