SERIKALI YASHUSHA BEI DAWA ZA KUTIBU BINADAMU

0
883

Na ASHA BANI

SERIKALI imetangaza kushusha bei ya dawa na vifaa tiba hapa nchini, baada ya kuanza kufanya ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi bila kutumia mawakala.

Punguzo hilo limehusisha mikataba na wazalishaji 73, kati yao 10 ni wazalishaji wa ndani na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inaagiza dawa, vifaa vya maabara na vitendanishi kutoka nchi 20 tu.

Akitangaza mabadiliko hayo Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema kushuka kwa dawa hizo ni agizo la Rais Dk. John Magufuli.

“Hatua ya kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kama tulivyoeleza hapo awali imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za kununua dawa kwa asilimia 15 hadi 80.

“Mabadiliko haya ya bei, yaani unafuu huo wa bei kiuhalisia umeanza kuonekana tangu Julai Mosi, mwaka huu ambapo wazalishaji wanaleta dawa MSD. Kupungua kwa bei kutaviwezesha vituo vya afya na hospitali kununua dawa zaidi kwa bei nafuu,” alisema Ummy.

Alizitaja baadhi ya nchi walizotoa vibali kwa wazalishaji 46 ni Uganda, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, China, Afrika Kusini, Falme za Kirabu, Bangladeshi, India, Tanzania na Kenya.

Alisema aina 178 za dawa zinatoka kwa wazalishaji hao, huku vifaa tiba, jumla ya wazalishaji 18 wamepata mikataba kutoka katika nchi ya Uingereza, Ujerumani, India, Kenya na Tanzania.

Alizitaja baadhi ya dawa hizo kuwa ni chanjo ya homa ya ini iliyouzwa kwa Sh 22,000 kwa sasa itauzwa Sh 5,300, dawa ya sindano ya diclofenac kwa ajili ya maumivu vichupa 10 vya dozi, awali ilikuwa ni Sh 2,000, sasa itauzwa kwa Sh 800.

Pia alisema shuka moja iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh 22,000, sasa itauzwa kwa Sh 11,000, mipira ya kuvaa mikononi inayokaa 50 kwa boksi itakuwa ikiuzwa Sh 18,200 kutoka Sh 19,200 na dawa ya kupambana na maambukizi ya bakteria yenye vidonge 15 itauzwa Sh 4,000 kutoka Sh 9,800.

Pia amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri, waganga wakuu wa wilaya na mikoa kuhakikisha bei ya dawa zinashushwa kama watakavyoelekezwa na MSD.

Alizitaka halmashauri, vituo, hospitali kutumia bei elekezi ya dawa iliyotolewa na wizara hiyo iliyopo katika kitabu cha MSD.

Alisema watakuwa wanabandika mabango kama wanavyofanya Ewura na ikitokea muuzaji hajatekeleza hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu, alisema watajitahidi kuhakikisha dawa zinapatikana kwa asilimia 100, huku akimwomba Ummy kuhakikisha halmashauri na hospitali zinawasilisha mahitaji yao kwa wakati.

“Tunaomba ushirikiano wa wadau wote, tumejipanga kuhakikisha tunavuka malengo kusambaza dawa kutoka asilimia 81 ya sasa hadi 100,” alisema.

Pia alisema MSD itahakikisha dawa zinapatikana kwa wakati, hivyo ni muhimu wananchi kutoa ushirikiano.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here