HALMASHAURI D’SALAAM YATOZWA FAINI YA MIL 14/-

0
810

Na ASHA BANI

SERIKALI imeitoza faini Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kiasi cha Sh milioni 25, kwa kosa la utiririshaji wa maji taka katika Dampo la Pugu Kinyamwezi kwenda katika makazi ya wananchi wanaoishi jirani.

Akitoa agizo hilo Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina, alisema fedha hizo zinatakiwa kulipwa ndani ya siku 14 na kuhakikisha inajenga miundombinu ya kuzuia maji machafu kutoenda kwa wananchi.

Alisema agizo hilo linatokana na malalamiko ya wakazi wa Mtaa wa Viwege, uliopo Kata ya Majohe, yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Amina Rashid, ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo za vumbi, maji yenye kemikali kutiririkia kwenye makazi ya watu.

Pia aliitaka kuweka mpango mkakati utakaoweza kulipunguzia mzigo dampo hilo ambalo kwa sasa linatumika kupokea takataka zote za Dar es Salaam na kuonekana kuelemewa na mpango huo.

Alisema kila manispaa inatakiwa kuwa na  dampo lake litakalosaidia kupunguza mrundikano huo.

Pia alibaini kuwapo kwa udhaifu katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kuondosha taka katika manispaa za jiji.

Aliitaka kutafuta namna bora ya kuondosha taka sumu na kuelekeza taka zote za matairi katika jiji zitafutiwe sehemu tofauti na namna ya kuziteketeza.

“Hakuna kitu nisichopenda katika utendaji wangu kama kuona taasisi za Serikali zikiwa za kwanza katika suala zima la uchafuzi wa mazingira, faini hiyo jiji mtailipa ndani ya siku 14, na kuhakikisha mnarekebisha matobo yote yanayolalamikiwa kupitisha maji na kupeleka katika makazi ya wananchi.

“Pia kujenga mifereji ya maji ya mvua, maji ya sumu yaende katika mkondo sahihi wa maji hatarishi na bila kusahau kuruhusu maji hayo baada ya kujiridhisha na vipimo vinavyotakiwa kuwa hayana sumu,’’ alisema.

Awali, Mkuu wa Idara ya Usimamizi Taka wa Jiji la Dar es Salaam, Shedrack Maximillian, alisema jiji linakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kutokea kwa moto, kutokuwa la kisasa na maji yenye sumu kwenda katika makazi ya watu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here