30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Hofu ya kushindwa inatatanisha misimamo ya Donald Trump?

trump na hillary

IVUMAYO haidumu na ngoma ikipigwa sana hupasuka ngozi, ni semi zinazoanza kujiakisi katika kinyang’anyiro cha kuingia katika jumba kuu kuliko yote nchini Marekani la White House makao ya Rais wa taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi duniani.

Mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump aliyejizolea umaarufu tangu alipoanza kusaka kuteuliwa anayeshabikiwa na kuchukiwa na wanaomuunga mkono na wanaompinga, taratibu anaanza kuonesha dalili za kuyumba katika kampeni yake ya kuingia Ikulu kutokana na sababu kadhaa zikijumuishwa pamoja na ambazo zinaelekea kutatanisha misimamo yake.

Anaanza kuonesha kubadilika kila baada ya muda akijaribu kuridhisha matakwa ya wanaosimama nyuma yake lakini pia wahafidhina walioko ndani ya chama chake.

Trump ambaye amekuwa akigonga vichwa vya habari kutokana na hulka yake ya kutamka mambo kama yalivyo bila kujali diplomasia, anagubikwa na utashi wa wapambe wake ambao inaelekea nao wamegawanyika wakitaka matakwa yao yatimizwe katika matarajio yao akishakuwa Rais endapo atafanikiwa.

Kwanza aliwakera Wamarekani kwa kubadili msimamo kuhusu hasimu wao Rais Vladimir Putin wa Urusi, kwa kusema kuwa anadhani jimbo la Crimea lililomegwa na Urusi kutoka Ukraine ni halali kuwa la Kisovieti kwa kuwa wakazi wengi wa huko wanavutiwa kuwa upande wa Putin.

Anajaribu kuwajibia matakwa yao watu wa Crimea ambao walipiga kura tatanishi kufikia uamuzi wa kuelemea Urusi, lakini Trump ametoa msimamo huo unaokinzana na mtazamo wake wa awali ili kuridhisha timu yake ya mikakati ya kampeni, ambayo iaundwa na baadhi ya watendaji waliokuwa katika nyadhifa za serikali ya Ukraine iliyoondolewa madarakani ya Rais Viktor Yanukovych aliyeelemea mlengo wa Urusi na kuingia madarakani Rais wa sasa Petro Poroshenko anayeelemea Magharibi.

Lakini msimamo huo wa Trump unakinzana na mtazamo wa chama chake kilichomsimika ambacho kina hulka ya kutatua migogoro kijeshi kwa rekodi za marais waliopita kutoka katika chama hicho walioliongoza taifa hilo akiwemo Ronald Reagan, George Bush Sr na George Walker Bush.

Lakini jambo lingine lililoitikisa kambi ya kampeni ya Trump na yeye mwenyewe ni chama cha Democrat kutatua mivutano yao ya ndani, hususan Ben Sanders alipowekana sawa na Hillary Clinton muda mfupi kabla kusimikwa rasmi kuwa mgombea.

Kitendo ambacho kilirudisha nguvu ya Democrat na kusababisha Hillary kuongoza katika kura nyingi za maoni zinazoonesha kuwa kama uchaguzi ukifanyika sasa, amemuacha mbali Trump na timu yake ambao ni kama walijisahau kuhusu karata hiyo turufu ya Democrats waliyoitumia hata wakati Barack Obama anatafuta kuingia Ikulu.

Wakati huo mkongwe wa chama hicho Rais wa zamani, Bill Clinton alionesha kutomuunga mkono Obama na kusababisha mgawanyiko wa msimamo wa wafuasi wa Democrat, lakini akaja kujitokeza katika kampeni na kudai kuwa anamuunga mkono na awali alimpinga si kwa kuwa alimshinda mkewe katika kutafuta kusimikwa kugombea bali kimsimamo.

Kilichofuata baada ya hapo ni Obama kumteua Hillary kuhudumu katika wadhifa wa tatu kwa ukubwa wa Waziri wa Nje, turufu ambayo Republican wamejaribu kuitumia bila mafanikio wakishikia bango kashfa ya matumizi ya barua-pepe binafsi kwa masuala nyeti ya kiofisi suala lililofunikiwa kombe na FBI na kumfanya Clinton apete.

Trump akaibuka na turufu ya kuwatetea mno Wamarekani wenye asili ya Kiafrika ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kunyanyapaliwa na polisi wa Kizungu, akidai kuwa Obama si mweusi mwenzao kwenye nafasi kwani ameshindwa kuwalinda bali yeye mweupe ndiye mweusi mwenzao kwenye nafasi atakayesimamia vyema mustakabali wao.

Katika kura za maoni zilizogawanywa katika makundi matatu katika mvuto wa vyama, Democrats wanaongoza na katika wagombea wenyewe kura ya mwisho ya maoni inaonesha Hillary amefikia kilele cha asilimia 54 dhidi ya 47 za Trump.

Ni mara moja tu mnamo Juni mwaka huu ndipo Trump alimkaribia zaidi Hillary kwa asilimia 48 dhidi ya 54 za mpinzani wake. Pengine ni hali hiyo ndiyo inayoanza kumbadilisha lugha Trump anayetangatanga kwenye misimamo.

RAS INNO,+ 255 624 124 987

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles