24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Fukuto la urais Zanzibar

 ANDREW MSECHU– DAR ES SALAAM

WAKATI taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, suala la urais Zanzibar limekuwa miongoni mwa mambo muhimu yanayotazamwa kwa undani, hasa kutokana na historia ya mvutano wa muda mrefu ndani ya visiwa hivyo.

Safari hii, mvutano unaanzia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinatarajiwa kusimamisha mgombea mpya, baada ya rais wa sasa, Dk. Mohamed Shein kumaliza muda wake wa miaka 10. 

Kutokana na hali hiyo taarifa kutoka ndani ya CCM zinaeleza kwamba siri ya mgombea wa urais wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar imebaki ndani ya mioyo ya viongozi wakuu wa chama hicho, waliokutana jijini Dodoma wiki iliyopita chini ya Rais Dk. John Magufuli.

katika kikao hicho mbali na Rais Magufuli pia kilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally.

Kwa mujibu wa historia ya uchaguzi Visiwani Zanzibar zilitawaliwa na mizengwe na hata kuzua malalamiko hasa kwa upande wa Maalim Seif Sharif Hamad ambaye sasa amehamia Chama cha ACT-Wazalendo akitokea CUF.

Safari hii, wakati vyama vya upinzani vikiendelea kuangalia namna ya kuingia katika ushirikiano, mjadala umeanza kuibuka baada ya Chadema kutangaza kufungua milango kwa wanachama wanaotajakutangaza kuwania urais Zanzibar, hasa baada ya chama hicho kikuu cha upinzani kutangaza kufungua milango kwa ajili ya mazungumzo ya ushirikiano na vyama vingine.

Mjadala huo, unaibuka kutokana na taarifa kuwa Maalim Seif tayari ametangaza nia yake ya kuwania kwa mara nyingine urais wa visiwa hivyo, safari hii nakisubiri uteuzi wa chama chake kipya.

Maalim Seif ambaye amekuwa mwanasiasa mwenye nguvu wa upinzani Zanzibar, ndiye anayetarajiwa huenda akawa mgombea kupitia ushirikiano wa vyama hivyo, iwapo vitafikia makualiano.

Hatua ya Chadema kutangaza kufungua milango kwa wanachama wake kujitokeza kuwania nafasi hiyo, inatafisiriwa ni ya kuingiza vuguvugu linaloweza kuleta mvutano iwapo watajitokea wanachama wake wenye nguvu, hasa itakapokuja hatua ya kufikiwa makubaliano katika ushirikianokuhusu mgombea wa pamoja.

Kwa sasa, ushirikiano wa vyama unategemea zaidi makubaliano baina ya vyama vya upinani vyenye nguvu, hasa Chadema na ACT Wazalendo ambavyo vinatarajiwa kuwa wasimamizi wa mchakato huo, hasa baada ya Chama cha Wananchi (CUF) chini ya Mwenyekiti wake,Profesa Ibrahim Lipumba kuonyesha kutokuwa na imani baada ya kujitoa katika iliyokuwa Ukawa.

MSIMAMO ACT WAZALENDO

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana kuhusu msimamo wa chama chake, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema ni kweli wamewasikia Chadema wamezindua mchakato wa kutia nia kwenye ngazi ya urais wa Zanzibar na kuangalia ushirikiano baina ya vyama.

Alisema pia wamewasikia wakizindua mchakato kama huo kwa Zanzibar, anachoweza kusema ni kwamba Chadema ni chama cha siasa chenye haki zote za kujipanga na kufanya siasa.

“Katika kipindi cha uchaguzi kama hiki, inatarajiwa Chadema wana haki ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi, ikiwemo kuandaa wagombea wake wa ngazi zote na eneo lolote la Jamhuri ya Muungano waTanzania, ikiwamo Zanzibar. Chadema wana haki na wanachokifanya ni kitu ambacho kinapaswa na kinaweza kufanywa na chama chochote cha siasa.

“La pili, tumemsikia Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akisema milango ya ushirikiano iko wazi,mimi katibu mkuu baada ya kusikia kauli hii siku moja tu baada ya kutolewa, nilimwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema kumweleza jinsi ambavyo ACT Wazalendo, tumeipokea kwa mikono miwili na kumuonyesha utayari wetu wa ushirikiano.

“Nilimweleza tuko tayari sasa mchakato huo kuanza na muda wote tumekuwa tukisema ACT Wazalendo, tunaamini katika ushirikiano kwa sababu ndiyo silaha pekee ya kuhakikisha CCM inatolewa madarakani mwaka 2020,” alisema Shaibu. 

Alisema anaamini iwapo wataweza kushikamana kwa pamoja na kuweka kando tofauti za kiitikadi, wana fursa kubwa ya kuiondoa CCM madarakani kwa sababu anaiona ya sasa ni dhaifu maradufu. 

Shaibu alisema wanahitaji kushikamana ili kuwakomboa Watanzania kwa sababu uchumi wa nchi umevurugwa, haki za binadamu zinavurugwa, wanahitaji kuwa na mshikamano utakaoiondosha CCM madarakani na kuwakomboa Watanzania ili waweze kupata maendeleo.

Alisema jambo kubwa katika mambo ya ushirikiano, ni utayari kwa hiyo kama Chadema wameonesha na wametangaza mchakato sasa unaweza kuanza na ACT Wazalendo pia wameonesha utayari na wamewajibu kwa barua, hatua inayoonesha wanakoenda ni kuzuri. 

“ACT Wazalendo, tuna matumaini makubwa katika muda uliopo bado tuna uwezo wa kutengeneza vuguvugu kubwa litakalohakikisha tunakwenda kwenye uchaguzi tukiwa kwenye mshikamano,” alisema.

Alisema kuhusu uteuzi wa wagombea, wamejipanga na hatua ya kwanza Mei,mwka huu, walitangaza wanachama wao wanaotaka kujitokeza kwenye nafasi za udiwani na ubunge watangaze nia.

Alisema wanachama wengi zaidi ya 200 mpaka sasa wametangaza nia za kugombea nafasi za ubunge.

“Katikati ya Juni, mwaka huu, tutazindua rasmi mchakato wetu wa kuchukua fomu, kurejesha fomu, kura za maoni na mchakato wetu wa uteuzi wa wagombea wa ngazi za udiwani ubunge na urais wakati utakapofika,” alisema.

Alisema unapozungumzia umoja lazima uwe umoja wa vyama kwanza makini, pili vyenye dhamira ya dhati ya kuiondosha CCM na kuwakomboa Watanzania ili wapate maendeleo, kwa hiyo si suala la kuwa umoja wa vyama kwa sababu ya jina tu, hiki ni chama cha upinzani, lazima chenyewe kikisimana kijinasibishe kwa uwazi.

“Sisi tunaamini na nina imani Watanzania wanafahamu tuna wanachama wengi makini kote, Tanzania bara na visiwani wanaoweza kushika nafasi kubwa za uongozi katika urais na urais wa Zanzibar, ubunge na udiwani katika uchaguzi wa mwaka huu,” alisema.

KAULI YA CHADEMA

Akitoa ufafanuzi kuhusu hatua ya chama chake kuamua kufungua milango kwa ajili ya kutafuta mgombea urais wa Zanzibar, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema anaamii halitavuruga mchakato wa ushirikiano.

Alisema hatua ya Chadema kuendelea na mchakato wa kufungua milango kwa ajili ya wagombea ngazi zote ni suala la maandalizi ya ndani ya chama, ambalo kila chama tayari kinaendelea na michakato yake ya ndani.

“Ninaamini hii haiwezi kuathiri makubaliano ya ushirikiano yatakapofikiwa kwa sababu kuna suala la kuangalia namna ya kuagawana maeneo na nafasi kama ilivyokuwa kwa Ukawa mwaka 2015.

 “Itakapotokea chama fulani katika vilivyomo kwenye makubaliano ya ushirikiano, kina nguvu eneo fulani au mtu wake ana nguvu katika nafasi fulani tutazunguma na kuangalia mazingira mazuri ya kupeana nafasi katika ngazi zote,” alisema. 

Alilikiri kupokea barua ya ACT Wazalendo na tayari wamewajibu, sasa wanasubiri tu kuanza utaratibu wa mazungumzo kuhusu namna ya kushirikiana.

“Tunaendelea kufanya tathmini ya vyama vilivyo na utayari na kuelekea kwenye ushirikiano na tutaangalia namna ya kuanza vikao kwa ajili ya kufikia makubaliano,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles