KOREA KASKAZINI YAZIGOMBANISHA CHINA, MAREKANI

0
457

EIJING, CHINA

SERIKALI ya China imeghadhabishwa sana na hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo benki moja ya China ambayo inatuhumuwa kuhusika katika utakatishaji wa fedha za Korea Kaskazini.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Taifa hilo, ameitaka Marekani ‘kukoma kuchukua hatua zisizo sahihi’ kuepusha kudhuru ushirikiano baina ya nchi hizo.

Marekani ilitangaza hatua hiyo pamoja na vikwazo dhidi ya kampuni ya uchukuzi wa meli ya China na raia wawili wa China mnamo Alhamisi.

Ilisema lengo la vikwazo hivyo ni kupunguza fedha ambazo Korea Kaskazini inaweza kutumia kuendeleza mpango wake wa kustawisha silaha.

“Tutafuatilia pesa hizo na kufunga mirija,” Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin alikiambia kikao cha wanahabari.

Hata hivyo, alisema hatua hiyo haijatokana na China kutoichukulia hatua Korea Kaskazini na kusema: “Hii hailengi China, hii inaangazia benki pamoja na watu binafsi na mashirika yaliyopo China.”

Umoja wa Mataifa ulikuwa tayari umeiwekea Korea Kaskazini msururu wa vikwazo, lakini China inatazamwa na wengi kama taifa lililo na uwezo zaidi wa kuiyumbisha Korea Kaskazini kupitia vikwazo vya kiuchumi.

Serikali ya Washington imekuwa ikiishinikiza Beijing kuchukua hatua kali zaidi hasa kutokana na hatua ya Pyongyang ya kufanyia majaribio makombora ya masafa marefu.

Lakini kupitia mtandao wa Twitter mwishoni mwa Juni, Rais Donald Trump alisema hatua ambazo China imechukua kufikia sasa hazijatosha.

Vikwazo hivyo vilitangazwa huku Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in akizuru Washington kwa mashauriano na Trump kuhusu masuala ya usalama.

Vikwazo hivyo vina maana kwamba Benki ya Bandong sasa imepigwa marufuku kufanya biashara Marekani.

Wizara ya Fedha ya Marekani imesema benki hiyo imetumiwa kusafirisha na kutakatisha fedha za Korea Kaskazini na kwamba mamilioni ya dola zilizolipwa kampuni zilizohusika katika mpango wa silaha za Korea Kusini zilipitishiwa katika benki hiyo.

Raia wawili wa China ambao wanatuhumiwa kuunda kampuni ambazo zimekuwa zikitumiwa na mashirika ya Korea Kaskazini na kampuni moja ya uchukuzi wa meli ya Dalian Global Unity Shipping, zimedaiwa kuingiza kinyemela bidhaa hadi Korea Kaskazini na zimewekewa vikwazo.

Waziri Mnuchin amesema kwamba Marekani inaweza kuongeza vikwazo zaidi hivi karibuni.

Vikwazo hivyo vimetangazwa muda mfupi baada ya Marekani kutangaza mauzo ya silaha za thamani ya dola bilioni 1.42 kwa Taiwan, shughuli kama hiyo ya kwanza kabisa ya kibiashara chini ya utawala wa Trump.

Mauzo ya silaha kwa Taiwan kila mara yamekuwa yakiwakera Beijing kwani China huchukulia kisiwa hicho kinachojitawala kuwa sehemu ya himaya yake.

Kupitia taarifa hiyo, ubalozi wa China mjini Washington uliitaka Marekani kubatilisha hatua hiyo na kusema kuwa China ina kila haki ya kukasirika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema jana kwamba hatua ya Marekani ilienda kinyume na ‘moyo muhimu’ wa urafiki kati ya Trump na Rais wa China Xi Jinping waliouonesha walipokutana katika Jimbo la Florida, Marekani, Aprili mwaka huu.

Mapema wiki hii, Marekani pia iliiorodhesha China miongoni mwa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu duniani na kufanyiwa kazi kwa watu kwa lazima, hatua ya kwanza kabisa kuu ya utawala wa Trump dhidi ya China na haki za kibinadamu.

Trump akiri kuishiwa uvumilivu

Inaonekana kama rais wa Marekani ameguswa na tamko la Serikali ya China, hivyo amemua kusafisha anga na kusisitiza kuchoshwa na suala la Korea kaskazini.

Rais wa Marekani Donald Trump anasema muda wa uvumilivu wa kimikakati kwa Korea Kaskazini umekwisha sasa.

Trump amesema hayo jana katika hotuba ya pamoja na rais wa Korea Kusini, Moon Jae, kwenye Ikulu ya White house, na kusisitiza kuwa vitisho vya Korea Kaskazini vinafaa kupata majibu ya kijasiri.

Hata hivyo, Trump amesema ni muhimu kuwe na ushirikiano katika kugawana mzigo wa kuhakikisha usalama.

Naye Rais wa Korea Kusini amesema kwamba, Taifa lake litaweka marekebisho ya kiuslama na kujenga msingi dhabiti wa kujikinga. Rais Moon pia amesema ni muhimu kuendelea na majadiliano na viongozi wa Korea Kaskazini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here