25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

Hakielimu yatoa rai Serikalini kuhusu bajeti ya elimu 2024/2025

Na Esther Mnyika Mtanzania Digital

Taasisi ya Hakielimu nchini imetoa rai kwa Serikali kutenga bajeti ya kutosha 2024/2025 katika sekta ya elimu ili kuwezesha kushabihisha bajeti hiyo na malengo ya Dira ya Taifa ya maendeleo katika elimu lakini pia kuanza kwa utekelezaji wa mitaala na sera mpya ya elimu ya mwaka 2023.

Akizungumza leo Aprili 23,2024 na waandishi wa Habarijijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Hakielimu Dk. John Kalage amesema Serikali imefanya jitihada kubwa za kuleta mabadiliko na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu.

“Pamoja na Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu sisi tunapendekeza uzingatiwaji wa vipaumbele ili kuleta ufanisi katika sekta ya elimu,” amesema Dk. Kalage.

Ametaja vipaumbele hivyo ni pamoja na bajeti, inapaswa kuangalia namna ya kuajili walimu lakini pia kutoa mafunzo kwa walimu waliopo kwani mtaala mpya umekuja na majukumu ya ziada kwa walimu wa ngazi zote Msingi na Sekondari.

“Tunapendekeza Serikali itenge bajeti ya kutosha ili kuwapatia walimu wengi mafunzo ya mtaala mpya ili kuwezesha utekelezaji wa ufanisi kwani idadi ya walimu waliopatiwa mafunzo ni ndogo kulinganisha na idadi ya walimu waliopo,”amesema.

Amesema Serikali inapaswa kutoa mafunzo kwa walimu waliopo kazini lakini pia kuajiri walimu wapya na wenye uwezo na umahiri katika tahasusi kufuatia kuongezeka kwa tahasusi mpya 49 kidato cha tano kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia tahasusi 65.

Dk. Kalage ameongeza kuwa bajeti kwa ajili ya uchapaji na usambazaji wa vitabu vya kiada inapaswa kuongezwa pamoja na kuwa serikali imeweka juhudi kubwa katika Utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa bado shule nyingi hasa za umma bado hazijapata nakala ngumu(soft copies) ya vitabu hivyo kwa ajili ya utekelezaji.

“Pamoja na kuamini kuwa nakala tete(soft copies)zinaweza kuwa msaada mkubwa kwa walimu,sio kila mwalimu na mwanafunzi anauwezo na fursa ya kutumia nakala hizi kutokana na mazingira na uhitaji wake wa ujuzi katika teknolojia,”amesema.

Aidha amesema kwa kuwa mtaala ni chombo cha kulipelekea taifa katika dira ya maendeleo 2050 hivyo ni lazima mipango ya utekelezaji wa mtaala huo uoneshe wazi kuchangia matumizi ya Teknolojia kuanzia ngazi ya chini.

“Hakielimu inashauri Serikali kupitia wizara za sekta ya elimu kutenga bajeti kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari ili kuziandaa na utoaji wa elimu kwa mtaala mpya na matumizi ya Teknolojia,”amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kupanga bajeti kwa ajili ya marekebisho ya sheria ya elimu 2022 na utengenezaji wa mpango wa nne wa Maendeleo ya sekta ya elimu (ESDP IV).

“Kuanza kwa utekelezaji wa mtaala mpya elimu ya msingi na sekondari sio tu kunapelekea mabadiliko katika mfumo wa elimu bali pia kunaongeza hitaji la hatua za haraka ili kuhakikisha taifa linatekeleza mabadiliko haya kwa ufanisi,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles