23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

FURSA ZA UWEKEZAJI ZINAHITAJI MJADALA MPANA

Na Mwandishi Wetu


BIASHARA ni shughuli kongwe sana na yenye kuibua changamoto kila uchao toka zama hizo.

Changamoto zake zinadai ubunifu ili kusonga mbele. Watanzania lazima tukubali ukweli huu na tujifunze kutoka kwa mataifa mengine.

Kikubwa cha kujifunza ni kwamba fursa za uwekezaji daima zitahitaji mjadala mpana, nia njema na kutanguliza masilahi ya Taifa mbele.

Ni kweli Watanzania tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa mataifa mengine.

Mwaka 1898, Rais wa 25 wa Marekani, William McKinley, alianzisha utaratibu ulioonekana mpya kwa jamii ya Kimarekani. Aliamua kufanya biashara na China ya wakati ule, jambo ambalo kwa wakati huo lilionekana ni kituko. Uamuzi huo akauwekea  utaratibu ulioitwa  sera ya kufungua milango (Open Door Policy).

Sera hii hadi sasa inatumika nchini humo; ni sera ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kukuza uchumi na leo uchumi wa Marekani ndiyo mkubwa kuliko chumi zote duniani. Marekani hata ukipeleka njugu zitauzika kwa faida kubwa, kinachotakiwa ni kuwa na bidhaa zenye ubora na viwango vya hali ya juu. Mazingira ya kufanya biashara ni ya uhakika kwa kila mwekezaji.

Toka mwaka 1967, Serikali iliwania kumiliki njia kuu za uchumi. Lakini  wakati Rais mstaafu, Ali Hasaan Mwinyi anachukua uongozi mwaka 1986, athari hasi za vita  na Idi Amini zilikuwa kali, uchumi wa dunia ulitibuka, ukazuka utandawazi na biashara duniani ikawa ngumu sana. Hapa ndani  mashirika ya umma yalikuwa yanayumba sana na mengine yakafilisika.

Rais mstaafu aliyefuata, Benjamin Mkapa, alishiriki katika jitihada za kimataifa za kuufanya utandawazi  unufaishe mataifa yote. Jitihada hiyo haikuzaa matunda makubwa.

Mwaka 2001, Mkapa alianzisha kitu kama ‘open door policy’ kwa sababu athari hasi za utandawazi na uchumi wa Taifa ulikuwa unayumba.

Tayari ilikwishatoka hoja iliyopendwa sana, kwamba Serikali haiwezi kufanya  biashara.

Mkapa  aliamua kuanzisha chombo cha kuwakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na Serikali ili kujadiliana kwa pamoja changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.

Chombo hicho kikaitwa  Baraza la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Council-TNBC). Baraza lilianzishwa kupitia waraka wa rais namba moja wa Septemba 12, 2001.

Malengo ya TNBC ni  kuibua  ushauri na kusikiliza kero za pande zote mbili; sekta binafsi na sekta ya umma yaani baraza ni daraja kati ya pande mbili.

Kila mwaka kunakuwa na mkutano wa kujadili changamoto wanazokumbana nazo watendaji katika  sekta ya umma na ya binafsi hadi mwaka huu imeshafanyika mikutano 10.

Mkutano wa mwisho umefanyika Mei 6, mwaka huu katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa mikutano hii kiutaratibu anakuwa rais wa Tanzania.

Nimejaribu kuleta historia fupi ya TNBC ili kuwa sawa katika hiki ninachotaka kueleza.

Pamoja na ukweli kwamba  malengo ya kuanzishwa utaratibu wa kufungua milango kwa wafanyabiashara na wawekezaji yalikuwa mazuri, bado kuna mazingira yanayowakwaza wawekezaji; ama kwa makusudi au kwa kutoelewa  misingi na mipaka ya sheria zilizowekwa na mamlaka husika.

Katika uongozi wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, mikutano mingi ya TNBC ilikazania  kuweka mazingira bora ya biashara nchini.

Lakini ni salama kusema bado kuna dalili za pande zote mbili kutoaminiana.

Katika mkutano wa sita iliamuliwa kuwa, Presidential Delivery Bureau (PDB), TNBC na TPSF (Taasisi ya Sekta Binafsi), wasimamie masuala mtambuka yanayoonekana yanajirudia kila mwaka katika malalamiko ya sekta binafsi.

Katika mkutano wa saba, Mwenyekiti  Kikwete aliamua kuundwe kikosi kazi kitakachosimamia kuwepo kwa  mazingira bora ya biashara Tanzania. Hata hivyo, hadi anaondoka madarakani inaonekana  suala hili halikupata ufumbuzi.

“Kuimarisha mazingira ya biashara ni suala muhimu katika mikakati ya kukuza uchumi kwa Watanzania wengi,” alisema Mwenyekiti Kikwete katika mkutano wa saba wa Baraza.

President Delivey Bureau (PDB) ni idara maalumu ndani ya ofisi ya rais iliyoanzishwa mwaka 2013 kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Malalamiko yanayojirudia ni upatikanaji ardhi, mikopo nafuu ya benki, kodi, mikataba ya kimataifa na sheria ya kazi.

Rais Kikwete katika mkutano wake wa mwisho  wa baraza alisema: “Tunahitajika kuweka mazingira bora ya biashara ikiwa tunataka kuimarisha maendeleo endelevu.

“Nakiri biashara ndiyo itakayoleta maendeleo nchini na hatimaye kufuta umasikini. Hili pia linanikumbusha kuwa ili biashara iwe huru na ipewe nafasi ya kutosha, ni lazima Taifa liweke mazingira bora ya wawekezaji na hii ni kazi ya Serikali kufanya yote haya. Lazima Serikali na sekta binafsi wawe na majadiliano murua yatakayoleta mabadilko kwenye biashara na uwekezaji.”

Katika mkutano wa mwaka huu, ulikuwapo mjadala mrefu katika maeneo hayo. Wajumbe  wa sekta binafsi walieleza  mlolongo mrefu wa tozo na kutoshirikishwa katika mabadiliko ya sera na ulipaji kodi.

Mkutano wa mwaka huu ulikuwa  wa kwanza kuongozwa na Rais John Magufuli. Nao ulisisitiza kuwa lazima Serikali iwe karibu na sekta binafsi ili kujua matatizo yao.

Ingawa kuna matatizo hayo lakini Tanzania ina bahati moja, majadiliano yanaibua nia njema ya kulitumikia na kulinufaisha Taifa.

Nia hii unaweza kuigundua kwa kuelewa kilichotokea wakati wa mkutano uliofanyika hivi karibuni. Wakati ratiba ya mkutano ikisomwa, ilionekana mjadala kati ya sekta binafsi na umma ungechukua chini ya saa moja; takribani dakika 45 na saa nyingine zingetumika kwa hotuba na taarifa za Serikali.

Lakini Mwenyekiti Magufuli akasema lazima wawakilishi wa  sekta binafsi wapewe muda mwingi ili waeleze dukuduku walizonazo. Kwa saa tatu  wafanyabiashara walisikilizwa na Serikali ilipewa muda wa kujibu.

Wa kwanza kujibu alikuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema ni kweli kuna baadhi ya maeneo watendaji wamelala, akatilia msisitizo Mamlaka ya Bandari (TPA) kuwa kazi zifanyike saa 24 kuhudumia taasisi na mamlaka zote.

“Hakuna sababu za kushindwa na Bandari ya Mombasa, wenzetu wanatumia siku tatu kutoa mizigo sisi tunatumia wiki nzima, haiwezekani. Naagiza kuanzia Jumatatu (Mei 8, 2017) TRA, TFDA na mamlaka zote miambata pale bandarini zifanye kazi saa 24, fedha na vifaa si vipo?”

Kuhusu suala la ardhi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema: “Changamoto ya ardhi ilikuwepo lakini sasa mambo yamebadilika. Niwahakikishieni  wafanyabiashara, mtu yeyote anayetaka ardhi anifuate. Ukishalipia na kufuata taratibu zote ndani ya saa 24 unapata hati yako,” ameahidi.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba, aligusia changamoto ya upatikanaji pembejeo za kilimo hasa mbolea. Akasema Serikali inajipanga kutunga sera ili kuwe na mtu mmoja anayeagiza mbolea kutoka nje.

“Hili litatusaidia kudhibiti bei.  Mheshimiwa Waziri Mkuu huko ulikoona bei za mbolea zinatofautiana na mahali pengine mbolea za ruzuku zinauzwa kwa bei kubwa ni kwa sababu waagizaji wamekuwa wengi. Tutadhibiti uingizaji wa mbolea kwa manufaa ya wakulima,” alisema Tizeba.

Tukiri matatizo kwa nchi masikini kama Tanzania ni mengi, magumu na yanahitaji nia njema kuyatatua.

Kila aliyekuwa katika mkutano huu ni shahidi wa majadiliano yenye nia njema na kuaminiana. Majadiliano ya aina hii yanapunguza sana  chuki na hali ya kukata tamaa na yanaibua ari ya kulitumika Taifa kwa moyo mmoja.

Pengine ni kwa sababu ya funzo hili Rais Magufuli aliagiza kwa bashasha kwamba uandaliwe mkutano mwingine  maana uzoefu tayari umeonyesha kwamba mjadala mpana,  wenye nia njema na kutanguliza masilahi ya Taifa mbele unaleta ufumbuzi wa kero na  matatizo ambayo juu juu yanonekana magumu na ya kutisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles