27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Hakimu: Kesi ya kina mbowe ni mgogoro

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

HAKIMU Mkazi Mkuu, Thomas Simba, amesema kesi inayowakabili viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (Chadema) akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, imetawaliwa na migogoro mwanzo mwisho.

Alisema kesi hiyo ina mgogoro, kwani kusikilizwa mgogoro, kuahirishwa mgogoro na ndiyo sababu zilizofanya ichelewe kuisha hadi sasa.

Hakimu Simba alisema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati Gaston Shundo anayemwakilisha wakili Peter Kibatala, akiomba ahirisho la siku 20 kwa sababu mawakili wa washtakiwa hawapo.

Kina Mbowe walitakiwa kuanza kujitetea, lakini wakili Gaston alidai mawakili wanaowatetea washtakiwa wako Mahakama Kuu.

Alisema Profesa Safari yuko Shinyanga, Kibatala yuko Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Wakili Hekima Mwesipo yuko Mahakama Kuu Tanga.

Wakili huyo alidai pia mshtakiwa Mchungaji Peter Msigwa kafiwa na bibi yake na John Heche kafiwa na mtoto wa kaka yake, Alphonce Mwita hivyo walihitaji kwenda kwenye maziko.

Aliomba kesi hiyo iahirishwe hadi Oktoba 7 ama 10 washtakiwa kuanza kujitetea.

Akijibu hoja hizo, Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi alidai hoja ya kwanza haina msingi sababu mawakili wako wengi, akiwemo Jeremiah Myobesy, John Mallya na wengine ambao wanaweza kuendesha kesi kama wenzao hawapo.

Nchimbi alidai hakuna hati za wito zinazoonyesha mawakili hao wako katika mahakama hizo, lakini katika hoja ya kufiwa alidai ni suala la kibinadamu.

Aliomba kama mahakama itakubali kuahirisha iahirishe isipokuwa ipange tarehe ya karibuni.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba alisema kutokana na mazingira hayo kesi kwa jana isingeweza kuendelea.

“Hii kesi mgogoro, kuanzia kusikilizwa hadi kuahirishwa, migogoro ndiyo ilisababisha ichelewe hadi leo.

“Naamini wenzetu wamefiwa na mawakili wako Mahakama Kuu, siridhishwi kama ni busara kuahirisha kesi kwa siku 20, haujaletwa uthibitisho kwamba mawakili hawatakuwepo mpaka Oktoba 7.

“Tunalalamikiwa kuchelewesha mashauri na hili likiwemo, tuondoke katika hii migogoro ambayo inazuka hata katika kuahirisha,” alisema Hakimu Simba.

Aligoma kuahirisha kwa muda wanaotaka wa siku 20, badala yake aliahirisha kesi hiyo na kuipanga isikilizwe mfululizo kuanzia Septemba 24 hadi 27 na Oktoba 1 hadi 3.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na  wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai, ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, Ester Bulaya alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Februari 16, mwaka huu Barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, wanadaiwa kufanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara, mshtakiwa Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki.

Heche anadaiwa kuwa alitamka maneno yaliyoelekea kuleta chuki kati ya Serikali na Watanzania kwamba; “kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii… wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano… watu wanapotea… watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome…”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles