*Ni wa Kinyerezi II uliogharimu Mabilioni
Na Jonas Mushi, Dar es Salaam
HARUFU ya kuwapo jipu la ufisadi katika mradi mkubwa wa umeme wa Kinyerezi II imebainika, huku Serikali ikitoa dhamana kwa kampuni inayoujenga.
Mradi huo uliozinduliwa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, umegharimu zaidi ya Sh trilioni 1.6.
Kutokana na namna ilivyoendeshwa tenda hadi kupatikana Kampuni ya Sumitomo ya nchini Japan, baadhi ya wanasiasa walipiga kelele kuhusu gharama kubwa kuliko mahitaji halisi ya mradi huo.
Fedha za ujenzi wa mradi wa Kinyerezi II zinatokana na ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Japan wakati ujenzi wa Kinyerezi III na IV zitatokana na ubia kati ya Serikali na kampuni ya Kichina.
Taarifa za ndani kutoka ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), zinaeleza kwamba asilimia 12 ya fedha hizo zinatoka serikalini, huku nyingine zikiwa ni mkopo kutoka katika benki moja ya nchini Japan.
Mradi huo unatarajia kuzalisha umeme megawati 239.5, ambapo mitambo yake itatumia gesi asilia kutoka Mtwara.
Taarifa zinaeleza kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Mtwara na Lindi na pia ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara.
GHARAMA YA MRADI
Kwa mujibu wa mkataba ulioingiwa kati ya Tanesco na Kampuni ya Sumitomo iliyopewa tenda hiyo kwa njia ya kawaida bila kutangazwa, gharama za mradi ni kubwa na bei ya uuzaji wa umeme ukishazalishwa ni ya juu kulinganisha na kampuni nyingine.
Kampuni ya Tallawara Power Station ya nchini Australia ilionyesha nia ya kujenga mradi huo kwa gharama ya dola milioni 350 na kuiuzia Tanesco umeme kwa dola 875 kila kilowati moja wakati Sumitomo ikiuza kwa dola 1,488.
Serikali ya Tanzania ilisaini mkataba huo wa ujenzi wa mradi huo mwishoni mwa mwaka jana na hata kutoa dhamana kwa kampuni hiyo ambayo tayari imeshapata fedha za mkopo, huku mradi ukiwa bado unasuasua kuanza kujengwa.
MASWALI TATA
Pamoja na Serikali kuonyesha nia njema ya ujenzi wa mtambo wa Kinyerezi II, lakini bado kumekuwa na maswali ambayo yanakosa majibu ikiwamo kwanini mradi huo umetolewa kwa kampuni hiyo kwa mfumo wa kawaida bila kufuata sheria za manunuzi.
Mkopo uliokopwa na Sumitomo kwa dhamana ya Serikali huku wao wakiwa hawana kitu, nani ataulipa pamoja na riba yake kwa kila mwezi?
Kampuni ya Sumitomo itaendesha mradi huo kwa ubia ambapo yenyewe itakuwa na hisa asilimia 60 na Serikali asilimia 40 je, kwanini hakuna uwazi katika hili?
Ingawa hivi sasa Serikali ipo katika vita dhidi ya ufisadi je, viongozi wake wanajua kuwa kuna hatari ya kupoteza zaidi ya Sh bilioni 360 katika mradi huu huku mwekezaji aliyepewa dhamana akinufaika yeye?
KAULI YA TANESCO
MTANZANI ilipomtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba, alisema taarifa hizo si sahihi na hakuna sheria iliyokiukwa.
“Takwimu unazonipa hazina ukweli wowote na kama unataka taarifa kuhusu mradi wa Kinyerezi II njoo nikupeleke kwa wasimamizi wa mradi waweze kukupa taarifa sahihi za mradi huo,” alisema Mhandisi Mramba.