Na Mwandishi wetu
-Dodoma
SERIKALI imezipatia halmashauri 12 nchini ruzuku ya Sh bilioni 137 kwa ajili ya kutekeleza miradi 15 ya mkakati kuongeza mapato ya ndani.
Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Doto James na wakurugenzi wa halmashauri hizo, walitia saini mkataba wa makubaliano hayo Dodoma jana.
James alizitaka halmashauri zilizopata fedha hizo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa .
Alionya hatua kali za sheria zitachukuliwa kwa watendaji watakaokiuka makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wa makubaliano.
“Maofisa masuuli mhakikishe mnafuata na kuzingatia Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 na kanuni zake, ambayo pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya matumizi bora ya fedha kwa shughuli zilizoidhinishwa” alisema James.
Alisema Serikali ilipoanzisha utaratibu huo haikuwa inatania wala kufanya mazingaombwe, inayo dhamira ya dhati ya kuzijengea uwezo halmashauri zijitegemee kwa uchumi na kutoa huduma bora kwa wananchi badala ya kutegemea ruzuku ya Serikali Kuu.
Aliwahakikishia wadau kuwa fedha hizo zipo na kuzitaka halmashauri zichangamkie fursa hiyo kwa ukamilifu.
Miradi inayotarajiwa kutekelezwa inahusisha masoko ya kisasa, kiwanda cha kusindika korosho, uendelezaji wa fukwe ya Oysterbay na maegesho ya malori, iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Kigamboni, Tanga, Kibaha, Bagamoyo, Mwanza, Tarime, Hanang, Iringa na Biharamulo.
Kamishna wa Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga alisema awamu ya pili ya miradi ya mkakati kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa miradi iliyokidhi vigezo ni 15 yenye thamani ya Sh bilioni 137.38.
Naibu Katibu Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi, Dk. Doroth Gwajima, aliipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha ambazo zitachochea miradi ya maendeleo katika halmashauri nchini.
Dk. Gwajima, alizitaka halmashauri zilizofanikiwa kusaini mikataba hiyo kuhakikisha zinazingatia lengo la mkataba huo na kutekeleza miradi kwa muda mwafaka na viwango vilivyoainishwaa na kwamba ufuatiliaji wa miradi hiyo utakuwa ni wa kiwango cha juu.