26.2 C
Dar es Salaam
Friday, December 3, 2021

CHARLES BLE GOUDE: Jabari lililokuwa likimpa kiburi Laurent Gbagbo

KATIKATI ya mwezi uliopita, majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) walimuachia huru Rais wa zamani wa Ivory Coast na mshirika wake mkuu Charles Blé Goudé.

Lilikuwa pigo jingine kwa mahakama hiyo kwamba ni kwa ajili ya waasi au wanamgambo kuliko viongozi wahalifu wa mataifa, ambao kila wanapofikishwa mahakamani hatimaye huachiwa kwa madai ya ushahidi hukosekana.

Uamuzi wa majaji hao wakiongozwa na Jaji Cuno Tarfusser ulitokana na kile walichosema upande wa mashitaka kukosa ushahidi wa kutosha katika mashitaka dhidi yao.

Gbagbo na dogo wake huyo aliyemteua kuwa waziri wa vijana kipindi kile cha shinikizo la ndani na nje mwaka 2010/2011 walishitakiwa kwa mauaji, ubakaji, utesaji na matendo mengine yasiyo ya kibinadamu wakati wa machafuko baada ya kugoma kukubali matokeo yaliyompa ushindi mpinzani wake Alassane Ouattara mwaka 2010.

Outtara akiungwa mkono na Umoja wa Mataifa uliomsaidia kumchomoa Gbagbo kutoka Ikulu na kumpeleka ICC hatimaye akawa rais, ambao anaushikilia hadi sasa.

Waliachiwa licha ya upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi zaidi ya 80 pamoja na kufahamika wazi kitendo chao cha kung’ang’ania madaraka kilisababisha upotevu wa maisha ya watu 3,000.

Vifo hivyo vilitokana na vikosi vilivyoongozwa na ‘kamanda wa mitaani’ Goude kupambana na waandamanaji.

Gbagbo aliyezaliwa 1945, ambaye ni msomi anahesabiwa kuwa alikuwa tayari kuibomoa nchi yake kwa kugoma kukataa kushindwa kwake katika sanduku la kura.

Na kitendo chake cha kumteua Goude kuwa waziri wa vijana kipindi hicho, ilidhihirisha dhamira ya rais huyo ya kutokuwa tayari kusalimu amri dhidi ya shinikizo za ndani na nje ya nchi zinazomtaka ajiuzulu.

Kamanda au luteni huyo wa mitaani, akiwa mtu wa kuogopewa zaidi nchini humo wa Gbagbo.

Mara baada ya uwaziri huo anakumbukwa wakati alipotafuta vijana 5,000 hasa wale wanaomuunga mkono Gbagbo katika jeshi la Ivory Coast na baada ya wiki nne za mafunzo akawapatia bunduki aina ya AK47 na kuwasambaza mitaani.

Aidha anakumbukwa pia kwa kutoa kauli iliyolaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa, baada ya kutoa mwito kwa vijana wa nchi hiyo kuyavamia makao makuu ya serikali ya mpinzani wao   Alassane Ouattara.

Jumuiya ya Kimataifa ilimtambua Ouattara kama mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa mwaka huo, kitu ambacho Gbagbo hataki kukisikia, akidai kuibiwa kura katika eneo la kaskazini mwa nchi.

Baada ya kumaliza masomo yake ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Abidjan, kiongozi huyo wa vijana aliyekuwa na miaka 38 kipindi hicho sasa aliyejitengeneza kwa staili yake mwenyewe kisiasa, aliripotiwa kusomea usuluhishi wa migogoro katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.

Hata hivyo, mpenda ubabe huyo, maarufu kama ‘Jenerali wa Mitaani’ kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuwakusanya makumi kwa maelfu ya vijana mitaani ndani ya saa chache, kipindi chote cha uanafunzi wake, badala yake alionyesha kipaji cha kuchochea machafuko badala ya suluhu.

Ushabiki wake wa machafuko, mapenzi yake kwa wanamgambo na matamanio yake ya kisiasa huku akiwa na mlolongo wa kutupwa jela, kulimpatia uongozi katika shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu nchini humo (FESCI).

Mwaka 2002, wakati nchi ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe baina ya Gbagbo na waasi wa kaskazini, vuguvugu la Blé Goudé, Young Patriot lilikuwa nyuma ya kila maandamano ya yaliyomuunga mkono Gbagbo.

Mwaka 2004, wakati askari wa kulinda amani wa Ufaransa walipouawa katika shambulio la anga dhidi ya waasi wa kaskazini, kabla ya baadaye askari hao kujibu mapigo, Goude aliendesha kampeni za nguvu za kuchochea mashambulizi dhidi ya wageni, ambayo yalimweka katika orodha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa (UN).

Orodha hiyo ilitolewa Februari 7, 2006, na Kamati ya Vikwazo ya UN kwa kuchochea machafuko dhidi ya maeneo na maofisa wa UN, kuamuru na kushiriki katika machafuko ya mitaani, ikiwamo kupiga, kubaka na mauaji ya kikatili na kuwa kikwazo kwa mchakato wa amani.

“Mimi si mwanamgambo, ninaiweka sawa mitaa,” kiongozi huyo mcheshi lakini kiburi na katili wa wanamgambo wa Young Patriots aliwahi kukaririwa akisema.

Lilikuwa kundi lake lililoendesha maandamano makubwa mitaani mwanzoni mwa muongo huu, likitaka kuondoka kwa walinda amani wa UN na Ufaransa.

Young Patriots, kundi lililoundwa mwaka 2001 na ambalo jina lake kamili ni Congres Panafricain des Jeunes Patriotes (COJEP), linahusisha sehemu kubwa ya wanafunzi na vijana kutoka kabila la Bete.

Kundi hilo lilisambaza propaganda kwamba vita ya wenyewe kwa wenyewe kipindi hicho ni harakati za kupigania uhuru kutoka koloni la zamani Ufaransa.

Ble Goude alidai kwamba waasi ambao walikuwa wakidhibiti nusu ya kaskazini ya nchi ni vibaraka waliowekwa na Ufaransa, kauli ambayo iliwaingia Waivory Coast wengi miezi ya kwanza ya vita hiyo.

Hata hivyo, dhana hiyo ikafutika taratibu miongoni mwa vichwa vya wengi wakati machafuko yalipozidi kuongezeka.

Akitumia vyema hasira ya umma wakati ndege za Ufaransa zilipotokomeza karibu jeshi zima la anga la nchi hiyo, Novemba 2004, Ble Goude alikusanya makumi kwa maelfu ya vijana mitaani kupitia hotuba kali aliyoitoa kwenye televisheni.

Kauli yake ya kutaka kuondoshwa kwa jeshi la Ufaransa ilionekana wakati huo kama ruksa kwa vijana kufanya uasi mkubwa ulioambatana na uporaji dhidi ya nyumba za Wafaransa na biashara zao.

Mbali ya kuchochea chuki dhidi ya Ufaransa na UN, Ble Goude pia alichochea mashambulizi dhidi ya magazeti na waandishi wa habari wenye ukaribu na upinzani.

Rinaldo Depagne wa Taasisi ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro (ICG) alisema kipindi gicho kwamba  dogo huyo ni silaha muhimu kabisa kwa Gbagbo katika nyakati za vita.

“Gbagbo ana sauti mbili: sauti yake nyororo kwa ajili ya dunia ya Kimagharibi ambayo tumeisikia katika mahojiano mbalimbali, na sauti yake ya ndani kwa ajili ya wafuasi wake mitaani,” alisema na kuongeza; “Blé Goudé anawakilisha sauti ya pili na huwahesabu wanamgambo wa Young Patriots kama mbwa wake walinzi.”

Ble Goude alizaliwa katika mji wa katikati wa Guiberoua na akawa karibu na Rais Gbagbo wakati Gbagbo na mkewe Simone wakiwa bado wachanga na katika siasa za upinzani.

Akiwa mwanafunzi, Ble Goude pia alikuwa rafiki wa Guillaume Soro, kiongozi wa zamani wa lililokuwa kundi kuu la waasi la New Forces, na msemaji wa zamani wa waasi sidikui Konate.

Soro alikuja kuwa waziri mkuu katika serikali ya mpito kupitia makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2007, wadhifa ambao ulikuwa nao hadi mwezi uliopita baada ya kufanyika uchaguzi uliozua mgogoro mpya unaotishia kuirudisha nchi hiyo vitani.

Kimsingi Ble Goude umaarufu wake ulianzia pale alipomrithi Soro kama kiongozi wa FESCI, shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu lililojulikana kwa misimamo yake mikali kisiasa.

Baada ya Gbagbo kushinda uchaguzi wa urais wa mwaka 2000, Ble Goude alipata ufadhili wa kuendelea na masomo yake ya Kiingereza kabla ya kusomea usuluhishi wa migogoro katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.

Lakini alirudi nchini Ivory Coast baada ya kushindikana kwa jaribio la kumpindua Gbagbo Septemba 2002.

Kiingereza chake safi na uwazi wake kwa vyombo vya habari vya kimataifa kulimsaidia kumweka juu kisiasa.

Wanadiplomasia wanasema kwamba mkuu huyo wa wanamgambo wa Young Patriot tangu enzi mwanzoni mwa mwongo huu amekuwa akilipwa na rais.

Kipindi hicho amekuwa akiishi katika vyumba vya maalumu na vya kudumu katika hoteli ya nyota nne, huku akisafiri na walinzi.

Ble Goude alikuwa akisema hatapumzika hadi wapiganaji wa waasi waliokuwa wakidhibiti sehemu ya kaskazini ya Ivory Coast watakaposalimisha silaha zao.

Ble Goude alidai kwamba waasi ambao walikuwa wakidhibiti nusu ya kaskazini ya nchi ni vibaraka waliowekwa na Ufaransa, kauli ambayo iliwaingia Waivory Coast wengi miezi ya kwanza ya vita hiyo.

Hata hivyo, dhana hiyo ikafutika taratibu miongoni mwa vichwa vya wengi wakati machafuko yalipozidi kuongezeka.

Akitumia vyema hasira ya umma wakati ndege za Ufaransa zilipotokomeza karibu jeshi zima la anga la nchi hiyo, Novemba 2004, Ble Goude alikusanya makumi kwa maelfu ya vijana mitaani kupitia hotuba kali aliyoitoa kwenye televisheni.

Kauli yake ya kutaka kuondoshwa kwa jeshi la Ufaransa ilionekana wakati huo kama ruksa kwa vijana kufanya uasi mkubwa ulioambatana na uporaji dhidi ya nyumba za Wafaransa na biashara zao.

Mbali ya kuchochea chuki dhidi ya Ufaransa na UN, Ble Goude pia alichochea mashambulizi dhidi ya magazeti na waandishi wa habari wenye ukaribu na upinzani.

Mwaka 2006, pamoja na Rais Gbagbo kuunga mkono maridhiano na waasi, Blé Goudé aliendelea kuwa mstali wa mbele katika siasa kali za kizalendo.

Migogoro yake ya waziwazi na wanaitikadi kali na wanachama wa chama cha Gbagbo,  FPI, pamoja na kuendeleza mashambulizi dhidi ya wafuasi wa upinzani, hayo yamemfanya daima amulikwe mbele ya umma.

Mei 2007, Blé Goudé alikubali cheo cha ‘balozi wa amani wa Ivory Coast’ na alisafiri huko na huko akihubiri usuluhishi.

Patriots wanasema kwamba wao si wapenda machafuko huku Ble Goude akijifananisha na Martin Luther King.

Aidha anasema amekuwa akiwahusudu Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba na Thomas Sankara.

Moja ya kauli zake nyingi zisizosahaulika ni;  “Leo hatimaye nimefikia uamuzi kwamba sidhani kabisa Hitler alikuwa mbaya na kadhalika Milosevic. Kwa sababu vyombo vile vile vya habari vya kimataifa kama vile BBC, VOA, RFI, na kadhalika vivyowaeleza Hitler na Milosevic kuwa wahalifu, sasa vimenigeukia mimi na wana-Young Patriots, ambao tumeumia sana kutokana na uasi, kama wanyongaji, pamoja na kwamba ni sisi tunaoumia kutokana na waasi.”

Baada ya kuishi kama digidigi mafichoni, alikamatwa na polisi wa kimataifa nchini Ghana Januari 17, 2013 na kupelekwa Ivory Coast kukabili amshitaka yanayomkabili kabla ya mwaka uliofuata kwenda ICC, alikoachiwa huru mwezi uliopita.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,875FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles