23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hukumu ya Bageni ilivyodhihirisha kuwa taifa lina mpasuko

Christopher Bageni
Christopher Bageni

Na DEUS KIBAMBA,

KATIKA habari zenye kishindo wiki hii, ni taarifa ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kigogo mzito katika Jeshi la Polisi na ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP), Christopher Bageni.

Bageni amepata hukumu hiyo katika Mahakama ya Rufani kutokana na rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutokubaliana na kuachiwa kwake huru.

Bageni na wenzake kadhaa, akiwemo Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam zamani, ACP Abdallah Zombe, walikwa wakikabiliwa na kesi ya kuwaua wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ifakara wakiwa na dereva teksi mkazi wa Manzese mwaka 2006.

Baada ya miaka 10 ya vuta nikuvute kuhusu ukweli wa sakata hilo, hatimaye Mahakama ya Rufani wiki iliyopita imemkuta Bageni na hatia ya kuwaua Watanzania wasio na hatia.

Kwa majina ni Ephraim Chigumbi, Savings Chigumbi na Mathias Lunkombe. Pamoja na hao, Bageni amekutwa na hatia ya kumuua dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha wafanyabiashara hao kwa jina la Juma Ndugu ambaye alikufa akiwa katika harakati za kutafuta maisha katika kazi yake ya udereva teksi ambayo alikuwa akiifanyia maeneo ya Manzese.

Wanne hao waliuliwa kinyama kwa kupigwa risasi  Januari 14, 2006 siku ambayo ilikuwa ya majonzi kwa ndugu, jamaa na familia za marehemu pamoja na Watanzania wapenda haki, amani na utulivu.

Katika hatua ya sasa, hakuna habari kubwa sana juu ya hukumu ya Bageni ya kunyongwa hadi kufa au hata ya kuachiwa huru kwa Zombe ambaye alivuma sana katika kesi hiyo.

Suala kubwa hapa ni jinsi kesi hii ilivyoendeshwa na jinsi hukumu yenyewe ilivyopokewa. Kwa hakika, taifa la Tanzania limeonesha mpasuko mkubwa wa kiimani na kimaono kutokana na kesi hii. Na kama kawaida ya kesi nzito kama hizi, kulikuwa na mvuto mkubwa kila mara kesi yenyewe ilipokuwa inatajwa kiasi kwamba Bageni, Zombe na maafisa wengine waliokuwa nao katika kesi hii akiwemo Rajabu Bakari na Ahmed Makelle walikuwa katika masononeko.

Ilifikia wakati kulikuwa na hisia kuwa bila kujali hukumu itakuwaje, Bageni na wenzake wangepaswa kupatiwa msaada mkubwa wa kisaikolojia ili kupambana na hali iliyowakuta.

Wakati hayo yakitokea kwa Bageni na maofisa wenzake wa Polisi, familia za ndugu wanne waliokatishwa maisha yao kabla ya muda waliopangiwa na Mungu zilikuwa katika majonzi.

Upo wakati pande moja ilikuwa ikitamani kesi hiyo iishe na watuhumiwa watakaopatikana na hatia wapate stahili yao ya kifo vile walivyowafanyia wafanyabiashara wale wasio na hatia.

Kwa upande mwingine, kulikuwa na watu waliotoa rai kwa maafisa wale wa Polisi kuachiwa huru kama hawana kesi ya kujibu kwa kuwa kuendelea kuwaweka rumande kama mahabusu kwa miaka yote hiyo tangu 2006 ilionekana kuwa ni kuwaathiri kisaikolojia, kijamii na nyanja nyinginezo.

Nilichojifunza ni kwamba Watanzania wengi wasio wabobevu katika masuala ya sheria, wanadhani kuwa kesi ni kama blanketi, likiwepo litafunika wote na likikosekana baridi ni kwa kila mtu. Ukweli ni kwamba mahakamani lolote linawezekana, watuhumiwa wote, wachache au hata mmoja wanaweza kukutwa na hatia. Inaonekana Watanzania waligawanyika kati ya wale waliotegemea maafisa wote wanne watiwe hatiani na upande wa pili uliotegemea watuhumiwa wote waachiwe huru.

Kesi hii pia imekuwa ngumu katika minajiri ya vyombo vya Kiserikali kutofautiana. Ilifika wakati Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka walitofautiana katika maono ya kesi hii. Tazama ingawa DPP na Polisi wote hufanya upelelezi kwa kiwango fulani, Mkurugenzi wa Mashtaka alitofautiana na suala la kuachiwa huru kwa watuhumiwa wote wanne hadi kufikia kukata rufaa.

Kwa Watanzania wengi, jambo hili limeishangaza dunia ikizingatiwa kuwa wakati mwingi DPP amekuwa akilaumiwa kwa kuchia watuhumiwa katika mazingira ambayo wengi walitatanishwa kwa kutumia kanuni ya taifa kutokuwa na masilahi katika kesi husika (nolle prosequi), lakini katika kesi hii, DPP alionekana kusisitiza kuwa kulikuwa na kila mazingira ya kumtia hatiani mtuhumiwa angalau mmoja kwa kosa la kuwaua wafanyabiashara wale wanne.

Hakika kesi hii imeonesha pia kuwa katika masuala ya kutafuta haki, kukata tamaa ni kitu kibaya sana! Dhana ya haki iliyocheleweshwa ni haki iliyopotea imeingia katika mtihani mkubwa sana.

Ndani ya mahakama zenyewe, kumetokea mpasuko wa kitaaluma. Baada ya hukumu ya Mahakama Kuu kuwaachia huru watuhumiwa, imewashangaza wengi hasa miongoni mwa wasio wasomi wa masuala ya sheria kwamba Mahakama ya Rufani imemtia hatiani Bageni kwa mauaji.

Kwa tuijuayo kazi ya Mahakama vema, si jambo la ajabu hata kidogo kwa Mahakama kutofautiana katika ngazi ya Mahakama Kuu na ya rufani kuhusu jambo lolote.  Kwa kweli, dhana ya rufaa katika mahakama ina maana kwamba kunaweza kuwa na utofauti wa maamuzi katika mahakama ya juu dhidi ya hukumu ambayo ilikuwa tofauti katika mahakama ya chini.

Pamoja na yote hayo, Watanzania wamegawanyika kati ya wale wanaoona kuwa mahakama katika ngazi hii au nyingine ilitenda haki zaidi kuliko nyingine. Huo nao ni mpasuko mwingine!

Miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu, pia nako kuna mpasuko. Kwa kesi hii na nyingine zilizowahi kuhukumu adhabu ya kifo, wapo watetezi wa haki za binadamu wanaoona kuwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ina mapungufu makubwa kuendelea kutoa adhabu ya kinyongo mpaka kufa kwa mtu aliyeua.

Katika utetezi wao, hawa wanatoa hoja kuwa lengo la sheria ni kurekebisha. Kwa sababu hiyo, watetezi hawa wanauliza kumnyonga mtu ni kumrekebisha? Pia, watetezi wa mrengo huu wanaona kuwa kutoa adhabu ya kifo kwa aliyeua ni kurudia kosa la mkosaji. Mtu ameua, taifa nalo linaua? Wanahoji! Kwa upande wao, mtu aliyeua anapaswa kuadhibiwa kwa adhabu nyingine yoyote isipokuwa kifo.

Kwa mtazamo wao, watetezi wa aina hii watataka adhabu ya kifo iondolewe katika sheria zetu za Tanzania. Wakati wa Mchakato wa Katiba mpya, taifa lilionesha mpasuko kuhusu suala la adhabu ya kifo pale walipoibuka Watanzania walioamini katika dhana ya jino kwa jino na wale walioamini katika dhana ya kusamehe wakosaji, huku wao wakishauri kuwa mtu aliyeua anahitaji msaada ili ajute, ajirekebishe, abadilike na awe mtu mwema ambaye hatakuja fikiria kuua tena milele. Kama hili lingekuwa linatekelezwa, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ingepaswa kurekebishwa ili kufuta adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala hata kama ni kifungo cha maisha.

Kikatiba, watetezi hawa wa haki za binadamu wanaitaja ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ulinzi wa hoja ya kuwa kila mtu anayo haki ya kuishi.

Aidha, ibara ya 12, 13 na 15 zinatajwa pia kuwa na mwelekeo wa kuvunjwa kama tunaendelea kunyonga watu waliokosa. Kwa mujibu wa ibara hizo za Katiba, kila mtu huzaliwa huru na anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Swali hapa ni je, kumnyonga mtu ni kutambua na kuthamini utu wake? Jambo moja dhahiri linaloonesha mpasuko ni kwamba pamoja na utetezi huo, Katiba imeshindwa kukataza au kufuta adhabu ya kifo kama adhabu halali na hata katika mchakato wa Katiba mpya, jambo hili limedhihirisha kutugawa kiasi kikubwa mno.

Kwa upande wa pili, kuna watetezi wa Haki za Binadamu pia ambao kwa uchungu wa kutaka kukosesha mauaji ya Watanzania wasio na hatia kama vile wale wenye ulemavu wa ngozi yaani albino wanaona kuwa adhabu ya mauaji ibaki kuwa kunyongwa, tena mpaka kufa. Kwa maoni ya wataalamu wa taasisi kama Under the Same Sun, adhabu ya kifo ikiondolewa katika mwenendo wa adhabu, nchi yetu inaweza kushuhudia mauaji makubwa zaidi ya watu wanaoishi na ualbino pamoja na wazee au vikongwe kwa kisingizio cha uchawi.

Kwa sababu hiyo, lipo kundi la Watanzania, tena si dogo linalolilia adhabu ya kifo ibaki kama adhabu halali, huku wakitaka pia adhabu hiyo iwe inatekelezwa ikishatolewa badala ya hali ya sasa ambapo kwa awamu takribani tatu sasa za uongozi wa nchi, Rais amekuwa akisita kusaini adhabu hiyo kutekelezwa.

Inasemekana Rais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli hawajawahi kusaini mtu yeyote kunyongwa.

Kwa hakika, suala la adhabu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa kwa kachero Bageni wa Jeshi la Polisi si tu ni pigo kwake, familia yake na Jeshi zima la Polisi bali limezua ubishani mkubwa na mgawanyiko katika taifa zima.

Aidha, hukumu hii imeonekana kuhuisha mjadala wa adhabu ya kifo ambao kila ulipoibuka uliligawa taifa kati ya wanaoiunga mkono na wanaoipinga kwa nguvu zote.

Kwa maoni yangu, suala hili linastahili kura ya maamuzi ya taifa zima ili ijulikane kwamba kwa wakati huu, adhabu ya kifo itafutwa! Natoa pole kwa wafiwa wa ndugu wanne mwaka 2006 na wafiwa watarajiwa wa kachero huyu wa Polisi, kwa kuwa kwa hali ya sasa upenyo wa kutonyongwa kwake uko katika mikono ya rais ama kutosaini adhabu hiyo itekelezwe!

Mwandishi ni Mhadhiri wa Masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia na Haki za Binadamu. Amesomea masuala ya Sheria za Kimataifa.Pia nii Mwenyekiti wa JUKWAA LA KATIBA TANZANIA na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Taarifa Kwa Wananchi (TCIB).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles