27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Fukuto la wapinzani lapania kumwondoa Rais Mugabe

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe

NA BALINAGWE MWAMBUNGU,

NILIWAHI kuandika huko nyuma kwamba viongozi kama Mugabe waogopwe, nikashambuliwa na baadhi ya wasomaji, hawakujitaja majina, lakini nadhani ni watu waliowahi kuwa karibu na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Nikaambiwa kuwa nilikuwa ‘kasuku’ wa mawazo ya Kizungu (Eurocentric copy-cat).

Lakini niliyoyaandika miaka 2007 (miaka 9) iliyopita sasa yanatokea nchini Zimbabwe. Maelfu kwa maelfu ya wananchi wiki iliyopita, waliandamana kupinga utawala wa Mugabe na wakionesha kuchoshwa na maisha duni yanayotokana na kuanguka kwa uchumi mnamo mwaka 2009, ufisadi na umasikini unaozidi kuongezeka nchini humo.

Nchi hiyo sasa inatumia fedha aina mbili Dola ya Zimbabwe (haina thamani) na Dola ya Kimarekani. Aidha, wananchi wanapinga mipango ya Benki Kuu ya kutaka kubadili noti na kuingiza sokoni dola mpya kwamba itakuwa na madhara makubwa na watu wengi waliojiwekea akiba, watafilisika.

Wakati naandika wakati ule, Zimbabwe ilikuwa imetoka kufanya Uchaguzi Mkuu na nilivinukuu vyombo vya nje na waangalizi wa kimataifa waliotamka bayana uchaguzi ule haukuwa huru na wa haki.

Wananchi wa Zimbabwe (kama Watanzania katika Uchaguzi Mkuu uliopita), walishindwa kufanya mabadiliko ya kisiasa, japo dalili zote zilionekana kwamba upinzani ulikuwa na nguvu na uwezo wa kukiondoa madarakani chama cha Rais Mugabe cha ZANU-PF.

Rais Mugabe (92), amekuwa madarakani kwa miaka 36 sasa. Amekuwa akiendesha chaguzi kama kiini macho tu kama wafanyavyo baadhi ya viongozi barani Afrika. Ni nchi chache sana ambazo zimewahi kuendesha chaguzi huru na za haki katika Afrika.

Viongozi wengi walio madarakani, hawataki kuondoka na hivyo kutumia hila nyingi ili waonekane bado wanakubalika na wananchi.

Nguvu za kisiasa za Mugabe zilitokana na kuungwa mkono na wanajeshi waliopigana kwenye vita vya msituni vilivyoangusha utawala wa Wazungu wachache walowezi  na Waafrika vibaraka. Lakini kabla ya maandamano ya Ijumaa iliyopita, Maveterani wa vita vya msituni nao maji yamewafika shingoni.

Hali yao ya maisha ni mbaya. Mapema mwezi huu, waliandamana na kwa mara ya kwanza wakasusia hotuba ya Rais Mugabe katika sherehe za kila mwaka za kuwaenzi. Maveterani hao walimtaka Mugabe aachie ngazi na baadhi yao walikamatwa na polisi. Maveterani pia wanadai nyongeza ya pensheni. Badala ya kukaa kitako na kuwasikiliza, Serikali ya Mugabe ikawapiga kwa mabomu ya moshi na kuwatawanya.

Sasa Maveterani hao kupitia chama chao cha Zimbabwe National Liberation War Veterans, wameamua kumuunga mkono aliyekuwa Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Joyce Mujuru, ambaye wanasema alikuwa na mchango mkubwa wakati wa vita ya ukombozi. Mujuru aliunda chama chake cha Zimbabwe People First (ZPF), baada ya kufukuzwa kazi na Mugabe.

Katibu Mkuu wa Chama cha Maveterani, Victor Matemadanda, alinukuliwa akisema kwamba Mujuru alitumikia Zimbabwe katika nafasi mbalimbali kama waziri kwa miaka 34 na hakuna kiongozi yeyote wa ZANU-PF aliyewahi kumnyooshea kidole kwamba alikuwa na mapungufu, lakini baada ya kuondoka, wanampiga madongo.

Anaanika kwamba vigogo wengi ndani ya ZANU-PF si wasafi katika mambo yao binafsi. “Kumpiga madongo Mujuru ni sawa na kuliambia taifa kwamba katika ZANU-PF hakuna kiongozi aliye msafi kwa kuwa ukiwa ndani ya chama hakuna atakayesema mabaya yako, lakini ukitoka na unakikosoa chama, unakuwa adui,” alikaririwa Matemadanda.

Wakati wa uchaguzi, ZANU-PF kinatumia vyombo vya ulinzi na usalama kuhujumu haki ya raia ya kubadilisha uongozi kwa njia ya sanduku la kura. Wanasaidia kuhujumu demokrasia. Wanawaliza wapinzani kwa kuiba kura kwa njia ya elektroniki wakati wa majumuisho (tallying).

Mchezo hufanyika nyuma ya Tume ya Uchaguzi na waangalizi ambao wanakuwa hawajui kinachoendelea nyuma ya pazia. Mtindo wa zamani wa kuwajaza kura za wizi kwenye masanduku ya kura au kuyaondoa baadhi ya majina kwenye orodha ya wapiga kura hasa katika maeneo ambako walijua kuwa ni ngome ya upinzani, umepitwa na wakati.

Lakini labda si ZANU-PF tu ya Mugabe ni mchezo mchafu ambao unahujumu matakwa ya wananchi ya kufanya mabadiliko. Mchezo huu pia hudumaza demokrasia na kukatisha wananchi tamaa.

Mugabe na umri wake mkubwa, anajiona kuwa ni ‘jongwe’, jogoo pekee katika Zimbabwe akidhani kwamba bila yeye hakuna Zimbabwe. Wako viongozi katika chama tawala hapa nchini ambao kama Mugabe, wanadhani bila Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchi itakwama. Wanasahau kabisa kwamba wao wataondoka, Tanzania itabaki.

Mugabe amesema atagombea tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2018 na anajitapa kwamba yeye ‘ni Mungu’. Anasahau kwamba Mungu ndiye yote katika yote. Na vivyo hivyo kuna baadhi ya viongozi hapa Tanzania, wanatamka wazi kwamba chama chao kitatawala kwa miaka mingine 100, ila wanasahau kwamba dunia inabadilika na kwamba wao hawatakuwapo wakati huo.

Mugabe amepangua pangua uongozi ndani ya ZANU-PF na kuwaweka kando wenye nia ya kumrithi, wengine wakisingiziwa kutaka kumroga! Sasa inazungumzwa wazi wazi kwamba ama atamwachia madaraka mkewe Grace au Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa.

Lakini wakosoaji wanasema amejenga mtandao wa kiukoo ‘Mugabe Dynasty’, ukoo wa watawala kama ilivyo katika nchi za utawala wa kifalme. Siku moja  mwandishi wa habari Mwingereza alimuuliza lini atastaafu, naye akamrushia swali: Malkia wa Uingereza atastaafu lini?

Baadhi ya wanaharakati, wakiongozwa na Mchungaji Evan Mawarire, mwanaharakati anayetaka mabadiliko, ndiye aliyewatia hamasa Wazimbabwe waanze kudai haki zao.

Amejenga fukuto la wananchi linalojulikana kama ‘This Flag’, linaloongozwa na dhamira ya; Why must we be in this situation: Kwanini tuendelee kuwa katika hali hii, wanadai maisha bora na wanataka Mugabe ang’atuke mapema. Lakini yeye anasema muda wake bado na kwamba hapatakuwa na ‘Arab Spring’ nchini Zimbabwe.

Wachunguzi wa mambo nchini Zimbabwe, wanasema ikiwa Mugabe ameshindwa kusoma alama za nyakati. Vyama vya upinzani 18 na wanaharakati wameungana na kumwambia ni wakati mwafaka kuondoka madarakani. Maandamano makubwa yaliyofanyika Ijumaa iliyopita, pamoja na kwamba Mahakama ilitoa amri kwamba yasiingiliwe, polisi waliwatawanya waandamaji kwa mabomu na kusababisha vurugu kubwa katika Mji Mkuu wa Harare.

Kiongozi mwandamizi wa chama cha ZPF, Didymusb Mutasa, alikaririwa akisema Serikali inayojidai kufuata Katiba, inavunja sheria ilizozitunga yenyewe kwa kuanzisha vurugu na kuanza kuwapiga wananchi ambao walikuwa wamekusanyika kwa amani. Viongozi wa vyama vya upinzani wamesema, maandamano hayo yalikuwa ni mwanzo tu. “Tutakuwa mitaani tena Ijumaa ijayo,” alisikika mmoja wao akisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles