27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Faraji Ali Kilumanga nembo ya mashujaa waliosahaulika

Marehemu Faraji Ali Kilumanga.
Marehemu Faraji Ali Kilumanga.

SIJUI kama hakuna watu ambao hawamfahamu Nina Simone mwimbaji maarufu wa Marekani na duniani. Kila nikimsikiliza, moyo wangu unashikwa na huzuni na majonzi. Anaimba na kuingiza katika nyimbo zake kila maovu watu weusi waliyofanyiwa Marekani.

Ni sauti inayobeba machozi mengi na miaka mingi ya kunyanyaswa, kudanganywa, kudharauliwa, kutukanwa na kutumiwa kama mtumwa. Marehemu Nina Simone anaonyesha kupitia muziki wake picha halisi ya jinsi watu na hasa kutoka tamaduni zetu, tunavyoishi.

Kukubalika katika jumuiya kwa mambo unayofanya na mchango wako kutambulika si jambo rahisi. Wanaughaibuni hatuna jinsi ila ni kuendelea tu kupambana na mazingira haya mpaka tutambulike kwamba mchango wetu kweli unaleta manufaa kwa Taifa.

Asikudanganye mtu, maisha ya Ughaibuni si rahisi, wengi wananyimwa na maisha yao kukamilika kwa sababu ya rangi ya ngozi yako, hii si kusema kwamba hakuna mafanikio, yapo wakati mfumo unafanya kazi kama ilivyolengwa kufanya bila ya kuingiliwa na kukwamishwa na watu wenye hisia mbaya.

Kuna watu wanaishi kupigania na kupigana kuweka usawa. Maisha yao yote ni kushindana na mfumo ambao hauwatendei haki. Kwa sisi Wanaughaibuni baada ya kuona jinsi wenzetu wanavyojitahidi kuweka hiyo misingi inayoleta fursa na maendeleo kwa wananchi wa nchi wanazoishi na Wanaughaibuni kwa kiu kubwa sana wanataka hivyo hivyo.

Nyumbani, kwa Wanaughaibuni, ni ngome ya mwisho bila kuwa na mawasiliano na ngome hiyo maisha ya Ughaibuni hayana maana. Kuimarisha hiyo ngome ni kuja na ujuzi na maarifa hata kama ni madogo ukilinganisha na michango mikubwa ya kimataifa.

Wakati namsikiliza Nina Simone anaimba na kuelezea kwenye nyimbo zake mapambano na changamoto anazozikuta Ughaibuni na jinsi anavyoiona nchi ambayo alipozaliwa haimtaki na haimkubali, inanipeleka mbali sana tofauti tu ni kwamba mapenzi yanayotukuta nyumbani ni makubwa.

Wakati unarudi kijijini unaona na kustaajabu jinsi mapokezi na upendo unavyotiririka, unaona jinsi ulivyokuwa na kiu na hamu ya wapendwa wako.

Upendo kwa Tanzania ni kwamba Wanaughaibuni wanao na wanataka kuuonyesha kwa vitendo, Stockholm sasa hivi matayarisho yanaendelea kutoa mchango wao kusaidia waathirika wa maafa yaliyowapata ndugu zetu wa Kagera.

Makamu wa Jumuiya ya Watanzania Sweden (Tanriks), Norman Jason na Katibu wake, Seynab Haji, wako mbioni kutayarisha na kuweka mikakati ya kukusanya mchango wetu kwa ndugu zetu wa Kagera. Hakuna mtu Ughaibuni ambaye hili jambo halijamgusa.

Dunia imepoteza mashujaa wengi, wengi wao walijitolea wakiwa wanajua kwamba maisha yao yalikuwa hatarini. Mmoja wao alikuwa Mzee Faraji Ali Kilumanga. Inanisikitisha kwamba mpaka sasa amepotea katika kurasa za historia. Marehemu Faraji Ali Kilumanga amefia kazini wakati anatumikia Taifa lake, anakumbukwa na wachahe.

Mashuja hawa wanasahaulika bila kuimbwa kwenye nyimbo za kishujaa, matendo mengi ya kishujaa ambayo muda unapita bila ya kukumbuka mchango wao kama watu binafsi au kama kundi.

Sisi wazawa wa Tanzania ambao tunaishi Ughaibuni tunao mchango kama huu, na kuhangaika kwetu ni bila malipo mara nyingi tunafanya kazi nyingi sana za kujitolea, yote ni kwa sababu tunapenda jumuiya yetu na tunaona mafanikio ya jumuiya hiyo ni mafanikio ya wote.

Taasisi ya Diaspora itasaidia kuweka miundombinu ambayo itarahisisha sisi kujipanga na kuweza kusaidia nyumbani bila ya matatizo. Hiyo barabara kuu itatuwezesha kuratibu shughuli zote za Diaspora na kuhamasisha wengine kutumia mfumo huo kuwekeza na kusaidia katika kujenga nchi.

Mifano gani ambayo tunaweza kuleta hapa kama si mifano ya sisi wenyewe. Ni kazi ngumu kuhamasisha watu kama mapenzi hayapo kwenye mioyo yao. Ni rahisi kuelezea dira na maono kwa wale ambao wana kiu ya kutaka kusaidia nchi yao na wale ambao wanaelewa kwamba kama tutaendelea ni kwa kushikana na kushirikiana.

Baadhi ya watu hawaoni kuna kupata chochote kutoka kwa Wanaughaibuni na hii inatokana na kutokuelewa kwamba hata kama tunaishi nje, lakini sisi wakati wote ni sehemu ya jumuiya zetu Tanzania.

Watanzania mpaka sasa Ughaibuni tumepeleka misaada moja kwa moja kwa walengwa kama ndugu na jamaa, lakini kupitia mfumo ambao umewekwa kurahisisha mawasiliano kati ya sisi tunaoishi nje na ndugu zetu, inaleta mambo mengi ya kimaendeleo.

Jambo moja litazaa jingine na hivyo hivyo. Tusiogope kuwa mashujaa, tusiogope kujitahidi kuumia mwanzoni, kwani hakuna mahali maendeleo yamepatikana bila ya kuwa na kafara ya namna moja au nyingine. Watu wanajitolea kwa sababu vizazi vijavyo vipate nafuu. Tuweke mazingira yakae sawa ili tuweze kufanikisha malengo yetu.

Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyakusudia.

Tengo Kilumanga Email: [email protected] Tel: +467051263303 Twitter: @tengo_k

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles