33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu bure majanga

Rais Dk. John MagufuliNA WAANDISHI WETU, DAR/MIKOANI

MPANGO wa Rais Dk. John Magufuli kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari umeanza kwa kusuasua na kuashiria mwanzo mbovu wa huduma hiyo iliyokuwa imepokewa kwa mikono miwili na wananchi.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA katika maeneo mbalimbali nchini, unaonyesha fedha za ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya kuhudumia mahitaji mbalimbali kwa kipindi cha mwezi mmoja tu wa Januari hazitoweza kukidhi mahitaji.

Katika baadhi ya shule jijini Dar es Salaam imebainika kuwa kiwango cha fedha kilichotolewa na Serikali hakilingani na mahitaji yanayokusudiwa.

Ruzuku inayotolewa katika shule hizo inalenga kugharamia ununuzi wa vitabu vya kiada na ziada, vifaa vya kufundishia zikiwamo chaki, madaftari, kalamu za risasi na wino, karatasi za kufanyia mitihani, ukarabati miundombinu ya shule na shughuli za utawala.

Hatua ya Serikali kutangaza kutoa elimu bure kuanzia msingi hadi sekondari ilipokewa kwa furaha kubwa, huku wananchi wengi wakiwa na matarajio kwamba sasa habari ya michango na ada itakuwa ahueni kwao  Wengi walikuwa na matarajio hayo kutokana na kuwapo kwa michango mbalimbali shuleni pamoja na gharama kubwa za ada katika shule binafsi na Serikali.

Hata hivyo, kumekuwapo na mitizamo tofauti juu ya mpango huo, huku baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari wakionyesha wasiwasi wao kama utatekelezwa ipasavyo.

Walimu wengine waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walirejea Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), ambapo pia Serikali ilikuwa inatoa fedha za ruzuku shuleni.

Lengo la ruzuku hiyo kwa kila mwanafunzi ilikuwa ni kuziba pengo la mapato lililotokana na kuondolewa kwa ada mashuleni.

Ruzuku hiyo pia ililenga kuinua ubora wa elimu kwa kuhakikisha kuwa rasilimali muhimu zinapatikana shuleni.
Ililenga hasa kugharimia ununuzi wa vitabu vya kiada na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kugharamia ukarabati, gharama za utawala na mitihani.

Katika MMEM ruzuku ya uendeshaji kwa kila mwanafunzi ilikuwa Sh 10,000 kwa mwaka lakini hata hivyo baadhi ya shule zilikuwa zikipelekewa fedha pungufu.

Hata hivyo, sera iliyopitishwa awali ya ugawaji wa ruzuku kwa wanafunzi ya dola 10 za Marekani kwa kila mwanafunzi haikuwahi kufuatwa.

Na wakati mwingine fedha hizo zilikuwa hazifikishwi kwa wakati na pengine kutokufika kabisa ambapo baadhi ya walimu walikiri hilo walipozungumza na gazeti hili mwishoni mwa mwaka jana.

Hivyo waliposikia kuwapo kwa mpango wa elimu bure, wengi walikumbuka MMEM na kutoa angalizo kwamba madudu yake yasije yakajirudia katika utekelezaji wa sasa wa elimu bure.

Hivi karibuni, Serikali ilitangaza kuwa imekwishatenga Sh bilioni 137 kugharamia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikaririwa na vyombo vya habari akisema fedha zipo na tayari zimeshaanza kusambazwa.

“Hatuhitaji mwanafunzi achangishwe fedha ya mitihani, na zile shilingi 10,000 kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma sekondari nazo pia tutazipeleka.

Na huu ni mpango wa dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwahiyo tutalazimika
kuziombea kibali.

“Serikali imekwishafanya hesabu za kubaini kiasi kinachohitajika kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa wale walioko bweni na wale wa kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa tutazimudu.

“Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na sisi tumedhamiria kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi tutatekeleza,” alisema Majaliwa.

Wiki iliyopita Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alithibitisha kupelekwa kwa fedha hizo kwa kila shule lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanaanza muhula wa masomo bila kulipa
ada.

MTANZANIA lilipozungumza na baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari walikiri kupokea fedha kwa ajili ya utekekezaji huo.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makongo, Emerenciana Kallanga, alisema kwa awamu ya kwanza ya Januari mwaka huu shule yake imepokea Sh 600,000 lakini kiasi hicho hakitoweza kukidhi mahitaji ya shule yake yenye jumla ya wanafunzi 1,255 kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba.

“Tuna mahitaji mengi ikiwamo kununua zana za kufundishia, maji, umeme, mlinzi ambaye mshahara wake kwa
mwezi tunamlipa Sh 300,000, hapo bado matumizi mengine ya lazima kwa shule,” alisema.

Alisema pia zana za kufundishia zinahitajika kwa wingi kwa kuwa shule hiyo ina wanafunzi wengi.
“Serikali imetuambia kuwa
fedha hizo zitatolewa kwa awamu, mwezi huu ndiyo tumetumiwa kiasi hicho, kwa Januari tutakuwa na wiki mbili tu zilizobaki, sasa tunasubiri hizo awamu nyingine tuone tutapewa kiasi gani,”

alisema mwalimu huyo. Mmoja wa walimu wakuu katika moja ya shule za msingi jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina lake wala shule yake gazetini, alisema amepokea Sh 1,194,000.
Kulingana na mwalimu huyo, amepewa maelekezo kuwa kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya ukarabati (asilimia 30), vifaa (asilimia 30), mitihani (asilimia 20), michezo (asilimia 10) na utawala (asilimia 10).

Alifafanua kuwa fedha za ukarabati ni Sh 358,200, vifaa vya shule Sh 358,200, mitihani Sh 238,800 na nyingine za michezo na utawala.

“Yaani ni kichekesho sijui hata tufanyeje maana kama hizi fedha za vifaa nikisema ninunue chaki, ‘makapeni’ na maandalizi ya walimu zinakuwa tayari zimeisha,” alisema mwalimu huyo.

Kuhusu fedha za mishahara ya walinzi, mwalimu huyo alisema wameambiwa kwamba wakurugenzi ndio wamepewa jukumu hilo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya walimu wameonyesha wasiwasi wao na kudai kuwa hawatarajii
kama kutakuwa na matokeo mazuri katika utoaji wa elimu bure.

Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda, alisema tayari fedha zimepelekwa katika akaunti za kila shule.
Alisema fedha hizo zimepelekwa kulingana na idadi ya wanafunzi katika shule husika. Mapunda alisema ruzuku kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi itakuwa Sh 10,000 wakati kwa mwanafunzi wa sekondari itakuwa Sh 45,000 ambazo ni kwa ajili ya fidia ya ada na ruzuku.

“Fedha zitakuwa zikitolewa kila mwezi, hizi zilizopelekwa ni kwa ajili ya mwezi huu wa Januari. Kwa wanafunzi wa bweni hakuna cha kuchangia, chakula gharama zote zitagharamiwa na Serikali,” alisema Mapunda.

KITETO

Mpango huo wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari umegonga mwamba wilayani Kiteto mkoani Manyara baada ya baadhi ya walimu kuwataka wazazi kutoa Sh 20,000, debe nne za mahindi na maharage debe mbili
kwa wanafunzi wa bweni. Barua kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Lesoit, Parkosidi Kambi ambayo MTANZANIA imeona nakala yake, inawataka wazazi wa wanafuzi waliofaulu kujiunga na shule hiyo kuripoti
wakiwa na chakula pamoja na fedha hizo ili kuweza kukidhi mahitaji yao na kwamba hatua kali
zitachukuliwa kwa mzazi atakayeshindwa kumpeleka mwanafunzi shuleni.

Kwa mujibu wa barua hiyo, kila mwanafunzi wa shule hiyo ya bweni kwa wavulana na wasichana, anatakiwa kufika shuleni akiwa na godoro, shuka za kimasai mbili, kiti kimoja na meza yake pamoja na panga au fyekeo.

Akizungumza na MTANZANIA mmoja wa wazazi wa shule hiyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, alisema kwa maelekezo haya inaonyesha kuwa maagizo haya yatakuwa na manu-faa kwa uongozi wa shule kutokana na wazazi kulazimishwa huku kukiwa na agizo la Serikali kugharamia michango hiyo.

“Kinachotushangaza wazazi na ambacho jibu lake hatujawahi kupata hata siku moja ni kuhusu kushurutishwa kiti na meza kwa kila mwanafunzi anayejiunga na sekondari, haya madawati mbona hatuoni mabaki yake hata kama yamechakaa, huwa yanaenda wapi?” alihoji.

Kwa upande wake mwananchi Bakari Maunganya alisema uongozi wa wilaya hauwezi kukwepwa lawama kwa kuwa siku zote wanaona maagizo hayo na hawachukui hatua kwa wahusika.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Bosko Ndunguru, alisema shule zimegawanyika katika kuhudumiwa na Serikali.

Alisema Serikali itagharamia Sh 1,500 za chakula cha kila mwanafunzi kwa siku na zile zilizoanzishwa hivi karibuni wazazi watalazimika kuchangia Ndunguru alisema kila shule imepata mgawo kulingana na maelekezo yaliyotolewa na wizara na kusisitiza kuwa anaamini fedha hizo zitatumika kwa uadilifu kulingana na maelekezo yaliyotolewa na kwamba hatarajii wakuu wa shule kufanya kinyume na maagizo hayo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka, akizungumza kuhusu suala hilo, alisema atafuatilia kujua undani wake lakini alisisitiza kuwa Serikali haijakataza michango yote bali kuna baadhi lazima wazazi wachangie ili kuboresha shule zao.

MWANZA

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ibanda iliyopo Kata ya Mkorani jijini Mwanza, Bahati Parapara, alisema ruzuku iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya elimu bure haikidhi mahitaji.
Alisema Desemba 30 mwaka jana alipokea Sh 647,000 na watoto walioandikishwa shule ya awali ni 210, darasa la kwanza 230 na darasa la pili hadi la saba 1,250 ambapo shule ina jumla ya wanafunzi 1,690.

Mwalimu Parapara alisema fedha iliyotolewa ni ndogo kulinganisha na idadi ya wanafunzi ambayo ni kubwa.
Alisema mbali na fedha hizo, pia amepokea Sh milioni 5 za ujenzi wa matundu ya vyoo kutoka kwa mkurugenzi.

Mwalimu Parapara alisema wanaiomba Serikali kuongeza fedha mara mbili ya hizo zilizotolewa kwa sababu zilizotolewa hazitoshi.
“Mgawanyo wa ruzuku hiyo ni kwa ajili ya ukarabati asilimia 30, vifaa asilimia 30, mitihani asilimia 20, michezo asilimia 10 na utawala asilimia 10,” alisema Parapara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Buhongwa, Rehema Maruzuku, alisema amepokea ruzuku lakini hakuweka wazi kiasi ambacho amepelekewa.

Alisema fedha hizo zitasimamiwa na mwenyekiti wa mtaa, kamati ya shule, mratibu wa kata na ofisa wa halmashauri.
“Shule hii ina jumla ya wanafunzi 800, mgawanyo wa ruzuku hiyo ni kwa ajili ya ukarabati asilimia 30, vifaa asilimia 30, mitihani asilimia 20, michezo asilimia 10 na utawala asilimia 10,” alisema mwalimu Rehema.

Aidha ameitaka Serikali kutoa ruzuku hiyo kwa wakati ili kuepuka kulimbikiza deni kama yalivyo madeni ya walimu ambayo kila kukicha yanaongezeka kutokana na kutokulipwa kwa wakati.

KILIMANJARO

Baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, walisema utekelezaji wa sera ya elimu bure ni changamoto kwao.

Walimu hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema utekelezwaji wa sera ya elimu bure ni kiini macho kwa kuwa fedha zilizotolewa na Serikali ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya shule.

“Mwanzoni tulikuwa tukiendesha shule kwa ruzuku ndogo kutoka serikalini pamoja na michango ya wazazi, lakini bado tulipata shida katika uendeshaji wa shule.

“Fedha hizo hazijahusisha vitabu wala chakula kwa shule za kutwa,” alisema mmoja wa walimu hao.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari katika Manispaa ya Moshi, Tullo Fundi, alisema shule za Manispaa ya Moshi, zimepokea fedha za ruzuku za utekelezaji wa sera ya elimu bure zaidi ya Sh milioni 155.

Naye Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Msingi katika Manispaa ya Moshi, Agnes Methew, alisema shule iliyopata fedha kidogo katika manispaa hiyo ni Shule ya Msingi Kibo iliyopata Sh 97,000 na shule iliyopata fedha nyingi ni
Shule ya Msingi Azimio iliyopata Sh 501,000.

MTWARA

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Rahaleo mkoani Mtwara, Kulwa Gamba, alisema fedha zilizopelekwa shuleni kwake hazitoshi kwa kuwa kuna baadhi ya matumizi hayakuelekezwa.
“Tatizo kubwa litakalojitokeza ni jinsi gani ya kutumia hizo fedha, hasa ukiangalia malipo ya umeme, maji na mlinzi havipo kwenye hiyo ruzuku,” alisema Mwalimu Gamba.

Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bandari, Zainabu Dadi, alilalamikia fedha zilizopelekwa shuleni hapo bila kutaja ni kiasi gani.

CWT YAWAFUNDA WALIMU

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Yahaya Msulwa, aliwataka walimu wakuu kote nchini kutofumbia macho changamoto zote zinazowakabili kuhusu mpango wa serikali wa utoaji wa elimu bure.

“Sisi kama CWT tunaunga mkono mfumo wa elimu bure, lakini walimu wajiandae na changamoto nyingi, wategemee
kukutana na mambo mengi katika kutekeleza sera ya elimu bure, lakini wasizifumbie macho ili Serikali iweze kurekebisha mahali penye kasoro,” alisema.

KAULI YA SERIKALI

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, akizungumzia mgawanyo wa ruzuku hiyo ya Serikali, alisema kasoro zilizojitokeza zimechangiwa na maombi yaliyofikishwa kimakosa
na walimu wakuu wa shule husika.

“Suala la kutokea kwa upungufu wa fedha nadhani limechangiwa na kazi hiyo kuanza Desemba hali iliyosababisha walimu kujikuta wakishindwa kutoa hesabu zao kwa umakini kutokana na haraka walizokuwa nazo, lakini tunashukuru kwa kutukumbusha hivyo tutafuatilia na tukigundua tatizo tutarekebisha,” alisema.

Manyanya alifafanua kuwa Rais Magufuli alipotangaza elimu bure alimaanisha Serikali itatoa fedha za kulipia bili za umeme, maji, mshahara wa mlinzi na vifaa vya maabara.

Alisema wazazi wanatakiwa kuchangia huduma ndogondogo kama vile nauli za daladala, madaftari, mabegi, kalamu na nguo za shule za wanafunzi.

Habari hii imeandaliwa na Shabani Matutu, Grace Shitundu, Esther Mnyika (DAR), Peter Fabiani (MWANZA), Mohamed Hamad (KITETO) na Upendo Mosha (MOSHI).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles