23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kwaheri mwanahabari Godfrey Dilunga

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MHARIRI wa gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga, amefariki dunia baada ya kuugua maradhi ya tumbo.

Dilunga aliyekuwa akipatiwa matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), tangu Septemba 9, mwaka huu alifariki dunia jana alfajiri wakati akiendelea kupata matibabu.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Jamhuri Media Ltd, Deodatus Balile, ilieleza kuwa awali Dilunga alikuwa amelazwa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala kutokana na tatizo la maumivu ya tumbo.

Alisema baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako madaktari na wauguzi walijitahidi kuokoa maisha yake, lakini Mungu alimpenda zaidi.

Balile alisema uongozi wa Kampuni ya Jamhuri kwa kushirikiana na familia ya marehemu wanaandaa utaratibu wa kuaga mwili Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika mkoani Morogoro ambako alizaliwa.

“Tunaendelea na taratibu za kuandaa mipango ya mazishi ya mwenzetu Dilunga, ambayo yatafanyika mkoani Morogoro ambapo mwili utasafirishwa kesho (leo),” alisema Balile.

Akizungumzia historia ya Dilunga, alisema aliajiriwa na kampuni hiyo tangu Februari mosi mwaka huu, akiitumikia nafasi ya Mhariri wa gazeti hilo hadi mauti yalipomfika.

Alisema kabla ya kujiunga na Jamhuri, Dilunga aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Habari Corporation akiwa mwandishi na baadaye mhariri wa magazeti ya Rai na MTANZANIA.

Hata hivyo baada ya mabadiliko ya muundo wa kampuni, alijiunga na kuwa mhariri wa gazeti la kila siku la Raia Mwema.

Pia alisema kwa muda mfupi aliofanya kazi  katika gazeti la Jamhuri amekuwa mtu wa msaada na ametoa mchango mkubwa katika kuboresha maudhui ya gazeti hilo la uchunguzi.

“Hakika pengo lake ni vigumu kuzibika. Tunasikitika tumempoteza mtu muhimu ndani ya tasnia ya habari,” alisema Balile.

Balile aliwashukuru madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mwananyamala na Muhimbili, wahariri, waandishi wa habari, maofisa uhusiano, wanasiasa na watu mbalimbali ambao walifika hospitalini kumjulia hali wakati wa ugonjwa wake.

Dilunga aliyezaliwa Oktoba 28, mwaka 1976, ameacha mjane na watoto watatu.

‘Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe, amen’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles