HANSPOPPE AKATAA KUMKAIMU AVEVA

0
427

NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili Simba, Zakaria Hanspope, amesema kwa sasa hayupo tayari kukaimu nafasi ya raisi wa klabu hiyo, Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi.

Aveva na Makamu wake Kaburu, Juni 28, mwaka huu walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka matano ikiwamo kutakatisha fedha, huku wakiwekwa ndani hadi Julai 13, mwaka huu kutokana na makosa hayo kutokuwa na dhamana.

Kutokana na tuhuma hizo kuwabili viongozi wa juu wa klabu hiyo waliokuwa wakisimamia shughuli mbalimbali za klabu, baadhi ya mashabiki wametaka jina la  Hanspope kukaimu moja ya nafasi hizo kutokana na kukaa muda mrefu  kwa mujibu wa  Katiba ya Simba.

Hanspope ameibuka na kutoa kauli hiyo saa chache baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba kukutana kwa ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali, ikiwemo uendeshaji wa klabu hasa katika kipindi hiki wanachokabiliwa na maandalizi ya msimu ujao.

Inaelezwa kuwa idadi kubwa ya mashabiki wanaunga mkono kati ya Hanspope au msaidizi katika Kamati ya Usajili, Kassim Dewji, mmoja kuchukua mikoba ya kuiongoza klabu hiyo hadi pale mambo yatakapokaa vizuri.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Hanspope aliwataka wanachama wa klabu hiyo kutafuta mtu mwingine sahihi atakayeweza kuingoza Simba kwa kipindi hiki ambacho viongozi wao wamepatwa na matatizo.

“Siko tayari kukaimu moja ya nafasi za juu za kuiongoza Simba kutokana na kukabiliwa na shughuli nyingi binafsi ambazo zinanifanya kusafiri mara kwa mara, hivyo muda mwingi sitakuwa karibu na timu.

“Wanachama wanatakiwa kuchagua mtu sahihi ambaye ataiongoza Simba kwenye kipindi hiki kigumu cha mpito, hasa ukizingatia sasa hivi tupo katika mchakato wa kujenga kikosi imara kwa ajili ya msimu ujao pamoja na michuano ya kimataifa,” alisema Hanspope.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here