31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kitukuu cha familia ya kwanza ya India kinajitayarisha

NA OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI

BABA yake  Rajiv Gandhi alikuwa  Waziri Mkuu wa India, Bibi yake Indira Gandhi alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa kike katika nchi hiyo na baba wa bibi yake  Jawaharlal Nehru alikuwa Mkuu wa Serikali punde baada ya nchi hiyo kuwa huru kutoka ukoloni wa Mwingereza.

Wawili wa mwanzo kati ya hao watu niliowataja juu, kwa masikitiko, waliuliwa wakiwa madarakani.  Katika makala hii ninamzungumzia Priyanka Gandhi (Bibi Vadra), binti wa Rajiv Gandhi  na ambaye sasa anaingia katika ulingo wa siasa za India.

Yaonesha Priyanka anaingia katika siasa akiwa ni karata ya mwisho ya ukoo wa kisiasa wa Gandhi ambao kwa miongo ya miaka uliamua juu ya mustakabali wa siasa za chama cha Congress. Chama hicho si tu kimeamua kwa muda mrefu juu ya mwelekeo wa India, lakini pia ni chama kikongwe kabisa katika taifa hilo lililoko barani Asia.

Wiki iliyopita Priyanka Gandhi, mwenye watoto wawili, alitimia umri wa miaka 47 na akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha Congress katika Mkoa wa Uttar Pradesh, UP kama mkoa huo unavyoitwa huko india. Ni mkoa wenye wakaazi wengi kabisa katika nchi hiyo, ukipeleka wabunge 80 kati ya 545 wa India nzima.

Mashariki ya Uttar Pradesh, katika Mji mtakatifu wa Mabaniani- Varanasi- ndiko ambako Waziri Mkuu wa India mwenye siasa kali za uzalendo wa Kihindu, Narendra Modi, ana kiti chake cha Bunge.  Hadi ifikapo Mei mwaka  huu inabidi ufanyike uchaguzi wa Bunge la Taifa.

Priyanka, jina lililoko vinywani mwa watu wengi hivi sasa, anatarajiwa kuwashinda kabisa wazalendo wa Kibaniani ambao hivi sasa wana usemi katika mkoa huo. Wazalendo hao walishindwa katika uchaguzi uliopita wa mkoa. Lakini katika mkoa huo kuna pia vyama viwili vya itikadi kali za Kibaniani vinavyoshirikiana na ambavyo vina nguvu, kwa hivyo vitamtoa jasho Priyanka.

Priyanka ni mdogo wa Rahul Gandhi, kiongozi wa sasa wa Congress na anaonekana anavutia zaidi kwa wananchi. Rahul hana bashasha sana na hadharani anaonekana kuwa mwenye haya na anakosa ujasiri. Priyanka alisomea Saikolojia na dini ya Kibuddha na kwa muda mrefu alikataa kukamata wadhifa wowote wa kisiasa. Aliwasaidia mama yake, Sonia na kaka yake Rahul, katika chaguzi zilizofanikiwa kwenye majimbo yao ya uchaguzi ambayo pia yako katika Mkoa wa Uttar Pradesh.

Uttar Pradesh ni mkoa muhimu, mlango wa kufikia madarakani katika siasa za India. Priyanka anaingia siasa wakati chama cha Congress kinajitahidi kurejea tena kutajika baada ya kupita miaka migumu ya kusukumwa pembeni kutokana na umaarufu wa Waziri Mkuu Modi. Chama cha Congress ni cha ukoo na watu walio katika familia huheshimiwa kama miungu. Sasa kuna familia iliyojitokeza hadharani kwa mara ya kwanza. Hili ni jaribio ambalo litakipa nguvu chama hicho. Mwenyewe Priyanka anasema ameivaa siasa na kuisoma siasa katika meza ya kulia chakula nyumbani kwao.

Akiwa ana umri wa miaka 26, Priyanka alilitembelea gereza lililoko mbali Kusini mwa India kukutana na mwanamke aliyepatikana na hatia ya kumuuwa baba yake, Marehemu Waziri Mkuu, Rajiv Gandhi. Rajiv Gandhi aliuliwa wakati akifanya kampeni ya uchaguzi mwaka 1991 na mtu aliyejiua mwenyewe baadaye. Binti yake wakati huo alikuwa na umri wa miaka 19. Vyombo vya habari vya India viliigundua safari hiyo ya siri aliyoifanya Priyanka katika jela. Lakini yeye mwenyewe baadaye aliwaomba watu waheshimu maisha yake ya faragha. Sasa ameamua kuikoga siasa, na kwa hivyo asitarajie maisha yake ya binafsi yatabakia kuwa siri.

Maisha yalivurugika mwaka 1984 pale Indira Gandhi alipouliwa na mpambe wake wa Dini ya Kisingasinga. Rajiv, ambaye hapo kabla alifanya kazi ya urubani katika Shirika la Ndege la India, alilazimika kuchukua wadhifa wa Waziri Mkuu wa nchi. Pale alipouliwa miaka saba  baadaye, mjana wake aliyekumbwa na huzuni, mzaliwa wa Italiana, pamoja na watoto wake waliamua kuendesha maisha ya upweke. Lakini mwaka 1990 alivutiwa na siasa pale mama yake, Sonia, alipowakubalia wanasiasa wa Congress waliomtaka awanie ubunge na kukiongoza chama hicho kilichokuwa kinapoteza umaarufu.

Akiwa msomaji sana wa fasihi ya Lugha ya Kihindi, Priyanka alijitolea kuandika hotuba za mama yake na pia kuendesha kampeni za uchaguzi kwa niaba ya mama yake katika Jimbo la Amrithi.

Kama mdogo kabisa katika ukoo wa Gandhi-Nehru, Priyanka sasa anatarajiwa kupeperusha bendera ya  Chama cha Congress ambacho sasa kiko upande wa Upinzani katika Bunge la Taifa. Washabiki wa Priyanka wanashikilia kwamba amefanana na bibi yake, Indira Gandhi. „Indira anarejea“, ndivyo yalivyoandikwa mabiramu mabarabarani. Katika enzi zake, Indira Gandhi alikuwa mtawala wa mabavu na mtu aliyebishwa sana.

Rahul, kama mkuu wa Congress, amemsifu Priyanka kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongoza. Msemaji wa Wazalendo wa Kihindu alitangaza kwamba kwa Chama cha Congress kumtaja Priyanka kama mwenyekiti  wa mkoa inadhihirisha kwamba Rahul ameshindwa. „Sasa anahitaji magongo kutoka kwa familia yake mwenyewe ili yamsaidie atembee.“

Kwa Congress familia ndio chama, lakini kwa Wazalendo wa Kibaniani chama ndio familia. Wapinzani wa Congress wanaashiria juu ya mume wa Priyanka, mfanya biashara Robert Vadra, ambaye analaumiwa kufanya biashara ya uuzaji wa viwanja kwa njia ya magendo. Kwa vile Chama cha Congress hadi sasa kinadhibitiwa na familia ya Gandhi, kukamatwa karibu nyadhifa zote za juu za chama hicho na familia hiyo hakutamsaidia Priyanka kupanda juu na kuurefusha uongozi wa familia hiyo kwa kizazi kingine.

Lakini pale anapowavutia watu wengi zaidi kila anapochomoza hadharani na tetesi zikizidi kwamba atafuata nyao za bibi yake ambaye anafanana naye sana, Priyanka alikwenda kufanya ibada ya faragha iliyodumu siku kumi. Hapo aliamua kutoingia katika dimbwi la siasa. Priyanka alitumia miongo miwili akilea watoto wake mjini New Delhi. Pia amekuwa msiri na mshauri rasmi wa mama yake-Sonia Gandhi-aliyekiongoza Chama cha Congress hadi mwaka jana- pamoja na Rahul.

Katika miezi ya karibuni, Priyanka amezidi kuijongelea siasa, na hasa pale watu wanapozidi kushuku juu ya uwezo wa kaka yake mkubwa katika kukabiliana na vishindo vikubwa vya siasa. Lake yeye amebaki kuwa mtiifu sana kwa kaka yake ambaye watu wanamshambulia kwa kukosa umahiri wa siasa. Inasemakana kwamba Priyanka „hajaonekana kutaka kumgubika kaka yake.“

Uamuzi wake wa kujichovya ndani ya siasa umekuja baada ya kupita wiki baada ya Rahul kukiongoza chama katika mafanikio matatu yasiotarajiwa katika chaguzi za mkoa kwenye maeneo matatu yaliokuwa yakishikiliwa na Chama cha Bharati Janata cha  waziri mkuu Modi. Katika chaguzi hizo udhaifu wa Modi ulionekana. „Kuna Chama cha Congress ambacho kinajaribu kujipanga upya“ alisema Nalanjan Sirca, profesa wa taaluma ya siasa katika Chuo Kikuu cha Ashoka. „Wamefikiri kwamba katika wakati muhimu tunamhitaji mtu kama Priyanka Gandhi kuzuwia kile kinachonekana kuwa aina ya kudhoofika daima kwa chama.“

Mwongo mmoja uliopita Priyanka alimwambia mwandishi wa habari: „Itakuwa vigumu kwangu mimi kushawishika kwamba Chama cha Congress kinanihitaji.“  Yaonesha wakati huo umewadia sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles