24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

RONALDINHO GAUCHO NA UCHAWI WAKE WA SOKA 1998 – 2018


ADAM MKWEPU NA MITANDAO

UNAWEZA kutamani kila kitu utakachokiona katika mwili wa Ronaldo de Assis Moreira na ana majina mengi huyu binadamu, lakini maarufu anajulikana kwa jina la Ronaldinho Gaucho.

Huyo ni fundi wa mpira ambaye hajadumu sana kwenye ulimwengu wa soka, ila jina lake litaendelea kudumu hadi mwisho wa maisha yake.

Unaweza kuwa mpinzani wake na kumshutumu. Lakini mwisho wa siku utabaki kuwa shabiki wake. Na utaguswa na kutamani kumbukumbu zake.

Ronaldinho, ambaye amemaliza soka lake akiwa Atletico Mineiro, aliumia kuona anamaliza soka lake huku akishindwa kutwaa taji la Kombe la Dunia la klabu, baada ya kufungwa na Raja Casablanca.

Nguli huyo mwenye umri wa miaka 37, alishindwa kuisaidia timu yake kabla ya kuamua kustaafu kucheza soka la kulipwa. Alistaafu akiwa na maumivu mengi, licha ya tabasamu lake mororo mbele ya kadamnasi.

Unaweza kumuona Zinedine Zidane akiwa kwenye ubora wake, Thierry Henry, Didier Drogba, Raúl González Blanco,  Daniel Rodríguez ‘Toti’, Miroslav Klose na wengine, lakini bado utakoshwa zaidi na Gaucho.

Zama hizi zinatawaliwa na mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ‘CR7’ pamoja na Lionel Messi wa Barcelona, wanafanya madoido mengi sana hawa watu, lakini bado hawajafanikiwa kuifuta picha ya Gaucho kwenye ubongo wa wapenda burudani ya mpira duniani.
Gaucho acha aitwe Gaucho, anakupiga tobo huku anacheka, anakuvisha kanzu huku anacheka.Timu ikipata ubingwa wa Dunia yeye anacheka, ikitolewa robo fainali bado anacheka.
Haya mabao tunayobishana siku hizi, yeye alishayafunga kitambo, chenga ndo usiseme, mipira ya adhabu ndo baba lao.

Messi, CR7, Franky Ribery wa Bayern Munich hata kama wakichukua tuzo ya mchezaji bora, Ballon d’Or mara 10 kila mtu, bado Gaucho atawafunika wote kwenye ubongo wa wapenda burudani.
Ana mambo mengi huyu mtu ndani na nje ya uwanja, kwani kabla wakina Theo Walcott hawajaja na sura zao za mahaba, Gaucho alishawateka wanawake kitambo. Huyu jamaa katimia kila kona.

Huyo ndio nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na klabu za PSG, Barcelona na AC Milan. Licha ya kutocheza soka la kiushindani tangu mwaka 2015, amekuwa akicheza michezo ya mabonanza.

Kaka na wakala wa mchezaji huyo, Roberto Assis, amethibitisha kuwa umefika mwisho kwa fundi huyo wa Brazil kucheza soka.

Ronaldinho alianzia soka yake katika klabu ya Gremio ya nchini kwao, kabla ya kujiunga na Paris St-Germain mwaka 2001 na baadaye kujiunga na Barcelona alikong’ara sana.

Katika msimu wa 2010 -2011 alijiunga na AC Milan ya Italia, kabla ya kurudi kwao na kujiunga na Flamengo mwaka 2011. Kisha alichezea klabu ya Atletico Mineiro, na Queretaro ya nchini Mexico, na kurudi tena kwao Brazil katika klabu ya Fluminense.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ambaye alimuuza nyota huyo AC Milan, anasema kwamba Gaucho akiwa Barcelona hakukuwa na mchezaji yeyote wa kumfananisha naye kabla ya kutokea Messi.

Ronaldinho aliisaidia Barcelona kuwa katika msingi wake ambao unaonekana sasa kama ambavyo anasema Guardiola, ambaye alimuuza nyota huyo ili kuandaa utawala mpya wa Messi ndani ya klabu hiyo.

Gaucho ameshinda taji la La Liga mfululizo, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ballon d’Or wakati wa utukufu wake kutoka mwaka 2003 hadi 2008.

Hata alipoondoka Barcelona ilimchukua muda Guardiola kutengeneza upya hitilafu iliyotokana na misingi aliyoacha Gaucho.

“Wakati Joan Laporta alipokuwa rais wa Barcelona alisababisha athari kubwa na alipomsaini Ronaldinho ulikuwa mvuto mkubwa kwa Barcelona.

“Ilisaidia kurejesha mustakabali wa klabu baada ya kipindi kirefu kupotea. Laporta akiwa rais na Ronaldinho ndani ya uwanja kwa pamoja walisaidia kurudisha heshima ya klabu kwa kipindi hicho. Gaucho alikuwa na mwaka mzuri alipoanza kucheza Barcelona, alishinda taji la ligi na Ligi ya Mabingwa Ulaya,” anasema Guardiola.

Guardiola anasema: “Alikuwa ni mchezaji wa daraja la juu hadi Messi alivyofika, lakini sikuwahi kumwona mchezaji wa aina yake kabla.

“Namtakia safari njema katika maisha yake, ana sifa nyingi si tu Barcelona, bali katika ulimwengu wa soka.”

Ronaldinho ametokea kwenye familia ya watoto watatu, wa kike akiwa mmoja, lakini Ronaldinho alikuwa wa mwisho kuzaliwa katika familia ya mzee Joao de Assis Moreira, ambaye alikuwa anafanya kazi kwenye meli. Alizaliwa Machi 21, 1980.

Maisha ya familia hiyo kwenye mji wa Porto Alegre huko nchini Brazil yalikuwa ya kawaida sana, kwa kuwa baba yao alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo, lakini maisha yao yalianza kubadilika baada ya kaka wa mchezaji huyo, Roberto de Assis, kusajiliwa na klabu ya Gremia.

Ronaldinho alianza kupenda mpira huku akiwa na umri wa miaka nane, alipata nafasi ya kucheza timu za mtaani na alionesha kiwango cha hali ya juu, alipata sifa nyingi kwa kuwa alionekana mchezaji mfupi na mdogo kwenye michuano ya mtaani, lakini alikuwa na uwezo wa pekee.

Alianza kutambulika akiwa na umri wa miaka 13, baada ya vyombo vya habari kumuandika na kumuita jina la Ronaldinho, kutokana na kupachika mabao 23 peke yake kwenye mchezo mmoja wa ligi za mtaani, huku timu yake ikishinda mabao 23-0.

Kutokana na kiwango hicho, Ronaldinho akachukuliwa na timu ya vijana ya Gremio, ambayo kaka yake alikuwa anacheza ya wakubwa, hivyo mwaka 1998 alipandishwa timu kubwa na kuonesha uwezo wake hadi 2001 alipojiunga na PSG.

Dunia ilianza kumtambua vizuri mchezaji huyo mwaka 2003, alipojiunga na klabu ya Barcelona, hadi pale alipoondoka mwaka 2008 na kujiunga na klabu ya AC Milan.

Dunia ilitamani kumuona mchezaji huyo zaidi ya miaka 10 akiwa na kiwango ambacho alikionesha katika klabu ya Barcelona, lakini kitu kinachopendwa zaidi na watu wengi hakiwezi kudumu sana, ndicho kilichotokea kwa Ronaldinho.

Mchezaji huyo aliwahi kushangaza dunia baada ya kupigiwa makofi na mashabiki wa Real Madrid kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, huku akiwa na klabu yake ya Barcelona, hiyo ni kutokana na na kukubalika na mashabiki duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles