29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Kikwete alivyoitikisa Malawi-4

img_3605

MARA ya mwisho tuliona sehemu ya hotuba hii ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete iliyokuwa ikitoa ufafanuzi juu ya suala zima la mpaka baina ya Tanzania na Malawi.

Hebu tuendelee na hotuba hiyo ambayo ni sehemu ya mwisho.
Kwa maana halisi ya Mkataba wa Heligoland tangu Julai Mosi, 1890, wananchi wa upande wa Tanzania wamekuwa wanakunywa, kuoga, kuvua samaki na kusafiri katika maji ya Ziwa yasiyokuwa yao bali ya nchi nyingine.

Na kwa kuwa wamekuwa wanafanya hivyo bila ya kupata kibali cha Malawi wamekuwa wanaiba maji na samaki wa Malawi na kusafiri isivyo halali katika nchi ya watu.  Jambo hili haliingii akilini hata kidogo.  Ndiyo maana tunadai haki yetu stahili.

Na hiyo pia, ndiyo maana busara na hekima ya Sheria ya Kimataifa kuhusu mpaka wa kwenye maji kuwa katikati.  Sheria hii inazingatia hali halisi ya maisha ya jamii inayozunguka ziwa ambayo imekuwa inalitegemea maisha yao yote kwa shughuli zao za kuwapatia uhai na maendeleo yao.

Haiwezekani kuwatenganisha watu waishio kando ya Ziwa Nyasa kumiliki na kutumia maji hayo na rasilimali zake.  Hawataelewa wala kukubali kuambiwa kuwa wanatumia maji na rasilimali za ziwani kwa hisani ya nchi ya Malawi.

Kwa watu waliokuwepo tangu Mungu anawaumba wao na wenzao wa ng’ambo ya pili, si sawa na si haki hata kidogo kuwafanyia hivyo.  Kwa kweli ni unyanyasaji wa hali ya juu.  Ndiyo maana wazee wetu walidai suala hili liwekwe sawa wakati wa ukoloni, kabla na baada ya Uhuru.  Na ndiyo maana na sisi tunafuata nyayo zao katika madai haya ya haki.

Kuna mambo mengine mawili ambayo yanatufanya tudai haki ya kumiliki na kutumia Ziwa Nyasa.  La kwanza ni ule ukweli kwamba mito mingi ya Tanzania nayo inachangia kujaza maji katika ziwa.  Iweje leo maji yanayojaza ziwa ni jambo jema, lakini yakishaingia ziwani, ziwa hilo si mali yao wenye mito hiyo tena na wakiyatumia wanaiba mali ya watu wengine.

Hivi kweli ndivyo wanavyostahili kufanyiwa watu wanaotunza vyanzo vya mito hiyo na kuruhusu maji yake kutiririka na kuingia ziwani?

Jambo la pili ni kwamba mpaka wa Tanzania na Malawi kuwa ufukweni kunafanya ukubwa wa nchi zetu kuwa haujulikani kwa uhakika.  Unategemea mabadiliko kutokana na kuja na kupungua kwa maji ziwani.  Kunafanya mpaka wa nchi kuwa hautabiriki na unaweza kuwa tatizo siku moja mbele ya safari.

Isitoshe kuwa na nchi isiyojulikana ukubwa wake nalo ni tatizo la aina yake.  Ndiyo maana mpaka kuwa katikati ya ziwa ni bora zaidi.

Kama nilivyokwishasema, chimbuko la mzozo huu ni mkataba wa Heligoland ambao umepanda mbegu ya fitina baina ya nchi zetu.  Bahati mbaya sana Tume ya Mipaka haikumaliza kazi ya kuhakiki mipaka yote ya nchi yetu na majirani zake kufuatia kuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza mwaka 1914.

Ujerumani ikashindwa vita na koloni lake kuwa sehemu ya himaya ya Uingereza.  Bahati mbaya kwetu Waingereza waliotawala nchi zetu mbili tangu 1918 hawakuchukua hatua za kurekebisha mpaka kabla ya uhuru wa nchi zetu.

Ni maoni yetu kuwa nchi zetu sasa zifanye kile ambacho hakikufanywa na Tume ya Mipaka ya wakoloni,  Waingereza na Wajerumani.  Tukifanye sisi wenyewe kama nchi mbili huru kwa njia ya mazungumzo.
Bahati mbaya majaribio ya mwaka 1967 hayakufanikiwa.  Bahati nzuri kufuatia uamuzi wa kijasiri wa marehemu Rais Bingu wa Mutharika nchi zetu sasa zinazungumza.

Bado hatujafikia muafaka kuhusu kurekebisha mpaka na huenda ikatuwia vigumu kufikia muafaka.  Jambo linaloleta faraja, hata hivyo ni kuwa sote wawili tumekubaliana kuwa tutafute mtu wa kutusuluhisha.
Hayo ndiyo matokeo ya mazungumzo ya Tume yetu ya pamoja tangu ngazi ya Wataalamu, Makatibu Wakuu mpaka kwa Mawaziri, katika vikao vya Mzuzu na Lilongwe kati ya Agosti 20 – 27, 2012.  Katika mkutano wao wa Agosti 27, 2012 Mawaziri husika wa nchi zetu chini ya uongozi wa pamoja wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Ephraim Chiume na mwenzake wa Tanzania, Bernard Membe, wameafiki mapendekezo hayo.

Aidha, wamekubaliana kuwa pande zote mbili wakutane tena Dar es Salaam kati ya Septemba 10 – 15, 2012 kukubaliana juu ya usuluhishi wa aina gani unafaa.
Mtakubaliana nami kuwa tumepiga hatua muhimu kuelekea kwenye kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili.  Hata hivyo, bado safari ni ndefu na huenda ikawa na magumu mengi.  Maombi yangu kwa viongozi na wananchi wa Tanzania na Malawi ni kuendelea kuunga mkono jitihada hizi.  Tuwaunge mkono wataalamu na Mawaziri wetu ili wafanikishe vizuri jukumu lao.

Tuzingatie na kuheshimu walichokubaliana Lilongwe kuwa viongozi na wananchi wa nchi zetu wajiepushe na kutoa kauli au kufanya vitendo vinavyoweza kuchafua hali ya hewa, kuleta uchochezi na kuathiri majadiliano yanayoendelea.
Nawasihi Watanzania wenzangu kuzingatia ushauri na rai hiyo ya Mawaziri na wataalamu wetu, ili kuwe na mazingira mazuri ya mazungumzo na kuwezesha mzozo huu kuisha kwa amani na kirafiki.
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kusisitiza kuwa si makusudio yangu wala ya Serikali yetu kutafuta suluhisho la suala hili kwa nguvu ya kijeshi.

Nawahakikishia Watanzania wenzangu kuwa hatuko vitani na Malawi na wala hakuna maandalizi ya vita dhidi ya jirani zetu hawa kwa sababu ya mzozo wetu wa mpaka katika Ziwa.  Ondoeni hofu na endeleeni na shughuli zenu za ujenzi wa taifa letu kama kawaida.

Nilimhakikishia hivyo Rais wa Malawi, Joyce Banda nilipokutana naye Maputo, Msumbiji Agosti 18, 2012.  Tanzania haina mpango wa kuingia vitani na Malawi.  Mimi na wenzangu Serikalini tunaona kuwa fursa tuliyoitafuta miaka mingi ya kukaa na ndugu zetu Malawi kuzungumzia suala hili lenye maslahi kwetu sote sasa tumeipata.

Hatuna budi kuitumia ipasavyo.  Naamini, tukifanya hivyo, inaweza kutufikisha pale tunapopataka. Ni muhimu, kwa ajili hiyo kwa pande zetu mbili, kuipa fursa ya mazungumzo nafasi ya kuendelea bila ya vikwazo visivyokuwa vya lazima.

Kwa sababu hiyo basi, napenda kutumia nafasi hii kuwasihi ndugu zetu wa vyombo vya habari na wanasiasa wenzangu tuepuke kauli au matendo yatakayovuruga mazungumzo na kuchochea uhasama kati ya nchi zetu mbili jirani na rafiki.

Kuna manufaa makubwa ya kumaliza mzozo wetu kwa njia ya mazungumzo kuliko kwa njia ya vita.  Kufikiria sasa kutumia njia nyinginezo hasa za nguvu za kujeshi, si wakati wake muafaka.

Aidha, tukitumia njia ya vita, badala ya kuwa tumepata suluhisho inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa mgogoro mpana zaidi.  Tuendelee kuwaunga mkono wawakilishi wetu katika tume yetu ya pamoja.  Naahidi, Serikali itakuwa inawapa taarifa kadiri mazungumzo yetu na wenzetu wa Malawi yatakavyokuwa yanaendelea.  Nina hakika tutamaliza salama.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa Kunisikiliza

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles