28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Gariboti linalotembea nchi kavu, majini kuweka rekodi nchini

GariBoti

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

MAENDELEO ya teknolojia duniani yamezidi kushika kasi siku hadi siku huku kukishuhudiwa watu mbalimbali wakionyesha uwezo wao hasa katika kuvumbua vitu ambavyo kwa namna moja ama nyingine vimesaidia kurahisisha shughuli za maendeleo.

Mashine, magari, mitambo na vitu vingi tunavyoviona leo hii ni matunda ya kukua kwa teknolojia sekta inayotajwa kukua kwa kasi nchini na duniani kwa ujumla.

Mchango wa sekta hiyo umeonekana mkubwa hasa katika kupunguza tatizo la ajira nchini kwani hivi sasa Watanzania wengi wameonyesha uwezo mkubwa katika kuvumbua bidhaa mbalimbali ambazo zimeingia sokoni na kukubalika kwa hali ya juu.

Katika Maonyesho ya Kimataifa ya 40 Biashara maarufu kama Sabasaba yaliyomalizika wiki iliyopita Katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), imeonyesha kwa vitendo namna inavyoendeleza teknolojia kwani imekuwa mfano hasa katika ugunduzi wa mambo mbalimbali yenye manufaa katika maisha ya kila siku.

Mamlaka hiyo ambayo iliibuka na kuwa washindi wa jumla ilionyesha kwa vitendo namna walivyoweza kuvumbua bidhaa mbalimbali na kuwa kivutio kikubwa katika maonyesho hayo.

Mojawapo ya kifaa kilichokuwa na mvuto ni botigari linalotembea baharini na nchi kavu ambapo aliyebuni gari hilo ni Mwalimu Emmanuel Bukuku wa Chuo cha Ufundi (VETA), Chang’ombe, Dar es Salaam.

Bukuku kwa kushirikiana na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo hicho Mohamed Hamza na Joseph Mbwilo walibuni gariboti ambalo lilikuwa kivutio hasa kwa watu waliofika katika maonyesho hayo.

“Baada ya ubunifu niliwashirikisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika uchomeleaji na uundaji wa vyuma katika kulitengeneza,” anasema.

Anasema walianza kuliunda gari hilo mwaka 2012 na hadi sasa gari hilo linatembea nchi kavu na lipo kwenye hatua za mwisho kulifanyia mazoezi ili liweze kutembea baharini.

“Kwenye maji kuna baadhi ya vifaa inatakiwa tuvifunge kuziba matundu ili iweze kutembea na tunaendelea na mchakato ili kuvifunga na hatimaye tufanye majaribio baharini,”anasema Bukuku.

Anasema baada ya kukamilika matengenezo boti hiyo itakuwa na kamera yenye uwezo wa kuchukua picha baharini na nchi kavu.

Mwalimu huyo anasema gari hilo linatembea kwa kutumia mifumo inayojiendesha ya mafuta na kwamba linatumia mafuta ya dizeli.

“Gari hili litakuwa na mabawa na linapokuwa nchi kavu linanyanyuka na likiwa baharini linashuka kulisaidia kuelea katika maji. Litakuwa na sehemu nne ya kukaa watu na eneo maalumu kwa uchunguzi baharini hususan chini ya bahari,” anasema.

UJUZI

Bukuku anasema katika chuo hicho yuko katika kitengo cha mashine uvumbuzi wa vifaa tofauti ambacho kimekuwa kikimsukuma kila kukicha kuunda kitu kipya ambacho kitasaidia jamii ya sasa na kizazi kijacho.

Anasema aliwahi kutengeneza boti yenye uwezo wa kupiga picha baharini na kutuma ambayo ilichukuliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Pia alishawahi kutengeneza mashine ya kuita samaki baharini, kufukuza ndege na nyinginezo ambazo zimekubalika katika jamii imezikubali na serikalini pia.

“Serikali ilikuja kwenye maonesho wakaiona mashine ya kufukuzia ndege na kuisifia sana lakini hakukuwa na jitihada zingine za kuendeleza hadi walipojitokeza wawekezaji nje na kuinunua kisha kuipeleka katika Mikoa ya Iringa na Mbeya ambako wanasema imeleta matokeo mazuri,”anasema Bukuku.

Anasema alifanya uvumbuzi huo ili kuwawezesha wanasayansi wanaofanya tafiti baharini au kwenye maji.

WANAFUNZI

Naye mwanafunzi Joseph Mbwilo ambaye ameshiriki katika ugunduzi huo anasema hatua hiyo imemuongezea uwezo wa kufikiri zaidi na kufanya vitu kwa faida ya taifa na kizazi kijacho.

Anasema anashukuru kwa nafasi hiyo ambayo kwake anaona kama ni adimu kwa sababu wanafunzi wengi wanaoshiriki kwenye ugunduzi ni wa mwaka wa pili na tatu lakini yeye na mwenzake Mohamed Hamza wamepata bahati ya kushiriki.

“Elimu yangu nililiyonayo ni ndogo ya kidato cha nne tu lakini kwa sasa ninaipenda fani hii kutoka moyoni nina imani ipo siku nitatoka na kuwa maarufu kwa sasa ya kugundua vitu mbalimbali vyenye kuisaidia jamii,”anasema Mbwilo.

CHANGAMOTO

Mwalimu Bukuku anasema wagunduzi wengi ni wazalendo lakini wanakatishwa tamaa kutokana na kasumba ya Watanzania kutopenda kununua bidhaa zinazotengenezwa nchini.

“Tunakatishwa sana tama yaani unaweza kubuni kitu wakaja watu kutoka nje wakakikubali lakini Mtanzania mwenzako anakibeza, hali hii inaumiza sana na kama usipokuwa mvumilivu unaweza kujikuta unashindwa kuendelea au kuongeza ugunduzi zaidi,” anasema.

Mwalimu huyo anapendekeza kuwepo na tamasha la wagunduzi ili kuwawezesha kusonga mbele kwa kuwakutanisha na wadau mbalimbali.

“Iko haja ya kuanza kujitangaza kwa sababu mfano madini ya chuma wenzetu Ujerumani wamepiga hatua wanasifika wakati vyuma vinapatikana Afrika na hii yote ni kutokana na kukosa uendelezaji na urasimishaji wa shughuli mbalimbali,”anasema Bukuku.

Anaishauri serikali kutenga fungu la kuwawezesha wagunduzi na kutatua matatizo yao ikiwa ni pamoja na kujenga utamaduni wa kuwekeza katika elimu badala ya biashara.

SERIKALI

Uvumbuzi wa bidhaa hizo umeifanya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. Magufuli kuanzisha ari ya kufufua viwanda ili kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda.

Katika kuhakikisha wazalishaji nchini wanapewa kipaumbele Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewagiza wazalishaji nchini kuhakikisha wana nembo ya Msimbomilia kabla ya kupewa cheti na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Nembo hiyo itasaidia kuwainua wazalishaji wa hapa nchini kutokana na bidhaa kupata thamani na uzalishaji wa bidhaa bora kuongezeka na hatimaye kuingia kwenye ushindani wa kimataifa.

Waziri huyo anasema pia atawezesha kupatikana kwa vibali kwa vifaa vitakavyoonekana vina manufaa ili vitumike nchini.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, anasema kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) wataendeleza ubunifu unaofanywa na mamlaka hiyo badala ya kuagiza vitu nje ya nchi.

Wakati Serikali ikiwa katika mchakato wa kufanya mapinduzi ya viwanda ni muhimu ugunduzi wa mambo mbalimbali yenye manufaa katika maisha ya kila siku ukapewa kipaumbele na kuhakikisha wagunduzi wanaungwa mkono katika bidhaa wanazobuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles