27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Halmashauri nchini zatakiwa kuhakikisha wataalam wa TEHAMA wanahudhuria mafunzo

Na Mwandishi Maalumu

Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kuhakikisha wataalam wa TEHAMA wanahudhuria mafunzo ya ukarabati wa vifaa vya sekta hiyo ili kuokoa fedha nyingi za Serikali ambazo zinapotea kwa kukosekana kwa utaalam wa kukarabati.

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Profesa Preksedis Marco Ndomba (aliyekaa wakwanza kulia) na Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka TAMISEMI, Erick Kitali na Mkuu wa Kituo cha Kikanda cha Umahiri wa Tehama (ITCoEICT), Kennedy Aliila wakiwa kwenye picha ya pamoja na wahitimu na wakufunzi wao wa mafunzo ya ukarabati wa mashine za printer na photocopier kutoka TAMISEMI.

Maagizo hayo yametolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mita (TAMISEMI), Erick Kitali alipomuwakilisha Katibu Mkuu wa TAMISEMI katika kufunga mafunzo ya ukarabati wa ‘Printer ‘ na ‘Photocopier ‘ kwa watumishi saba wa TAMISEMI yaliyofanywa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi Kuu ya Dar es Salaam. 

“Natoa wito na kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wataalam wa TEHAMA wanahudhuria mafunzo ya aina hii ili kuokoa fedha nyingi za Serikali ambazo zinapotea kwa kukosekana kwa utaalam wa kukarabati vifaa vya TEHAMA katika Halamashauri zetu kote nchini,”  amesema.

Kitali amesema umahiri wa DIT katika utoaji mafunzo si jambo la kutiliwa shaka na kwamba mafunzo hayo muhimu katika utunzaji wa vitendea kazi katika halmashauri nchini nzima.

Aidha, amesema mafunzo hayo si tu kwamba utaimarisha utoaji wa huduma bali pia utaongeza ufanisi katika uhudumiaji wa mifumo ya kidigitali na kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika katika ununuzi wa vitendea kazi vipya badala ya kufanya ukarabati mdogo na kifaa kurejea katika hali ya utendaji wake wa awali. 

Kitali amebainisha kuwa katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya kila siku TAMISEMI inategemea mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za Elimu na Afya. Huduma hizo mara nyingi  huhitaji kuchapishwa ama kutolewa nakala kwa mantiki hiyo vifaa hivyo vinakuwa ni vitendea kazi muhimu.

“Kwa muda mrefu sasa, halmashauri zetu za Wilaya, Miji, Manispaa, Majiji na Sekretarieti za Mikoa zimekua zikikumbwa na changamoto ya kuharibika kwa vifaa hivi hali inayosabasha kusuasua kwa utoaji huduma na kupunguza kasi ya kutoa huduma kwa Wananchi wetu,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam,  Prof Preksedis Ndomba amesema mafunzo hayo yamefanyika kwa vitendo zaidi, “kwa ushahidi wa wahitimu hawa watashuhudia namna  dhana ya ‘Teaching Factory’ inavyotimizwa katika mafunzo yetu yote, wakati wa mafunzo hayo, mashine za kutoa nakala tatu na mashine za kuchapa tatu, zilizokuwa na ubovu wa muda mrefu zimefufuliwa.”

Aidha, amesema lengo la utoaji mafunzo lilikuwa ni kuzalisha wataalam waliobobea katika ukarabati wa mashine hizo na kufikisha mafunzo hayo nchi nzima kupunguza gharama za matengenezo na ununuaji wa vifaa vipya mara kwa mara.

Naye mnufaika wa mafunzo hayo, Innocent  Sigred kutoka Kibaha Mji ameishukuru DIT kwa kufundisha kwa juhudi kwa vitendo zaidi.

Mafunzo haya yaliyohitimishwa leo yalianza rasmi tarehe 02 Agosti, 2021, yanatarajiwa kuendelea kutoa katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mtwara, Mbeya, na Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles