‘WATANZANIA WANA HOFU YA KUPOTEZA MAKAZI YAO’

0
596

VERONICA ROMWALD NA JOHANES RESPICIUS – DAR ES SALAAM

ASILIMIA 80 ya Watanzania wanaishi kwa hofu ya kupoteza maeneo na kubomolewa makazi yao kutokana na kujenga holela bila kuzingatia ramani za mipango miji.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mtaalamu wa Mipango Miji wa Kampuni ya Upimaji Ardhi ya Hosea, Renny Chiwa, wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Upimaji Ardhi katika Kata ya Saranga.

“Asilimia 80 ya makazi yetu katika ardhi ya jumla hayajapangwa, ni holela na hali hiyo inawakosesha wananchi fursa nyingi hasa za kumilikishwa maeneo yao.

“Ndiyo maana wananchi waliopo katika maeneo mengi wanaishi kwa hofu kwa sababu wakiona tu miradi mikubwa inaanzishwa katika maeneo yao kwa mfano barabara, wanaogopa kwamba wanatavunjiwa nyumba zao,” alisema.

Pia alisema kampuni hiyo imekusudia kuondoa hofu hiyo kwa kupima ardhi ili wananchi waweze kumilikishwa rasmi.

“Kupitia mpango huu tumekusudia kuwafikia takriban wakazi 32,000 tutakuwa tumewaokoa na tunatumia teknolojia ya kisasa kwa kutumia ndege zisizo na rubani na tunapata picha ya anga hali halisi ya watu na uendelezaji wa mji,” alisema.

Naye, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa John Lupala, alisema katika mwaka huu wa fedha wizara imekusudia kumilikisha wananchi hati 400,000.

“Kazi ya urasimishaji ardhi wizara tunaisimamia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama Hosea, tunaamini tutafikia lengo tulilo nalo la kurasimisha ardhi kwa wananchi,” alisema.

Kwa upande wake, Diwani wa Msigani, Israel Mushi, alisema kuanza kwa upimaji huo kutasaidia kupunguza migogoro ya ardhi katika eneo hilo.

“Lakini pia itasaidia Serikali kupata mapato yake inayostahili tofauti na ilivyo sasa ambapo maeneo mengi hayajapimwa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here