HAMA HAMA YA WANASIASA: INALETA PICHA GANI KWA WANANCHI?

0
1276

Na BARNABAS MARO


TANGU Tanganyika na baadaye Tanzania kuwa huru mwaka 1961, haijatokea wingi wa viongozi wa upinzani kuvikimbia vyama vyao na kujiunga na chama tawala (CCM) kama ilivyo sasa!

Ni ajabu, lakini ndivyo ilivyo. Kuna maswali mengi yanayohitaji majibu sahihi kuhusu hali hii inayowashangaza wapinzani, lakini ikiwafurahisha na kuwanufaisha viongozi, wanachama na mashabiki wa CCM kwa upande mwingine.

Wahenga waliuliza: “Humpendaje mtu kwa kuambiwa penda?” Maana yake itawezekana vipi kumpenda mtu kwa kuwa umeambiwa umpende?

Methali hii yatukumbusha kwamba hatuwezi kuzilazimisha hisia za binadamu. Mathalani, kama mtu hakitaki au hakipendi kitu fulani ni vigumu kumfanya akipende. Kupenda hutokana na hisia za mtu mwenyewe.

“Fedha ilivunja nguu, milima ikalala.” Nguu ni mlima mkubwa mrefu. Maana yake pesa zina uwezo wa kuivunja milima na vilima. Methali hii hutumiwa kupigia mfano uwezo wa fedha. Mtu akiwa na pesa anaweza kufanikiwa kufanya mambo ambayo asingeweza kuyafanya wala kudhania kuyafanya.

Pamoja na nguvu ya fedha, twaonywa kuwa “fedha fedheha” kwani pesa huweza kuleta mambo ya aibu baina ya wanadamu. Hutumiwa kutuonya kuhusu maovu yanayoweza kusababishwa na pesa.

Yanasemwa mengi kuwa msururu wa madiwani na wabunge wa upinzani wanaokimbilia CCM hufanya hivyo kwa ‘kuahidiwa vyeo, kupewa fedha au vyote pamoja.’

Ni vigumu kuthibitisha hili lakini kuna picha zilizochukuliwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, zikimwonesha kiongozi mmoja wa serikali ya wilaya akimkabidhi fedha diwani wa Chadema ili ajiunge na CCM.

Husemwa “fuata nyuki ule asali.” Ukitaka kula asali huna budi kuwafuata nyuki. Ni methali ya kutumiwa kumshauri mtu aandamane na watu wanaoweza kumfaidi au wenye manufaa.

Nassari alipeleka ushahidi wa picha kwenye Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru). Siku chache baadaye, wakati wananchi wakisubiri matokeo, ikatolewa taarifa kuwa jambo hilo limekuwa la kisiasa mno hivyo lisingeshughulikiwa! Kesi ya nyani kumpelekea tumbili unategemea nini?

Swali: Kama malalamiko yale yenye ushahidi wa picha zilizochukuliwa kwa siri yangetolewa na mbunge wa CCM yangepuuzwa kama ilivyokuwa kwa mbunge Nassari na Chadema yake?

“Lililopo ndilo lisemwalo.” Maana yake jambo linalosemwa au linaloongelewa juu yake ni lililopo. Lisilokuwepo halisemwi.

Methali hii hutumiwa na mtu anayelikana jambo fulani. Mathalani, mtu aliyefanya jambo fulani kisha akawa hataki kukubali ingawa watu wengine wanaufahamu ukweli wake.

Hebu fikiri: Diwani, mbunge au kiongozi wa upinzani anaisuta (kitendo cha kumkadhibisha mtu kwa maneno hadharani) Serikali kwa hoja lakini huyo huyo aliyekuwa akisema mpaka mapovu kumtoka kinywani ndiye anayetangaza kujiunga na CCM kesho yake!

Amepewa kitu gani, kalishwa au kaahidiwa nini? Baadhi yao huwa na madeni mengi na kwa sababu hiyo huahidiwa kulipiwa madeni wanayodaiwa na kupewa kazi. Hali kama hii yaitwaje?

‘Rushwa’ ni kitu mtu anachopokea kutoka kwa mwingine au anachotoa kumpa mwingine ili afanyiwe jambo kwa upendeleo. Ina majina mengine kama mlungula/mrungura (wasemavyo Wazanzibari), kilemba, hongo na chauchau.

‘Kosoa’ ni kitendo cha kumrekebisha mwingine. Je, Serikali  ya CCM haitaki kurekebishwa kwa sababu ‘haikosei’ kwamba kila iwafanyiacho wananchi ni ‘sahihi?’

Hapana. Asiyekosa ni malaika. Binadamu wote hukosa; malaika na Mungu ndio wasiokosa. Hii ni methali ya kutumiwa kuwashauri watu wakubali makosa yao au hata kuwapoza wanapokosa. Binadamu lazima afanye kosa na afanyapo kosa anapaswa kukiri (kuungama).

Nionavyo, huenda baadhi ya madiwani na wabunge wa upinzani wanaojiunga na CCM hubanwa sana na Serikali kiasi cha majimbo yao kutofanyiwa lolote kwa huduma za barabara, maji, umeme na mipango mingine ya maendeleo.

Katika hali hiyo wanaona ni bora wajiunge na CCM ili kama ‘wakichaguliwa’ tena ndipo Serikali itayashughulikia majimbo yao nao wataonekana na wapiga kura wao kuwa wanafanya kazi walizotumwa na wananchi wa maeneo yao.

Viongozi wa CCM na hata wa Serikali wamekuwa wakisema kwenye mikutano kuwa wananchi wajiunge na chama hicho ili wapate maendeleo kwani wapinzani hawawezi kufanya hivyo!

Je, ndivyo ilivyo kwa viongozi wa upinzani wanaohamia CCM kwa mtiririko? Wanakubaliana na methali isemayo “Mtumikie kafiri upate mradi wako?” Methali hii huweza kutumiwa kupigia mfano mtu mwenye sifa au wasifu mbaya, lakini anayewafaidi watu kwa namna moja au nyingine.

Ushindani wa kisiasa usigeuzwe kuwa uadui. Sote ni watu wa nchi moja iitwayo Tanzania. Kwanini twabaguana na kunyang’anyana fito ilhali twajenga jengo moja? Nchi zenye demokrasia halisi hakuna chama cha siasa kitakachotawala maisha.

Mara nyingi uroho wa madaraka hufanywa na baadhi ya viongozi wa Afrika wasiopenda kuachia madaraka wanapopata nafasi ya kutawala. Wanaponogewa huwatumia wapambe wao kuingiza hoja ya kubadili Katiba za nchi zao ili waendelee!

Ndio maana utaona Serikali nyingine huwa na vyama vinavyoitwa vya ‘upinzani’ kumbe ni vibaraka wa Serikali zilizo madarakani! Ndio maana husemwa penye msafara wa mamba na kenge pia wamo.

Kwa upande mwingine, watu na viongozi wa dini wanaojitokeza kuikosoa Serikali ya Tanzania huchokolewa kwa kuambiwa si Watanzania wakati wanazo pasi za Tanzania na baadhi kuitumikia Serikali katika nyanja mbalimbali na baadhi wakiwa viongozi wakuu wa madhehebu mbalimbali ya dini!

Kabla ya uhuru, kuna watu waliokujaTanganyika kufanya kazi kwenye mashamba ya mkonge. Watu hao walioitwa ‘manamba,’ wengi wao walitoka Rwanda na Burundi wakazaliana humu nchini na watoto wao wakasomea humu humu nchini na kupewa nafasi mbalimbali serikalini.

Leo kuhoji uraia wao maana yake nini? Tuchukulie ilivyokuwa kwa Askofu Severin Niwemugize wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Ngara. Huyu alisomea humu nchini, akaenda Seminari akapewa daraja la upadre baada ya kuhitimu kisha akawa Askofu.

Kote huko alikopita, hakuulizwa uraia wake. Kama haitoshi, akapewa hata pasi ya kusafiria. Hata hivyo, alipoikosoa Serikali, akaitwa na Idara ya Uhamiaji, eti akathibitishe uraia wake! Alipewaje pasi kama si raia wa Tanzania?

Tanzania ina watu wenye chimbuko la nchi mbalimbali kama Rwanda na Burundi walioenea sana mikoa ya Kigoma, Kagera, Tanga na Moshi. Pia kuna Wakurya, Waluo, Wamasai na baadhi ya Wachaga ambao pia walitokea Kenya. Aidha, Wangoni ambao chanzo chao ni Afrika Kusini na kusambaa mpaka Zambia, Malawi, Msumbiji na Tanzania.

Tunao Wasomali, Wahabeshi na wengine kutoka Sudan. Warangi, Wabarbeig, Wasandawi n.k. asili yao ni wapi? Sisemi Idara ya Uhamiaji isifanye wajibu wake, la hasha. Watu hao walipataje uraia wa Tanzania na kupewa pasi za kusafiria? Sina nia mbaya bali nauliza tu kwani aulizaye ataka kujua.

Magomvi: “Acha ugomvi, nawe utazipunguza dhambi zako; maana mwenye ghadhabu huchochea ugomvi, na mchongezi huhangaisha rafiki, hata kupenyeza hitilafu kati yao wakaao kwa amani.” (Yoshua Bin Sira 28: 8-9)

“Ugomvi ulioanzishwa na haraka huwasha moto na mapigano ya ghafla humwaga damu. Vuvia cheche, itawaka; tema juu yake, itazimika; na yote mawili yatoka kinywani mwako.” (Yoshua Bin Sira 28:11-12).

marobarnabas@yahoo.com  0784/0715  334 096

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here