23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mtifuano CUF una ‘mkono wa tatu’

Profesa Ibrahim Lipumba, akiingizwa ukumbini na maofi sa wa polisi katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CUF hivi karibuni.
Profesa Ibrahim Lipumba, akiingizwa ukumbini na maofisa wa polisi katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CUF hivi karibuni.

NA MWANDISHI MAALUMU,

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinapita kwenye wakati mgumu sana tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992. Mwaka 1994 kiliingia katika mgogoro wa uongozi na kumfukuza aliyekuwa mwenyekiti wake wa kwanza, James Mapalala pamoja na viongozi wengine 28.

Mgogoro wa sasa pia umeishia kuwafukuza viongozi waandamizi, Magdalena Sakaya, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma na wajumbe kadhaa wa Baraza Kuu na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba. Wengine waliofukuzwa na Baraza Kuu ni pamoja na Shashi Lugeye, ambaye alikuwa Katibu wa Baraza la Wazee na Abdul Kambaya (Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano). Wengine ni Wajumbe wa Baraza Kuu, Masoud Mhina, ambaye pia ni Katibu wa CUF wa Wilaya ya Handeni.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo katikati ya pilikapilika za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 akidai kwamba nafsi yake ilikuwa inamsuta kutokana na uteuzi wa Edward Lowassa kuteuliwa kubeba bendera ya Chadema kwa niaba ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Lowassa alijiunga na Chadema baada ya kutoswa na Chama Cha Mapinduzi katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya urais.

Baada ya uchaguzi, Profesa Lipumba aliandika barua ya kuifuta barua yake ya awali na kutaka arejee kwenye nafasi yake ya uenyekiti, jambo ambalo lilizua vurugu kwenye mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho uliofanyika Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.  Kundi moja liliunga mkono hoja ya kukataa kurejea kwa Lipumba na jingine likiunga mkono hoja ya kumrejesha.

Waliofukuzwa ni dhahiri kwamba wako upande wa Lipumba na bahati mbaya wote wanatoka Tanzania Bara. Hii ina maana CUF kimegawanyika kwa misingi ya Uzanzibari na Utanganyika, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa chama hicho. CUF hakina nguvu sana Bara ikilinganishwa na Zanzibar, ngome yake kuu ikiwa Kisiwani Pemba.

Kundi la Lipumba linawatuhumu wenzao wa Zanzibar kwamba wana ubaguzi. Kundi hilo linasema chama hicho kilikubali kumrejesha Duni Haji Duni katika chama na kumrejesha kwenye wadhifa wa Ujumbe wa Baraza la Uongozi bila masharti yoyote na kinamkataa Lipumba kwa kisingizio cha kukisaliti chama kilipokuwa katika harakati za uchaguzi. Duni Haji Duni alijiuzulu uanachama na kuteuliwa na Chadema kuwa mgombea mwenza wa Lowassa.

Kufukuzwa uanachama Sakaya, Naibu Katibu Mkuu  ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua na Maftah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini ambaye amesimamishwa uanachama, inaonekana kuna mkono wa tatu nyuma yake.

Hali ya utata iliyoonekana kwenye Mkutano wa CUF pale ofisa wa polisi aliposhiriki kumwingiza kwa nguvu Profesa Lipumba kwenye mkutano ambao hakuwa mjumbe inaonekana ni mbinu ya kukidhoofisha chama hicho.

Hata hivyo, kuendelea au kutoendelea kwa Sakaya na Nachuma kuwa wabunge, kunategemea busara ya Spika Job Ndugai, ambaye ana uzoefu wa kesi za namna hiyo kwani alikuwa Naibu Spika katika Bunge lililopita na anajua jinsi mtangulizi wake, Anne Makinda alivyoshughulikia suala la Hamad Rashid Mohamed na anaweza kuwaruhusu  wahusika kuendelea na ubunge wao hadi mwisho wa uhai Bunge mwaka 2020.

Endapo Spika hataridhia kufukuzwa kwa Sakaya, atakuwa amefuata mfano wa mtangulizi wake, Anne Makinda, ambaye alitoa msimamo kwamba Bunge halihusiani na migogoro ya vyama.

CUF walimfukuza uanachama aliyekuwa Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, lakini aliendelea kuwa Mbunge baada ya kupeleka shauri Mahakama Kuu ya Tanzania na kufungua kesi ya kumfuta uanachama, kesi ambayo iliisha uhai wa Bunge la 10 mwaka 2015.

Lakini sakata hili la CUF ni tofauti na lile lililomkuta aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye alivuliwa uanachama na Kamati Kuu ya Chadema mwaka 2013.

Zitto pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Kitila Mkumbo, walidaiwa kuandaa mipango ya siri ya kumwondoa madarakani Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Kama Sakaya na Nachuma watavuliwa ubunge, litakuwa pigo kwa upinzani ambao tayari umedhoofishwa na fukuza fukuza ya baadhi ya wabunge machachari kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge, ikiwamo kikao  ambacho kinaanza Dodoma mwezi ujao.

Lakini inaelekea fukuza fukuza hiyo imegonga ukuta, kwa sababu kikao cha Baraza Kuu kiliketi Zanzibar na hakikuwashirikisha wajumbe kutoka Bara, jambo ambalo huenda likawa ni baraka kwa Sakaya na Nachuma kuendelea na ubunge wao.
Katibu Mkuu wa CUF, Seif Hamad Sharif anatuhumiwa kuendesha chama kidikteta, anayoamua yeye ndiyo anataka yafuatwe kwa kuwa waliotangazwa kufukuzwa uanachama isipokuwa Shashi Lugeye, hawakupewa nafasi ya kujitetea.

Vinginevyo, Sakaya, ambaye alikuwa Mbunge Viti Maalumu kwenye Bunge la 10, ikiwa hatakwenda mahakamani kupinga kufukuzwa kwake uanachama wa CUF, atakosa sifa ya kuwa mbunge.

Hili la fukuza fukuza linaashiria ni mtifuano wa uongozi na kupimana nguvu. Wanachama wa CUF kutoka Bara inaelekea hawapendezwi na yaliyojiri kwenye kikao cha Baraza Kuu Zanzibar, ni hatua ya viongozi wanaotaka Zanzibar kuwa kitovu cha uwamuzi wa chama hicho kama Dodoma ilivyo kitovu cha uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi. Wazanzibari wamekuwa wakilalamika kwamba mambo wanayoamua kuhusu Zanzibar, hupinduliwa yakifika Dodoma.

Mgogoro huu ndani ya CUF umekuja wakati usio mwafaka, kwa kuwa chama hicho hakina uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi, Zanzibar kwa sababu chama hicho kilisusa uchaguzi wa marudio wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles