28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

TRA, TIB YAINGIA MAKUBALIANO KUKUSANYA MAPATO BANDARINI

Na KOKU DAVID


MWISHONI mwa wiki iliyopita, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliingia mkataba na Benki ya Biashara ya TIB (TIB Corporate) ili iisaidie mamlaka hiyo kukusanya mapato ya bandarini pamoja na kodi.

TIB imekuwa benki ya kwanza kuingia makubaliano na mamlaka hiyo katika suala zima la ukusanyaji mapato ya bandari pamoja na kodi kutoka kwa walipakodi.

Katika makubaliano hayo, Benki ya TIB iliunganisha mifumo yake ya benki pamoja na mifumo ya malipo ya kodi ya TRA, kwa lengo la kukusanya kodi bandarini.

Pamoja na kuisaidia TRA kukusanya kodi, pia ni katika kutekeleza agizo la Serikali la kutengeneza mazingira mazuri kwa walipakodi ili waweze kufanya miamala ya ulipaji kodi kwa haraka na ufanisi.

Sambamba na hayo pia utaratibu huo utasaidia kuwarahisishia  walipakodi kulipa kodi muda wowote kutokana na kuwa benki hiyo tayari imeshafungua tawi dogo maeneo ya bandari.

Katika ofisi za benki hiyo tawi la bandari, kutatolewa huduma zote za benki kwa saa 24 na kwamba mlipakodi ataweza kulipa kodi yake muda wowote.

Hii ni miongoni mwa mikakati ya TRA ya kuhakikisha inawatengenezea walipakodi mazingira mazuri ya kuweza kulipa kodi kwa hiyari na bila ya kupata usumbufu wowote.

Mbali na TIB, pia mamlaka hiyo imekuwa ikifanya kazi na benki mbalimbali katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ili kusaidia kufanikisha malengo ya Serikali ya kukusanya kodi kwa kila anayestahili kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, mamlaka hiyo ilifungua milango kwa benki nyingine ambazo ziko tayari kushirikiana nayo katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya bandari pamoja na kodi.

Ili kupata nafasi ya kuingia katika makubaliano hayo, TRA imezitaka kujipanga ikiwa ni pamoja na kufungua matawi katika maeneo ya bandari.

Kila mlipakodi atakayelipia kodi yake kupitia benki, mfumo wa benki  katika malipo ya kodi moja kwa moja utaonyesha malipo hayo katika mifumo iliyopo TRA.

Utaratibu huu wa kulipia kodi benki utamrahisishia mlipa kodi kulipa kodi kwa haraka bila usumbufu kutokana na ufanisi uliopo katika mifumo husika.

Pia utaratibu huo wa kulipia benki utapunguza malalamiko ya walipakodi ya kudaiwa kodi mara mbili na watumishi wa mamlaka wasio waaminifu.

Aidha, kutokana na mfumo huo utapunguza uwezekano wa makosa katika ulipaji wa kodi.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, anasema mfumo huo ni wa kisasa na kwamba mlipakodi anaweza kulipa kodi yake kupitia tawi lolote la benki hiyo na kwa muda mfupi taarifa zake zikaonekana katika mfumo wa TRA.

Anasema kwa kutumia mfumo huo, itamrahisishia mlipakodi kufanya muamala wa kulipa kodi kwa haraka na kuendelea na shughuli zake nyingine.

Anasema mikakati ya TRA ni kuhakikisha mlipakodi analipa kodi stahiki na kwa urahisi bila ya kupata usumbufu, ikiwa ni pamoja na kuisaidia Serikali kupata kodi yake stahiki kwa mujibu wa sheria.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles