24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Hivi ndivyo kodi inavyokusanywa

Efd-Machine
Efd-Machine

Na Koku David, Dar es Salaam

KWA kutambua umuhimu wa kulipa kodi na uelewa mdogo uliopo kwa wananchi walio wengi, MTANZANIA limeamua kuanzisha safu hii ambayo itakupa fursa mteja wetu kuweza kupata darasa kuhusu masuala ya kodi na jinsi inavyotakiwa kulipwa.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilianzishwa kwa sheria ya Bunge sura namba 339 ya sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1995 na kuanza kufanya kazi Julai mosi, 1996.

TRA imepewa jukumu na serikali kuhakikisha inakusanya kodi kutoka kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi, pia inawajibu wa kuhakikisha inasimamia kwa uadilifu mkubwa sheria mbalimbali za kodi za serikali kuu.

Katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ya ukusanyaji wa kodi, TRA inapaswa kufanya kazi hii kwa mujibu wa  sheria za kodi inazozisimamia kama ilivyoainishwa na jedwali la kwanza la sheria iliyoiunda TRA.

Katika ukusanyaji wa mapato, Serikali inamtaka kila mtu mwenye mapato kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 2004 na kwamba kodi hiyo inatakiwa kulipwa katika awamu nne katika mwaka wa mapato.

Katika mwaka wa mapato, mfanyabiashara atakadiriwa kodi ya mwaka mzima kulingana na mapato anayopata katika biashara yake na sheria inamtaka kutunza kumbukumbu za biashara ili makadirio ya kodi yatakayofanywa yaendane na hali halisi ya mauzo na manunuzi katika biashara husika.

Mpaka sasa, wafanyabiashara wameshalipa kodi ya awamu ya kwanza ambayo ni kipindi cha Januari hadi Machi 2016, na sasa wameshafikia mwisho wa kumaliza kukusanya kodi ya mapato awamu ya pili ambayo ukomo wake ulikuwa ni Juni 30, 2016 kama sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 inavyowataka kufanya.

Kwa mujibu wa sheria ya kodi ya Mapato ya 2004, mwaka wa mapato ni mwaka wa kalenda ambao  huanzia Januari hadi Desemba, lakini ulipaji wa kodi ya mapato umegawanywa katika awamu nne ambazo ni kuanzia Januari hadi Machi, Aprili hadi Juni, Julai hadi Septemba na awamu ya mwisho ni Oktoba hadi Desemba.

Kutokana na kuwa mlipakodi ndiye anayejua biashara yake inavyokwenda, anaruhusiwa kumuomba Kamishna wa Kodi ili amruhusu kuwa na mwaka wa mapato tofauti na ilivyoelezwa katika sheria.

Kuna aina tatu ya vyanzo vikuu vya mapato vinavyotambulika kisheria ambavyo ni mapato yatokanayo na biashara, ajira pamoja na mapato ya uwekezaji.

Unaposema mapato yatokanayo na biashara ni jumla ya mafao au faida ambayo mfanyabiashara anaipata kwa kufanya biashara ikihusisha ada ya huduma, bidhaa za biashara, faida itokanayo na kuuza mali na madeni ya biashara. Malipo kwa kukubali masharti ya biashara na zawadi zilizopokelewa kwa ajili ya kufanya biashara.

Mapato ya ajira ni yale anayopata mtu kutokana na ajira yake, hii inahusisha mshahara wa mwisho wa mwezi anaopata mfanyakazi, malipo badala ya likizo, bonansi, alawansi, malipo ya kukosa ajira, malipo ya mwisho ya ajira na malipo kwa kukubali masharti ya ajira.

Katika mapato ya uwekezaji, mwekezaji atatakiwa kulipa kodi kulingana na mapato anayopata kutoka katika uwekezaji wake. Kwa mfano; mtu akijenga nyumba na kuzipangisha huyo anatambulika kama mwekezaji hivyo kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato 2004 atatakiwa kulipa kodi ya mapato ya asilimia 10 ya malipo atakayolipwa kama pango la nyumba na itatakiwa kupelekwa TRA na mpangaji husika kutokana na kwamba yeye ndiye anayefaidika na huduma itokanayo na nyumba hiyo.

Eneo lingine ambalo kodi ya mapato hutozwa ni pale mtu anapouza eneo au nyumba ambapo wahusika wote watatakiwa kuwasiliana na TRA kwani mauziano hayo hayawezi kukamilika hadi kibali cha kodi kitolewe kwa kamishna wa ardhi ambaye ndiye mwenye uwezo wa kufanya uhamishaji wa milki ya ardhi husika baada ya kodi ya mapato kulipwa.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa Ofisa Mkuu wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Tanzania (TRA), Richard Kayombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles